1 Wakorinto 7

Unyumba.

1Mambo, mliyoniandikia, nayajibu hivi: Ni vizuri, mtu asipogusa mwanamke.

2Lakini kwa ajili ya ugoni kila mtu awe na mkewe mwenyewe, hata kila mwanamke awe na mumewe mwenyewe.

3Mume ampe mkewe yampasayo, naye mke ampe mumewe yayo hayo.

4Mke siye mwenye mwili wake, ila mumewe; vilevile naye mume siye mwenye mwili wake, ila mkewe.

5Msinyamane, isipokuwa mmepatana kukaa hivyo kitambo kidogo, mjipatie siku za kufunga na za kuomba. Kisha mwandamane tena, Satani asipate kuwajaribu, kwani hamwezi kuvumilia pasipo kukoma.

6Haya nayasema, kama ninavyoyatambua mimi, lakini siyo ya kuagiza.

7Kupenda napenda, watu wote wawepo kama mimi mwenyewe; lakini kila mtu amegawiwa na Mungu kipaji chake yeye, mmoja hivyo, mwenzake hivyo.[#Mat. 19:12.]

Kuachana.

8Lakini wasiooa na wajane nawaambia: Itawafalia, wakikaa kama mimi.

9Lakini kama hawawezi kujivumiliza, na waoe. Kwani kuoa ndiko kuzuri kuliko kuchomwa na tamaa.[#1 Tim. 5:14.]

10Nao waliokwisha oana nawaagiza, tena si mimi, lakini ni Bwana: Mke asiachane na mumewe![#1 Kor. 7:12,25,40; Mat. 5:32.]

11Lakini mke akiwa ameachana na mumewe, sharti akae pasipo kuolewa au apatanishwe tena na mumewe! Naye mume asiachane na mkewe!

12Nao wengine nawaambia mimi, si Bwana: Aliye ndugu akiwa na mke asiyemtegemea Mungu, naye mkewe anapenda kukaa naye, asimwache!

13Naye mwanamke akiwa na mume asiyemtegemea Mungu, naye mumewe anapenda kukaa naye, asimwache mumewe!

14Kwa maana mume asiyemtegemea Mungu hutakaswa na mkewe; naye mke asiyemtegemea Mungu hutakaswa naye aliye ndugu. Ikiwa sivyo, watoto wenu wangekuwa wachafu, lakini sasa wametakata.[#Rom. 11:16.]

15Lakini wale wasiomtegemea Mungu wakitaka kuvunja unyumba, na wauvunje! Hapo aliye ndugu, akiwa mume au akiwa mke, hakuna kifungo tena kinachomzuia; kwani ninyi Mungu amewaitia mapatano.[#Rom. 14:19.]

16Kwani wajuaje, wewe mke, kama utamwokoa mumeo? Au wajuaje, wewe mume, kama utamwokoa mkeo?[#1 Petr. 3:1.]

17Kwa hiyo nasema: Kila mtu avishike, Bwana alivyomgawia, kila mtu aendelee hivyo, alivyokuwa hapo, Mungu alipomwita! Hivyo ndivyo, ninavyoagiza katika wateule wote.[#1 Kor. 7:20,24.]

18Mtu akiitwa alipokwisha kutahiriwa asivifiche! Mtu akiitwa akiwa hajatahiriwa, asitahiriwe!

19Kule kutahiriwa siko, nako kutotahiriwa siko, ila kuyashika maagizo ya Mungu ndiko.[#Gal. 5:6; 6:15.]

20Kila mtu hivyo, alivyokuwa alipoitwa, na akae vivyo hivyo![#1 Kor. 7:17,24.]

21Kama ulikuwa mtumwa ulipoitwa, usivionee uchungu! Lakini ukiweza kujikomboa jikomboe![#Ef. 6:8.]

22Kwani mtumwa aliyeitiwa kuwa wa Bwana amekwisha kukombolewa na Bwana. Vivi hivi mwungwana aliyeitwa ni mtumwa wa Kristo.[#Ef. 6:6; File. 16.]

23Mmenunuliwa pakubwa. Msiwe tena watumwa wa watu![#1 Kor. 6:20.]

24Ndugu zangu, kila mtu hivyo, alivyokuwa hapo alipoitwa, sharti akae vivyo hivyo kwa Mungu![#1 Kor. 7:17,20; Gal. 3:28.]

Wanawali.

25Kwa ajili ya wanawali sikupata agizo la Bwana, ninawaambia, ninayoyatambua kwa hivyo, nilivyogawiwa na Bwana kuwa mwelekevu.[#1 Kor. 7:10,40; 1 Tes. 2:4; 1 Tim. 1:12-13.]

26Nionavyo kuwa vizuri, ni hivi: kwa ajili ya shida hii, tuliyo nayo inamfaa mtu kukaa hivyo, alivyo:[#1 Kor. 7:29; 10:11.]

27ukiwa umejifunga kuwa na mke usitafute kufunguliwa! Usipokuwa umejifunga kuwa na mke usitafute mke!

28Lakini hata ukioa hukosi, naye mwanamwali akiolewa hakosi. Lakini wafanyao hivyo huipatia miili maumivu, nayo ndiyo, mimi ninayoyataka kuwaponya

29Lakini nasema hivi, ndugu zangu: Siku zimepunguka. Hapo panaposalia nao wenye wake sharti wawe, kama hawana! Nao wenye kulia wawe kama wasiolia![#Luk. 14:26; Rom. 13:11.]

30Nao wenye furaha wawe kama wasiofurahi! Nao wenye kununua wawe, kama hawana kitu!

31Nao wenye kuvitumia vya ulimwengu huu wawe, kama wanajitumilia bure tu! Kwani ulimwengu huu, jinsi ulivyo sasa, unatoweka.[#1 Yoh. 2:15-17.]

32Nataka, msipatwe na masumbuko. Asiyeoa huyasumbukia mambo ya Bwana, apate kumpendeza Bwana.

33Aliyeoa huyasumbukia mambo ya ulimwenguni, apate kumpendeza mkewe; hivyo amekwisha kugawanyika.[#Luk. 14:20; Ef. 5:29.]

34Nayo ya mke na ya mwanamwali ni yaleyale: mke asiye na mume naye mwanamwali huyasumbukia mambo ya Bwana, apate kutakata mwilini na rohoni. Lakini mwenye mume huyasumbukia mambo ya ulimwenguni, apate kumpendeza mumewe.

35Lakini haya nayasema, kwa kuwa yanawafaa; siyasemi, niwategee kitanzi, ila nayasemea kwamba: Yenu yote yaendelee, kama yapasavyo, mfulize kumkalia Bwana pasipo kuzuiliwa.

36Lakini mtu akiona, ya kama haimfai mwanawe wa kike, akiwa mtu mzima pasipo kuolewa, -nayo hufikia hapohapo-, basi, na afanye, kama atakavyo! Hakosi, na amwoze!

37Lakini aliyeushikiza moyo wake ukashupaa vizuri, usiteseke, yuko na nguvu ya kuyashinda mapenzi yake mwenyewe; basi, mtu aliye hivyo akijipa moyo wa kumkataza mwanawe wa kike kuolewa, atafanya vizuri.

38Hivyo amwozaye mwanawe wa kike anafanya vizuri, lakini asiyemwoza mwanawe wa kike anafanya vizuri kumpita yule.

39Mke yuko na mwiko siku zote za kuishi kwake mumewe; lakini mumewe anapokufa, amefunguliwa kuolewa naye ye yote, ampendaye, ikiwa tu, kama Bwana atakavyo.[#Rom. 7:2.]

40Lakini vitakavyomfaa kupita hivi ni kukaa hivyo, alivyo. Hivyo ndivyo, nionavyo mimi; lakini najiwazia, ya kwamba nami ninayo Roho ya Mungu.[#1 Kor. 7:25.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania