2 Mambo 13

Abia anamshinda Yeroboamu.

(Taz. 1 Fal. 15:1-8.)

1Katika mwaka wa 18 wa mfalme Yeroboamu Abia akapata kuwa mfalme wa Wayuda.

2Akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 3; jina la mama yake ni Mikaya, binti urieli wa Gibeoni. Naye akapiga vita na Yeroboamu.

3Abia akajifunga kwenda vitani mwenye vikosi vya mafundi wa vita, watu 400000 waliochaguliwa. Naye Yeroboamu akajipanga vitani mwenye watu 800000 waliochaguliwa kwa kuwa mafundi wa vita wenye nguvu.

4Abia akaondoka kuja kusimama juu ya mlima wa Semaraimu ulioko milimani kwa Efuraimu, akasema: Nisikilizeni, Yeroboamu nanyi Waisiraeli wote!

5Je? Hamjui, ya kuwa Bwana Mungu wa Isiraeli alimpa Dawidi kuwa mfalme wa Waisiraeli kale na kale, yeye na wanawe, alipofanya naye agano la chumvi?[#3 Mose 2:13; 4 Mose 18:19.]

6Lakini Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyekuwa mtumishi wa Salomo, mwana wa Dawidi, akaondoka kwa kumkataa bwana wake na kuacha kumtii.

7Wakakusanyika kwake watu walio wa ovyoovyo tu wasiofaa kitu, wakajipatia nguvu za kumshinda Rehabeamu, mwana wa Salomo; kwani Rehabeamu alikuwa akingali kijana, nao moyo wake mchanga, hakuweza kujishupaza mbele yao.

8Sasa ninyi mnajiwazia, ya kuwa mtaweza kujishupaza mbele ya ufalme wa Bwana uliomo mikononi mwa wana wa Dawidi, kwa kuwa kwenu ni uvumi wa watu wengi, nazo ndama za dhahabu mnazo, Yeroboamu alizowatengenezea kuwa miungu yenu.[#1 Fal. 12:28.]

9Hamkuwafukuza watambikaji wa Bwana, wana wa Haroni, pamoja na Walawi, mkajifanyizia watambikaji, kama makabila ya nchi hizi? Kila ajaye na kuleta mtoto mume wa ng'ombe na madume saba ya kondoo, apate kulijaza gao lake, basi, hupata kuwa mtambikaji wao isiyo miungu.[#2 Mambo 11:15.]

10Lakini sisi Bwana Mungu wetu hakutuacha, nao wana wa Haroni wanamtumikia Bwana kuwa watambikaji, nao Walawi wanafanya kazi zao;

11kila kunapokucha na kila kunapokuchwa humvukizia Bwana wakimteketezea ng'ombe za tambiko na kumvikizia mavukizo yanukayo vizuri, tena humwekea mikate katika meza iliyo ya dhahabu tupu, tena hukiwasha kinara cha dhahabu na taa zake kila kunapokuchwa, kwani sisi tunaushika ulinzi wa Bwana Mungu wetu, lakini ninyi mmemwacha.[#4 Mose 28:3-8.]

12Na mwone, ya kuwa Mungu yuko kwetu, ndiye anayetutangulia, nao watambikaji wake watapiga matarumbeta ya kuvumisha sana, wawazomee ninyi! Wana wa Isiraeli, msije kupigana na Mungu wa baba zenu! Kwani hamtafanikiwa.[#4 Mose 10:9.]

13Lakini Yeroboamu alikuwa ametuma wengine, wawazunguke, wapate kuwavizia huko nyuma kuwajia migongoni kwao; kwa hiyo wengine wao walikuwa mbele ya Wayuda, nao waliowavizia walikuwa nyuma yao.

14Wayuda walipogeuka wakaona, ya kuwa hawana budi kupigana mbele na nyuma; ndipo, walipomlilia Bwana, watambikaji wakayapiga matarumbeta yao.

15Kisha watu wa Yuda wakapiga yowe; ikawa, watu wa Yuda walipopiga yowe, Mungu akampiga Yeroboamu na Waisiraeli wote mbele ya Abia na ya Wayuda.

16Ndipo, wana wa Isiraeli walipowakimbia Wayuda, naye Mungu akawatia mikononi mwao.

17Abia na watu wake wakawapiga, pigo likawa kubwa mno; kwao Waisiraeli wakaanguka kwa kuuawa watu 500000, nao ni watu wliochaguliwa.

18Ndivyo, wana wa Isiraeli walivyonyenyekezwa siku zile, lakini wana wa Yuda wakapata nguvu, kwa kuwa walimwegemea Bwana Mungu wa baba zao.

19Abia akakimbia, amfuate Yeroboamu na kumfukuza, akateka kwake miji, ndio Beteli na mitaa yake na Yesana na mitaa yake na Efuraimu na mitaa yake.

20Yeroboamu hakupata nguvu tena katika hizo siku za Abia, kisha Bwana akampiga, akafa.

21Abia akajipatia nguvu, akajichukulia wanawake 18, akazaa wana wa kiume 22 na wa kike 16.

22Mambo mengine ya Abia na njia zake na maneno yake yameandikwa katika kitabu cha maelezo ya mfumbuaji Ido.[#2 Mambo 12:15.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania