The chat will start when you send the first message.
1Rehabeamu alipofika Yerusalemu, akaikusanya milango ya Yuda na ya Benyamini, watu 180000 waliochaguliwa kupiga vita, wapigane na Waisiraeli, wamrudishie Rehabeamu ufalme huo.
2Lakini neno la Bwana likamjia Semaya aliyekuwa mtu wa Mungu, kwamba:
3Mwambie Rehabeamu, mwana wa Salomo, mfalme wa Wayuda, nao Waisiraeli wote walioko katika nchi ya Yuda na ya Benyamini kwamba:
4Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Msipande kwenda kupigana na ndugu zenu! Rudini kila mtu nyumbani kwake! Kwani jambo hili limefanywa na mimi. Walipoyasikia maneno haya ya Bwana wakarudi wakiacha kumwendea Yeroboamu.
5Rehabeamu alipokaa Yerusalemu akajenga miji yenye maboma katika nchi ya Yuda.
6Akajenga maboma Beti-Lehemu na Itamu na Tekoa,
7na Beti-Suri na Soko na Adulamu,
8na Gati na Maresa na Zifu,
9na Adoraimu na Lakisi na Azeka,
10na Sora na Ayaloni na Heburoni; hii ndiyo miji yenye maboma katika nchi ya Yuda na ya Benyamini.
11Haya maboma akayajenga kuwa yenye nguvu, akaweka humo wenye amri na vilimbiko vya vilaji na vya mafuta na vya mvinyo.
12Humo katika kila mji mmoja akaweka ngao na mikuki, akaijenga kuwa yenye nguvu nyingi mno. Nchi ya Yuda na ya Benyamini ikawa yake.
13Watambikaji na Walawi katika nchi zote za Isiraeli wakarudi upande wake na kutoka katika mipaka yao yote.
14Kwani Walawi wakayaacha malisho na mapato yao, wakaenda Uyuda na Yerusalemu, kwa kuwa Yeroboamu na wanawe waliwatupa, waiswe watambikaji wa Bwana.[#2 Mambo 13:9.]
15Akajiwekea mwenyewe watambikaji wa kutambika vilimani, nao wa kutambikia mashetani na ndama, alizozitengeneza.[#1 Fal. 12:31.]
16Katika mashina yote ya Isiraeli watu waliojipa mioyo ya kumtafuta Bwana Mungu wa Isiraeli wakawafuata wale, wakaja Yerusalemu kumtolea Bwana Mungu wa baba zao ng'ombe za tambiko.
17Hawa ndio walioutia ufalme wa Yuda nguvu, wakamwongezea Rehabeamu, mwana wa Salomo, uwezo miaka mitatu, kwani waliendelea katika njia za Dawidi na za Salomo miaka mitatu.
18Rehabeamu akamwoa Mahalati wa Yerimoti, mwana wa Dawidi na wa Abihaili, binti Eliabu, mwana wa Isai.[#1 Sam. 16:6.]
19Huyu akamzalia wana hawa: Yeusi na Semaria na Zahamu.
20Kisha akamwoa Maka, binti Abisalomu; huyu alimzalia Abia na Atai na Ziza na Selomiti.
21Rehabeamu akampenda maka, binti Abisalomu, kuliko wakeze na masuria zake wote, kwani alichukua wake 18 na masuria 60, akazaa wana wa kiume 28 na wa kike 60.
22Rehabeamu akamweka Abia, mwana wa Maka, kuwa mkuu na mwenye amri kwa ndugu zake, kwani alitaka kumpa ufalme.
23Kwa kuwa mwenye utambuzi akawatawanya wanawe wote katika nchi zote za Yuda na za Benyamini akiwaweka katika miji yote yenye maboma, akawapa vyakula vingi, akawaposea hata wanawake wengi.[#2 Mambo 21:3.]