2 Mambo 9

Mfalme wa kike wa Saba anamwamkia Salomo.

(1-28: 1 Fal. 10:1-28.)

1Mfalme wa kike wa Saba alipousikia uvumi wa Salomo, akaenda Yerusalemu kumjaribu Salomo kwa maulizo ya kufumbafumba, akaja na vikosi vikubwa mno na ngamia waliochukua uvumba na dhahabu nyingi na vito. Alipofika kwa Salomo akasema naye na kumwuliza yote, aliyokuwa nayo moyoni mwake.

2Salomo akamwelezea yote, aliyomwuliza, halikuwako neno lililofichika maana kwake Salomo, asiloweza kumwelezea.

3Ndipo, mfalme wa kike wa Saba alipouona werevu wa Salomo kuwa wa kweli, kisha akaitazama nyumba, aliyoijenga,

4na vilaji vilivyopo mezani na vikao vya watumwa wake na kazi za watumishi wake na mavazi yao, hata watunza vinywaji wake na mavazi yao na dari, aliyoiweka juu ya Nyumba ya Bwana; ndipo, roho yake ilipozimia,

5akamwambia mfalme: Kumbe ni ya kweli, niliyoyasikia katika nchi yangu ya mambo yako na ya werevu wako ulio wa kweli!

6Lakini sikuyaitikia hayo maneno yao kuwa ya kweli, mpaka nikija, nikayaona kwa macho yangu. Tena naona, ya kuwa sikuambiwa nusu tu ya werevu wako mwingi mno ulio wa kweli, maana ni mkuu kuliko ule uvumi, niliousikia.

7Wenye shangwe ni watu wako, nao hawa watumwa wako ni wenye shangwe kwa kusimama mbele yako siku zote na kuyasikia maneno ya werevu wako ulio wa kweli.[#Luk. 10:23.]

8Bwana Mungu wako na atukuzwe, kwa kuwa alipendezwa na wewe, akakukalisha katika kiti chake cha kifalme, uwe mfalme wa Bwana Mungu wako! Kwa kuwa Mungu wako anawapenda Waisiraeli, awapatie kuwapo kale na kale, alikupa kuwa mfalme wao, uwaamue kwa wongofu.

9Kisha akampa mfalme vipande vya dhahabu 120, ndio frasila 360, na uvumba mwingi sana na vito; uvumba mwingi kama huo, mfalme wa kike wa Saba aliompa Salomo, ulikuwa haujapatikana bado.

10Kweli nao watumishi wa Huramu na watumishi wa Salomo waliotoa dhahabu kule Ofiri wakaleta nayo miti ya uvumba na vito,

11naye mfalme akaitumia hiyo miti ya uvumba ya kutengeneza vipago vya Nyumba ya Bwana na vya nyumba ya mfalme na mazeze na mapango ya waimbaji. Lakini mali kama hizo hazijaonekana siku za mbele katika nchi ya Yuda.

12Kisha mfalme Salomo akampa mfalme wa kike wa Saba yote, aliyopendezwa nayo, aliyomwomba, kuliko yale, aliyomletea mfalme; kisha akarudi kwenda kwao katika nchi yake, yeye na watumishi wake.

Mali za Salomo.

13Uzito wa dhahabu, Salomo alizoletewa katika mwaka mmoja ulikuwa vipande vya dhahabu 666, ndio frasila 2000,

14pasipo zile, watembeaji na wachuuzi walizomletea; nao wafalme wote wa nchi ya Waarabu na watawala nchi wakamletea Salomo dhahabu na fedha.

15Mfalme Salomo akatengeneza ngao 200 za dhahabu zilizofuliwa, kila ngao moja ikatumiwa sekeli 600, ndio nusu kubwa ya frasila ya dhahabu zilizofuliwa.

16Kisha akatengeneza ngao ndogo 300 za dhahabu zilizofuliwa, hizi ngao ndogo kila moja ikatumiwa sekeli 300, ndio ratli tisa za dhahabu; mfalme akaziweka katika nyumba ya mwituni kwa Libanoni.

17Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme cha pembe za tembo, akakifunikiza dhahabu tupu.

18Hicho kiti cha kifalme kilikuwa na vipago sita vya kukipandia, tena hapo chini yake palikuwa pamefanyizwa pa kuwekea miguu, napo palikuwa pa dhahabu. Tena hapo pa kukalia palikuwa na maegemeo huku na huko, nayo mifano miwili ya simba ilikuwa imesimama hapo penye maegemeo.

19Tena mifano kumi na miwili ya simba ilikuwa imesimama juu ya vile vipago sita huku na huko. Kitu kilichotengenezwa vizuri hivyo hakikuwako katika ufalme wote.

20Navyo vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Salomo vilikuwa vya dhahabu, navyo vyombo vyote vya ile nyumba ya mwituni kwa Libanoni vilikuwa vya dhahabu zilizong'azwa; kwani fedha ziliwaziwa kuwa si kitu katika siku za Salomo.

21Kwani merikebu za mfalme zilikwenda Tarsisi zikipelekwa na watumishi wa Huramu; kila miaka mitatu hizo merikebu zilizokwenda Tarsisi zikaja mara moja, zikaleta dhahabu na fedha na pembe za tembo na tumbili na madege wenye manyoya mazuri mno wanaoitwa tausi.

22Hivyo ndivyo, mfalme Salomo alivyokuwa mkuu kuwapita wafalme wote wa huku nchini kwa utukufu na kwa werevu wa kweli.

23Wafalme wote wa huku nchini wakataka kuuona uso wake Salomo, wayasikie maneno ya werevu wake wa kweli, Mungu alioutia moyoni mwake.

24Nao wakaleta kila mtu matunzo yake: vyombo vya fedha na vyombo vya dhahabu na mavazi na mata na uvumba na farasi na nyumbu; vikawa hivyo mwaka kwa mwaka.

25Salomo akawa na majozi ya farasi 4000 na magari, tena wapanda farasi 12000, akawakalisha katika miji ya magari namo mwake mfalme mle Yerusalemu.[#2 Mambo 1:14-17; 1 Fal. 4:26.]

26Akawa akiwatawala wafalme wote toka lile jito mpaka nchi ya Wafilisti kuifikilia nayo nchi ya Misri.

27Mfalme akajipatia fedha kuwa nyingi mle Yerusalemu kama mawe, nayo miti ya miangati akajipatia kuwa mingi kama mitamba katika nchi ya tambarare.

28Wakamletea Salomo farasi, waliowatoa Misri na katika nchi zote.

Kufa kwake Salomo.

(29-31: 1 Fal. 11:41-43.)

29Mambo mengine ya Salomo ya kwanza na ya mwisho hayakuandikwa kwenye mambo ya mfumbuaji Natani na kwenye ufumbuaji wa Ahia wa Silo na kwenye maono ya mchunguzaji Yedi, aliyomchunguzia Yeroboamu, mwana wa Nebati?[#1 Fal. 11:29.]

30Salomo akawa mfalme mle Yerusalemu na kuwatawala Waisiraeli wote miaka 40.

31Kisha Salomo akaja kulala na baba zake, wakamzika mjini mwa baba yake Dawidi, naye mwanawe Rehabeamu akawa mfalme mahali pake.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania