1 Wafalme 21

Ahabu na Izebeli wanamwua Naboti.

1Hayo yalipokwisha kufanyika, kulikuwa na mtu wa Izireeli, ndiye Naboti; alikuwa na shamba la mizabibu huko Izireeli karibu ya jumba la Ahabu, mfalme wa Samaria.

2Ahabu akamwambia Naboti: Nipe shamba lako la mizabibu, liwe langu, nipapande mboga! Kwani ni karibu ya nyumba yangu. Nami mahali pake nitakupa shamba la mizabibu lililo zuri zaidi, au kama unapendezwa, nitakupa fedha kuwa malipo yake.

3Naboti akamwambia Ahabu: Bwana na anizuie, nisikupe fungu langu, nililolipata kwa baba zangu!

4Ahabu akaenda nyumbani mwake mwenye moyo uliokasirika na kuchafuka kwa ajili ya hilo neno, Naboti wa Izireeli alilomwambia kwamba: Sitakupa fungu langu, nililolipata kwa baba zangu. Akaja kulala kitandani pake, akauelekeza uso ukutani, akakataa kula chakula.

5Ndipo, mkewe Izebeli alipoingia mwake, akamwambia: Mbona roho yako inakasirika, ukakataa kula?

6Akamwambia: Nimesema na Naboti wa Izireeli, nikamwambia: Nipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au kama unapendezwa, nitakupa shamba jingine la mizabibu mahali pake; naye akajibu: Sitakupa shamba langu la mizabibu.

7Mkewe Izebeli akamwambia: Sasa wewe sharti uonyeshe, ya kuwa ndiwe mfalme wa Waisiraeli; inuka, ule, nao moyo wako na utulie! Mimi nitakupa shamba la mizabibu la Naboti wa Izireeli.

8Akaandika barua katika jina la Ahabu, akaitia muhuri ya mfalme, akaituma hiyo barua kwa wazee na kwa wakuu wa mji waliokaa humo na Naboti.

9Akaandika humo baruani kwamba: Tangazeni mfungo, naye Naboti mwekeni kuwa mkuu wa watu!

10Kisha wekeni kila kando yake watu wawili wasiofaa, wapate kumsingizia kwamba: Amemtukana Mungu na mfalme. Kisha mtoeni mjini, mmpige mawe, afe![#2 Mose 22:28; Iy. 1:5.]

11Wazee na wakuu waliokaa naye katika mji wake wakafanya hivyo, kama Izebeli alivyowatuma, kama vilivyoandikwa katika ile barua, aliyoituma kwao.

12Wakatangaza mfungo, wakamweka Naboti kuwa mkuu wa watu.

13Wakaja watu wawili wasiofaa kitu, wakakaa kando yake, kisha hao watu wasiofaa kitu wakamsingizia Naboti mbele ya watu kwamba: Naboti amemtukana Mungu na mfalme; kwa hiyo wakamtoa nje ya mji, wakampiga mawe, mpaka akifa.

14Kisha wakatuma kwake Izebeli kumwambia: Naboti amepigwa mawe, akafa.

15Izebeli aliposikia, ya kuwa Naboti amepigwa mawe, akafa, Izebeli akamwambia Ahabu: Haya! Litwae shamba la mizabibu la Naboti wa Izireeli, alilokataa kukupa kwa fedha! Kwani Naboti hayupo, kwani amekwisha kufa.

16Ikawa, Ahabu aliposikia, ya kuwa Naboti amekufa, Ahabu akaondoka kushuka kwenye shamba la mizabibu la Naboti wa Izireeli, aje kulitwaa.

Elia anamfumbulia Ahabu yatakayompata.

17Kisha neno la Bwana likamjia Elia wa tisibe kwamba:

18Inuka, ushuke kumwendea Ahabu, mfalme wa Isiraeli, aliye huko Samaria! Utamwona katika shamba la mizabibu la Naboti, alikokwenda kulichukua.

19Umwambie kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Kumbe umeua, kisha ukazitwaa mali za mfu? Kisha umwambie kwamba: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Mahali pale, mbwa walipoilamba damu ya Naboti, palepale mbwa watailamba nayo damu yako wewe.[#1 Fal. 22:38.]

20Ndipo, Ahabu alipomwambia Elia: Je? Umeniona, wewe mchukivu wangu? Akajibu: Nimeona, ya kuwa umejiuza kuwa mtumwa wa mambo yaliyo mabaya machoni pa Bwana, uyafanye.

21Utaniona, nikikuletea mabaya, nikuzoe. Kweli nitawatowesha wa Ahabu walio wa kiume, kama watakuwa wamefungwa, au kama watakuwa wamefunguliwa kwao Waisiraeli.[#2 Fal. 9:7-8.]

22Nitautoa mlango wako kuwa kama mlango wa Yeroboamu, mwana wa Nebati, na kama mlango wa Basa, mwana wa Ahia, kwa ajili ya hayo machafuko, uliyonichafukisha kwa kuwakosesha Waisiraeli.[#1 Fal. 15:29; 16:11-12.]

23Kwa ajili yake Izebeli Bwana akasema kwamba: Mbwa watamla Izebeli katika mfereji wa mji wa Izireeli.[#2 Fal. 9:33-36.]

24Wao wa Ahabu watakaokufa mjini mbwa watawala; nao watakaokufa shambani madege wa angani watawala.[#1 Fal. 14:11; 16:4.]

25Kweli hakuwako mtu kama Ahabu aliyejiuza hivyo kuwa mtumwa wa mambo yaliyo mabaya machoni pa Bwana, ayafanye; ni kwa kuwa mkewe Izebeli alimpoteza.

26Akatapisha sana kwa kuyafuata magogo ya kutambikia na kuyafanya yote, Waamori waliyoyafanya, Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Isiraeli.

27Ikawa, Ahabu alipoyasikia hayo maneno akazirarua nguo zake, akajivika gunia mwilini pake, akafunga mfungo; hata kulala akalala na kuvaa gunia, akawa akijiendeaendea na kunyamaza kimya.

28Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Elia wa Tisibe kwamba:

29Umeona, ya kuwa Ahabu amejinyenyekeza machoni pangu? Kwa kuwa amejinyenyekeza machoni pangu, sitayaleta yale mabaya katika siku zake, lakini katika siku za mwanawe nitauletea mlango wake yale mabaya.[#2 Fal. 9:26.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania