1 Wafalme 3

Ndoa ya Salomo.

(1-4: 2 Mambo 1:1-6.)

1Salomo akaingia udugu na Farao, mfalme wa Misri, akimwoa binti Farao, akamwingiza mjini mwa Dawidi, mpaka akiisha kuijenga nyumba yake na Nyumba ya Bwana na boma la kuuzunguka Yerusalemu.[#5 Mose 23:7.]

2Lakini watu walikuwa wakitambika vilimani, kwani Jina la Bwana halijajengewa nyumba bado mpaka siku hizo.

3Salomo akampenda Bwana, kwa hiyo akaendelea kuyafuata maongozi ya baba yake Dawidi, lakini naye alikuwa akitambika vilimani na kuvukizia huko.

Matambiko na maombo ya Salomo.

(5-15: 2 Mambo 1:7-12.)

4Mfalme akaenda Gibeoni kutambika huko, kwani hicho kilikuwa kilima kikuu cha kutambikia juu yake; Salomo akatoa ng'ombe elfu za tambiko za kuteketezwa nzima hapo pa kutambikia.[#1 Mambo 21:29.]

5Usiku huo Bwana akamtokea Salomo katika ndoto huko Gibeoni, Mungu akamwambia: Omba kwangu, uyatakayo, nikupe![#1 Fal. 9:2.]

6Salomo akasema: Wewe ulimfanyizia mtumishi wako baba yangu Dawidi mambo ya upole mwingi, kwa kuwa alifanya machoni pako mwenendo wenye kweli na wongofu kwa moyo uliokunyokea; nawe hukuacha kumtolea huo upole mwingi, ukampa mwana anayekaa katika kiti chake cha kifalme, kama vilivyotokea leo hivi.[#1 Fal. 1:48.]

7Sasa Bwana Mungu wangu, wewe umempa mtumishi wako kuwa mfalme mahali pa baba yangu Dawidi, nami nikingali mwana mdogo bado, sijui penye kutoka wala penye kuingia.

8Tena mtumishi wako yuko katikati yao walio ukoo wako, uliouchagua, nao ni watu wengi wasiowezekana wala kuhesabiwa wala kuwangwa kwa kuwa wengi.[#1 Fal. 4:20.]

9Kwa hiyo mpe mtumishi wako moyo wenye kutii, nipate kuwaamua walio ukoo wako na kuyatambua yaliyo mema nayo yaliyo mabaya! Kwani yuko nani anayeweza kuwaamua walio ukoo wako ulio wenye watu wengi?[#Sh. 143:10.]

10Neno hili likawa jema machoni pa Bwana, kwa kuwa Salomo ameomba neno kama hilo.

11Ndipo, Mungu alipomwambia: Kwa kuwa umeomba neno kama hilo, ukaacha kuomba siku nyingi za kuwapo, wala hukujiombea mali nyingi, wala hukutaka kufa kwa adui zako, ukajiombea utambuzi wa kusikia mashauri,

12tazama, nimekwisha kufanya, kama ulivyosema. Tazama, nimekupa moyo wenye werevu wa kweli na utambuzi. Kwa hiyo mtu kama wewe hakuwako mbele yako, wala hataondokea nyuma yako atakayekuwa kama wewe.[#Fano. 2:3-6.]

13Nayo usiyoyaomba nimekupa, kama mali nyingi na utukufu; kwa hiyo mtu kama wewe hatakuwako katika wafalme siku zako zote za kuwapo.[#Fano. 3:13-16; Mat. 6:33.]

14Kama utaendelea katika njia zangu na kuyaangalia maongozi yangu na maagizo yangu, kama baba yako Dawidi alivyoendelea, nitakupa hata siku nyingi za kuwapo.

15Salomo alipoamka akaona, ya kuwa ameota; alipofika Yerusalemu, akaja kusimama mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, akatoa ng'ombe za tambiko za kuteketezwa nzima, akatengeneza nazo ng'ombe za tambiko za shukrani, akawafanyia watumishi wake wote karamu.

Salomo anastaajabisha kwa kukata shauri.

16Siku zile wakaja wanawake wagoni wawili kwa mfalme, wakasimama mbele yake.

17Mwanamke mmoja akamwambia: E bwana wangu, mimi na huyu mwanamke tunakaa katika nyumba moja, mimi nikazaa mtoto mle nyumbani, nilimo naye.

18Ikawa siku ya tatu ya kuzaa kwangu, huyu mwanamke akazaa naye, nasi tulikuwa pamoja mle nyumbani, hamna mgeni tena pamoja nasi, ni sisi wawili peke yetu mle nyumbani.

19Basi, usiku mtoto wake huyu mwanamke akafa, kwa kuwa alimlalia.

20Kisha akaamka usiku wa manane, akamchukua mtoto wangu kitandani kwangu, kijakazi wako alipolala usingizi, akamweka kifuani kwake, naye mtoto wake mfu akamweka kifuani kwangu.

21Asubuhi nilipoamka kumnyonyesha mtoto wangu, nikimtazama, amekufa. Kulipokucha vema, nikamchungulia sana, nimtambue, nikamwona, ya kuwa si mtoto wangu, niliyemzaa.

22Ndipo, yule mwanamke mwingine aliposema: Sivyo! Mtoto wangu ndiye aliye mzima, naye mtoto wako ndiye aliyekufa. Lakini yule akasema: Sivyo! Mtoto wako ndiye aliyekufa, naye mtoto wangu ndiye aliye mzima. Wakabishana hivyo mbele ya mfalme.

23Mfalme akasema: Huyu anasema: Mtoto huyu aliye mzima ni wangu, naye aliyekufa ni mtoto wako. Naye mwenziwe anasema: Sivyo! Mtoto wako ndiye aliyekufa, naye mtoto wangu ndiye aliye mzima.

24Kisha mfalme akasema: Nileteeni upanga! Walipoleta upanga mbele ya mfalme,

25mfalme akasema: Mkateni huyu mtoto mzima, atoke vipande viwili! Huyu mpeni kipande, naye mwingine kipande!

26Ndipo, yule mwanamke aliyekuwa mamake mtoto aliyeishi aliposema kwa kumwonea mtoto wake uchungu, akamwambia mfalme: E bwana wangu, mpeni mtoto mzima, msimwue kabisa! Lakini yule mwingine akasema: Asiwe wangu wala wako; haya! Mkateni![#Yes. 49:15.]

27Ndipo, mfalme alipojibu akisema: Mpeni yule mtoto, akiwa mzima, msimwue kabisa! Yeye ni mama yake.

28Waisiraeli wote wakasikia, mfalme alivyolikata lile shauri, wakamwogopa mfalme, kwani wameona, ya kuwa moyoni mwake umo werevu wa Kimungu wa kuwaamulia watu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania