2 Mambo 1

Salomo anatambika Gibeoni.

(1-6: 1 Fal. 3:1-4.)

1Salomo, mwana wa Dawidi, akajipatia nguvu katika ufalme, naye Bwana Mungu wake akawa naye, akampa ukuu uliozidi.[#1 Fal. 2:12,46.]

2Ndipo, Salomo alipowaita Waisiraeli wote, wakuu wa maelfu na wa mamia na waamuzi na watukufu wa Waisiraeli wote waliokuwa vichwa vya milango,

3wakaenda, yeye Salomo pamoja na huo mkutano wote, kilimani kwa Gibeoni, kwani ndiko, lilikokuwa Hema la Mkutano la Mungu, Mose, mtumishi wa Bwana, alilolitengeneza nyikani.[#1 Mambo 16:39; 21:29.]

4Lakini Sanduku la Mungu Dawidi alikuwa amelitoa Kiriati-Yearimu, akaliweka hapo, alipolitengenezea yeye Dawidi, kwani alilipigilia hema Yerusalemu.[#1 Mambo 13:6; 15:3,28; 16:1.]

5Lakini meza ya shaba ya kutambikia, aliyoitengeneza Besaleli, mwana wa Uri, mwana wa Huri, ilikuwa huko mbele ya Kao lake Bwana; ndiyo, Salomo na mkutano waliyoiendea.[#2 Mose 38:1-8; 2 Mambo 1:3.]

6Salomo akamtambikia Bwana huko juu ya ile meza ya shaba iliyokuwa penye Hema la Mkutano, akatoa ng'ombe elfu za tambiko za kuteketezwa nzima juu yake hiyo meza.

Maombo ya Salomo.

(7-12: 1 Fal. 3:5-15.)

7*Usiku huo Mungu akamtokea Salomo, akamwambia: Omba kwangu, uyatakayo, nikupe!

8Salomo akamwambia Mungu: wewe ulimfanyizia baba yangu Dawidi mambo ya upole mwingi, ukanipa kuwa mfalme mahali pake.

9Sasa Bwana Mungu, neno lako, ulilomwambia baba yangu Dawidi, na litiwe nguvu, litimie! Kwani wewe umenipa kuwa mfalme wa watu walio wengi kama mavumbi ya nchi.

10Sasa nipe werevu wa kweli, nipate kujua penye kutoka mbele ya watu hawa na penye kuingia! Kwani mimi ni mtu gani wa kujua kuwaamua hawa watu wengi walio ukoo wako?

11Ndipo, Mungu alipomwambia salomo: Kwa kuwa jambo kama hili limo moyoni mwako, ukaacha kuniomba mali na mapato mengi na utukufu na kufa kwa wachukivu wako, wala hukuniomba siku nyingi za kuwapo, ila umejiombea werevu wa kweli, upate kujua, jinsi utakavyowaamua walio ukoo wangu, niliokupa, uwe mfalme wao,

12kwa hiyo umekwisha kupewa werevu wa kweli na ujuzi, tena nitakupa mali na mapato mengi na utukufu, wasioupata wafalme wote waliokuwako mbele yako, nao watakaokuwako nyuma yako hawatayapata.*

13Kisha Salomo akaondoka kilimani kwa Gibeoni, akaja Yerusalemu akitoka kwenye Hema la Mkutano, akawa mfalme wa Waisiraeli.

Mali za Salomo.

(14-17: 1 Fal. 10:26-29.)

14Salomo akakusanya magari na wapanda farasi, hata akawa na magari 1400 na wapanda farasi 12000, akawakalisha katika miji ya magari namo mwake mfalme mle Yerusalemu.

15Mfalme akajipatia fedha na dhahabu kuwa nyingi mle Yerusalemu kama mawe, nayo miti ya miangati akajipatia kuwa mingi kama mitamba katika nchi ya tambarare.[#2 Mambo 9:27.]

16Nao farasi, Salomo aliokuwa nao, walitoka Misri, wachuuzi wengi wa mfalme waliwaleta wengi wakiwanunua na kuzilipa bei zao.

17Magari, waliyoyatoa Misri na kuyapeleka kwao, moja lilikuwa fedha 600, na farasi mmoja fedha 150.

18Vivyo hivyo waliwapelekea nao wafalme wote wa Wahiti na wafalme wa Ushami kwa mikono yao.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania