1 Wakorinto 8

Nyama za tambiko.

1Mambo ya nyama za tambiko twayajua kwamba: Sote tumeyatambua; tena: Utambuzi huleta majivuno, lakini upendo hujenga.[#1 Kor. 8:4; Tume. 15:29.]

2Lakini mtu akijiwazia, ya kuwa amekwisha kutambua kitu, basi, yeye hajautambua bado utambuzi upasao.[#Gal. 6:3.]

3Lakini mtu akimpenda Mungu, huyo ametambuliwa naye.[#Gal. 4:9.]

4Kwa ajili ya kula nyama za tambiko tunajua: hakuna, kinyago kifaliacho humu ulimwenguni, tena hakuna aliye Mungu pasipo mmoja.[#1 Kor. 10:19; 5 Mose 6:4.]

5Kweli viko viitwavyo miungu, kama vya mbinguni au vya ulimwenguni, kwa hiyo miungu yao ni mingi nao mabwana zao ni wengi,[#Sh. 136:2-3; Rom. 8:38-39.]

6lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja, ni Baba. Yote yametoka kwake, nasi tu watu wake. Tena Bwana ni mmoja, Yesu Kristo; vyote viliumbwa naye yeye, hata sisi tumeumbwa naye.[#1 Kor. 12:5-6; Ef. 4:5-6; Kol. 1:16.]

7Lakini sio wote walio wenye utambuzi huu. Kwa hivyo, walivyozoea kutambikia mizimu, hata sasa wako wanaozila zile nyama, zikiwa za tambiko, lakini mioyo yao iliyo minyonge huchafuliwa kwa kujua maana.[#1 Kor. 10:27.]

8Tena hakuna, vyakula vinavyotupatia kwake Mungu. Ikiwa tukila, hakuna tunachoongezewa; ikiwa hatuli, hakuna tunachopungukiwa.[#Rom. 14:17.]

9Mwangalie tu, matumio yenu yasikwaze wanyonge!

10Maana wewe uliyeyatambua hayo ukikaa hapo, wanapotambikia mizimu, ule nyama machoni pa mwenzio aliye mnyonge kwa kutojua maana vema, je? Hatahimizwa moyoni mwake, mpaka naye azile nyama zile za tambiko?[#Gal. 5:13.]

11Hivyo kwa ajili ya utambuzi wako mnyonge anaponzwa, naye ni ndugu, ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake.[#Rom. 14:15.]

12Mkiwakosea ndugu hivyo na kuiponza mioyo yao iliyo minyonge kwa kutojua maana vema, basi, mnamkosea Kristo mwenyewe.

13Kwa hiyo, chakula kikimkwaza ndugu yangu, sitakula nyama kale na kale, maana nisimkwaze ndugu yangu.[#Rom. 14:21.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania