The chat will start when you send the first message.
1Abia akaja kulala na baba zake, wakamzika mjini mwa Dawidi, naye mwanawe Asa akawa mfalme mahali pake. Siku zake nchi ikapata kutulia miaka kumi.
2Asa akayafanya mema yanyokayo machoni pake Bwana Mungu wake.
3Akapaondoa pa kutambikia miungu migeni na matambiko ya vilimani, akazivunja nazo nguzo za mawe za kutambikia, nayo miti ya Ashera akaikatakata.
4Akawaambia Wayuda, wamtafute Bwana Mungu wa baba zao, wayafanye Maonyo na maagizo yake.
5Katika miji yote ya Wayuda akayaondoa matambiko ya vilimani na mifano ya jua; kwa hivyo, alivyoushika ufalme, nchi ikatulia.
6Akajenga miji yenye maboma katika nchi ya Yuda, kwani nchi ilikuwa imetulia, hakuwa na vita vyo vyote katika miaka hiyo, kwani Bwana alimpatia utulivu.[#2 Mambo 15:15.]
7Kwa hiyo aliwaambia Wayuda: Na tuijenge miji hii na kuizungushia maboma na minara na kutia humo malango yenye makomeo; nchi hii ingaliko wazi mbele yetu, kwani tumemtafuta Bwana Mungu wetu; naye kwa hivyo, tulivyomtafuta, ametupatia kutulia pande zote. Basi, wakaijenga, wakafanikiwa.
8Asa akawa na vikosi vya watu walioshika ngao na mikuki, Wayuda 300000 na Wabenyamini walioshika ngao ndogo, waliojua hata kupinda pindi 280000; hawa wote walikuwa mafundi wa vita wenye nguvu.
9Ndipo, alipotokea kwao Mnubi Zera mwenye vikosi vya watu milioni na magari 340, akaja mpaka Maresa.
10Asa akamtokea, wakajipanga kupigana katika bonde la Sefata karibu ya Maresa.
11Asa akamlalamikia Bwana Mungu wake akisema: Bwana, hakuna mwingine, usipokuwa wewe, anayeweza kumsaidia mwenye watu wengi naye asiye na nguvu; tusaidie, Bwana Mungu wetu! Kwani tumekuegemea wewe, tukaja kwa Jina lako kupigana na uvumi huu wa watu; Bwana, Mungu wetu ndiwe wewe! Hapa pasiwe na mtu atakayekushinda nguvu![#1 Sam. 14:6.]
12Ndipo, Bwana alipowapiga Wanubi mbele ya Asa na mbele ya Wayuda, Wanubi wakakimbia.
13Asa akawakimbiza pamoja na hao watu, aliokuwa nao, mpaka Gerari; kwa Wanubi watu wakauawa kabisa, hakusalia kwao waliopona, kwani walivunjwa mbele ya Bwana na mbele ya vikosi vyake. Kisha Wayuda wakachukua mateka mengi sana.
14Wakaipiga miji yote pia iliyokuwa pande zote za Gerari, kwani tisho la Bwana lilikuwa limewaguia, wakazipokonya mali zote zilizokuwa katika miji hiyo yote, nazo mali za kupokonya zikawamo nyingi sana.
15Nayo mahema ya makundi wakayavunja, wakateka mbuzi na kondoo wengi, hata ngamia, kisha wakarudi Yerusalemu.