1 Wakorinto 9

Matumio yampasayo mpiga mbiu.

1Je? Mimi sikukombolewa? Mimi si mtume? Mimi sikumwona Bwana wetu Yesu Kristo? Nanyi ham kazi yangu, niliyomfanyizia Bwana?[#1 Kor. 15:8; Tume. 9:3-5; 22:17; 26:16.]

2Nisipokuwa mtume wa wengine, lakini ninyi ndimi mtume wenu. Kwani ninyi m muhuri inayoujulisha utume wangu, ya kuwa ni wa Bwana.[#1 Kor. 4:15; 2 Kor. 3:2-3.]

3Makanio yangu kwao wanaoniulizauliza ndiyo haya ya kwamba:[#Luk. 10:8.]

4Je? Hatuna ruhusa ya kula na ya kunywa yo yote?

5Hatuna ruhusa pote, tunapokwenda, kuchukua na mke aliye ndugu, kama wanavyofanya mitume wengine na ndugu za Bwana, hata Kefa?[#Mat. 8:14; Yoh. 1:42.]

6Au labda mimi na Barnaba peke yetu hatuna ruhusa ya kuwapo pasipo kazi?

7Yuko askari aendaye vitani na kujilipa mwenyewe? Yuko mpanda mizabibu asiyekula matunda yao? Au yuko mchunga kundi asiyetumia maziwa ya kundi kuwa kitoweo?

8Haya nayasema kimtu? Maonyo nayo hayayasemi yayo hayo?

9Kwani imendikwa katika Maonyo ya Mose:

Ng'ombe mwenye kupura ngano usimfunge kinywa! Hapo Mungu anataka kuwapatia ng'ombe?

10Hapasemi kabisa kwa ajili yetu sisi? Kweli imeandikwa kwa ajili yetu sisi kwa kufaa, mkulima alimie kingojeo, naye mwenye kupura apurie kingojeo cha kugawiwa.

11Kama sisi tumewapandia ya kutunza roho, ni vikubwa gani, sisi tukivuna yenu ya kutunza miili?[#15:27.]

12Ikiwa wengine wamepata ruhusa ya kula matumio yenu, hayatupasi sisi kuliko wale? Lakini hatukuitumia hiyo nguvu yetu, ila twayavumilia yote, kwamba Utume mwema wa Kristo tusiuzuie kamwe.[#Tume. 20:34-35; 2 Kor. 11:9.]

13Hamjui, ya kuwa hao watumikiao Patakatifu hula yatokayo Patakatifu? Nao wachinja ng'ombe za tambiko hugawiwa fungu lao hapo chinjioni?[#4 Mose 18:8,31; 5 Mose 18:1-3.]

14Vivyo hivyo naye Bwana aliwaagiza watangazaji wa Utume mwema, wajilishe huo Utume mwema.[#Luk. 10:7.]

15Lakini mimi sikuyatumia mambo hayo hata moja. Nami sikuyaandika haya, kwamba yanitimilie hivyo; maana ningependa kufa kuliko kutenguliwa hilo tukuzo langu.[#Tume. 18:3.]

16Kwani nikiipiga hiyo mbiu njema sinalo la kujivunia, maana nitashurutishwa. Kwani nisipoipiga hiyo mbiu njema ningepatwa na mambo.

17Kwani nikiyafanya kwa kuyapenda, napata mshahara; lakini nikiyafanya pasipo kupenda, nako ndiko kuutimiza utunzaji niliopewa.[#1 Kor. 4:1.]

18Basi, mshahara wangu ndio nini? Ni huu: nautangaza Utume mwema pasipo upato, nisiyatangue matumio yangu yaliyomo katika huo Utume mwema.[#1 Kor. 8:9.]

Paulo mtumwa wao wote.

19Maana mimi niliyekombolewa katika utumwa wote nimejigeuza kuwa mtumwa wao wote, kusudi walio wengi niwapate, wanifuate.[#Mat. 20:26-27.]

20Kwao walio Wayuda nimekuwa kama Myuda, niwapate Wayuda. Kwao wenye miiko nimekuwa kama mwenzao mwenye miiko, tena miiko sinayo, ni kwamba tu, niwapate wenye miiko nao.[#Tume. 16:3; 21:20-26.]

21Kwao wasiojua maonyo nimekuwa kama mwenzao asiyejua maonyo, tena sipo pasipo Maonyo yake Mungu, kwani nayakalia Maonyo yake Kristo; huko ni kwamba tu, niwapate nao wasiojua maonyo.[#Gal. 2:3.]

22Kwao walio wanyonge nimekuwa kama mnyonge mwenzao, niwapate walio wanyonge nao. Hivyo wote nimejifananisha nao katika mambo yo yote, nipate po pote wenye kuokoka.[#Rom. 11:14; 2 Kor. 11:29.]

23Hayo nayafanya yote kwa ajili ya Utume mwema, nami nipate kugawiwa bia yake.

Mashindano.

24*Hamjui: Penye mashindano wote hupiga mbio, lakini atakayepewa tunzo ni mmoja tu? Nanyi pigeni mbio hivyo, kusudi mpewe![#Fil. 3:14; 2 Tim. 4:7.]

25Lakini kila aendaye kushindania hujinyima yote; hao hujinyima, wapewe kilemba kiangamiacho, lakini ninyi mjinyime, mpewe kilemba kisichoangamika![#2 Tim. 2:4-5; 1 Petr. 5:4.]

26Basi, nami napiga mbio hivyo, si kama sijui, ninavyokimbilia; napigana, lakini si kama anayejipigia tu.

27Ila nauponda mwili wangu, mpaka nguvu zake ziishie kama za mtumwa, maana mimi ninayetangazia wengine nisije kuwa mwenye kutupwa.*[#Rom. 8:13; 13:14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania