2 Mambo 21

Yoramu anatawala vibaya.

(Taz. 2 Fal. 8:16-22.)

1Yosafati akaja kulala na baba zake, akazikwa kwa baba zake mjini mwa Dawidi. Naye mwanawe Yoramu akawa mfalme mahali pake.

2Yoramu alikuwa na ndugu, nao walikuwa wana wa Yosafati, ndio Azaria na Yehieli na Zakaria na Azaria na Mikaeli na Sefatia; hawa wote walikuwa wana wa Yosafati, mfalme wa Waisiraeli.

3Hawa baba yao aliwapa vipaji vingi vya fedha na vya dhahabu na vya vitu vyenye kima, pamoja na miji yenye maboma katika nchi ya Yuda, lakini ufalme alimpa Yoramu, kwani huyu alikuwa mwanawe kwa kwanza.

4Yoramu alipokwisha kujisimikia ufalme wa baba yake na kujipatia nguvu, akawaua ndugu zake wote kwa upanga, hata wakuu wengine wa Waisiraeli

5Yoramu alikuwa mwenye miaka 32 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 8.

6Akaendelea katika njia za wafalme wa Waisiraeli, kama wale wa mlango wa Ahabu walivyofanya, kwani binti Ahabu alikuwa mkewe; basi, naye akayafanya yaliyo mabaya machoni pake Bwana.

7Lakini Bwana hakutaka kuuangamiza mlango wa Dawidi kwa ajili ya agano, alilolifanya na Dawidi, kwa kuwa alisema, ya kama atampa yeye na wanawe kuwa taa iwakayo siku zote.[#2 Sam. 7:12; 1 Fal. 11:36; Sh. 132:17.]

Waedomu na Walibuna wanavunja maagano.

8Katika hizo siku zake Waedomu wakalivunja agano wakijitoa mikononi mwa Wayuda, wakajiwekea mfalme wa kuwatawala.

9Ndipo, Yoramu alipoondoka kuwaendea pamoja na wakuu wake, akiyachukua magari yote. Ikawa, alipoondoka usiku, akawapiga Waedomu waliomzunguka yeye na wakuu wa magari.

10Lakini Waedomu wakalivunja agano tena, wakajitoa mikononi mwa Wayuda mpaka siku hii ya leo. Siku zile ndipo, nao wa Libuna walipolivunja agano na kujitoa mkononi mwake, kwani alimwacha Bwana Mungu wa baba zake.

11Yeye naye akafanya matambiko ya vilimani katika milima ya Yuda; ndivyo, alivyowazinisha wenyeji wa Yerusalemu, nao Wayuda akawaponza.

Barua ya mfumbuaji Elia.

12Ikafika kwake barua ya mfumbuaji Elia ya kwamba: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa baba yako Dawidi anavyosema: kwa kuwa hukuendelea katika njia za baba yako Yosafati, wala katika njia za Asa, mfalme wa Wayuda,

13ukaendelea katika njia za wafalme wa Waisiraeli, ukawazinisha Wayuda na wenyeji wa Yerusalemu, kama mlango wa Ahabu ulivyozini, ukawaua nao ndugu zako wa mlango wa baba yako waliokuwa wema kuliko wewe,

14na umwone Bwana, akiwapiga pigo kubwa watu wako, hata wanao na wake zako na mali zako zote.

15Lakini wewe utapatwa na magonjwa mengi kwa kuugua tumboni mwako, mpaka matumbo yako yatokee kwa kuugua hivyo siku nyingi na nyingi.

Kufa kwake Yoramu.

16Kisha Bwana akaziamsha roho za Wafilisti na za Waarabu waliopakana na Wanubi, wamjie Yoramu.

17Wakapanda katika nchi ya Yuda na kujipenyeza huko, wakaziteka mali zote zilizoonekana nyumbani mwa mfalme, hata watoto wake na wakeze, hakusalia mtoto kwake ila Yoahazi tu aliyekuwa mdogo katika wanawe wote.

18Baada ya hayo Bwana akampiga tumboni mwake, apate ugonjwa usio na mganga wa kuuponya.

19Ukawa wa siku nyingi na nyingi; matumbo yake yakatokea kwa huo ugonjwa, siku zilipokwisha kupita kama miaka miwili, akafa na kuumia vibaya. Kisha watu wake hawakumteketezea manukato, kama walivyowateketezea baba zake.[#2 Mambo 16:14.]

20Alikuwa mwenye miaka 32 alipoupata ufalme, akawa mfalme mle Yerusalemu miaka 8, akajiendea pasipo kuombolezewa, wakamzika mjini mwa Dawidi, lakini hawakumzika makaburini kwa wafalme.[#2 Mambo 21:5; 24:25.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania