The chat will start when you send the first message.
1Ikawa, Rehabeamu alipokwisha kuushikiza ufalme wake na kuutia nguvu, akayaacha Maonyo ya Bwana, yeye na Waisiraeli wote pamoja naye.
2Katika mwaka wa tano wa mfalme Rehabeamu akapanda Sisaki, mfalme wa Misri, kuujia Yerusalemu, kwani waliyavunja maagano ya Bwana.
3Akaleta magari 1200 na wapanda farasi 60000 nao watu waliokuja naye toka Misri hawakuhesabika, Walibia na Wasuki na Wanubi.
4Akaiteka miji yenye maboma iliyokuwako Uyuda, akafika hata Yerusalemu.[#2 Mambo 11:5-10.]
5Ndipo, mfumbuaji Semaya alipokuja kwake mfalme Rehabeamu na kwa wakuu wa Wayuda waliokusanyika kwake Yerusalemu kwa ajili ya Sisaki, akawaambia: Hivi ndivyo, anavyosema Bwana: Ninyi mmeniacha, basi, mimi nami nimewaacha na kuwatia mkononi mwa Sisaki.
6Ndipo, wakuu wa Isiraeli na mfalme walipojinyenyekeza, wakasema: Mwongofu ni Bwana!
7Bwana alipoona, ya kuwa wamejinyenyekeza, neno la Bwana likamjia Semaya kwamba: Kwa kuwa wamejinyenyekeza, sitawaangamiza, ila punde kidogo nitawapatia uponya, makali yangu yasimwagiwe Yerusalemu na huyo Sisaki.
8Lakini watakuwa watumishi wake, wapate kujua, utumishi wangu ulivyo, nao utumishi wa wafalme wa nchi nyingine ulivyo.
9Sisaki, mfalme wa Misri, akapanda, akaujia Yerusalemu, akavichukua vilimbiko vya Nyumbani mwa Bwana navyo vilimbiko vya nyumbani mwa mfalme, vyote pia akavichukua, nazo ngao za dhahabu, Salomo alizozitengeneza, akazichukua.
10Mahali pao mfalme Rehabeamu akatengeneza ngao za shaba, akazitia mikononi mwa wakuu wa wapiga mbio waliongoja pa kuingia nyumbani mwa mfalme, waziangalie.
11Kila mara mfalme alipoingia Nyumbani mwa Bwana, hao walinzi wakaja, wakazichukua, kisha wakazirudisha chumbani mwao wapiga mbio.
12Kwa kuwa amejinyenyekeza, makali ya Bwana yakageuka na kumwacha, asimwangamize na kummaliza kabisa, maana katika nchi ya Yuda yalikuwamo bado mambo mema.
13Kisha mfalme Rehabeamu akapata nguvu tena mle Yerusalemu na kuushika ufalme. Alipoupata ufalme alikuwa mwenye miaka 41, akawa mfalme miaka 17 katika mji wa Yerusalemu, Bwana aliouchagua katika mashina yote ya Isiraeli, alikalishe Jina lake humo. Jina la mama yake ni Nama aliyekuwa Mwaamoni.[#2 Mambo 6:20.]
14Akayafanya yaliyokuwa mabaya, kwani hakuuelekeza moyo wake, umtafute Bwana.
15Mambo ya Rehabeamu, ya kwanza na ya mwisho, hayakuandikwa kwenye mambo ya mfumbuaji Semaya na ya mchunguzaji Ido, kama mambo ya wakale yalivyoandikwa? Lakini Rehabeamu na Yeroboamu walikuwa wakipigana vita siku zile zote.[#2 Mambo 13:22.]
16Kisha Rehabeamu akaja kulala na baba zake, akazikwa mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Abia akawa mfalme mahali pake.