2 Wakorinto 12

Kujivunia unyonge.

1Nashurutishwa kujivuna, hata isifae kitu. Lakini sasa nitafikia, nilivyotokewa na Bwana, nayo niliyofunuliwa.

2Yuko mtu nimjuaye kuwa mwenye Kristo; sasa miaka yapata 14, kama alikuwa mwilini, sijui, au kama alikuwa ametengwa na mwili wake, sijui; Mungu anayajua. Mtu huyo alipokonywa na kupelekwa, mpaka aiingie mbingu ya tatu.

3Nami nimemjua mtu huyo; kama alikuwa mwilini, au kama alikuwa pasipo mwili wake, sijui; Mungu anayajua.

4Naye alipokonywa kupelekwa Paradiso, akasikia maneno yasiyosemeka, yasiyowezekana kusemwa na mtu.

5Kwa ajili yake yeye nitajivuna, lakini kwa ajili yangu mimi hakuna, nitakalojivunia, isipokuwa unyonge wangu.[#2 Kor. 11:30.]

6Kama ningetaka kujivuna, singekuwa mpuzi, kwani ningesema yaliyo ya kweli. Lakini najikinga, mtu asiniwazie kuwa mkuu kuliko hapo, anionapo na kunisikia.[#2 Kor. 10:8; 11:16.]

7Tena yako mafunuo makuu yote, niliyoyapata; lakini kwa kwamba nisijikweze kwa ajili yao, nimetiwa chomeo mwilini mwangu, ndio mjumbe wake Satani; akafunguliwa, anipige makonde nisijikweze.[#Iy. 2:6.]

8Kwa ajili yake yeye nimemlalamikia Bwana mara tatu, aniondokee;

9naye akaniamba: Gawio langu likutoshee! Kwani katika unyonge ndimo, nguvu yangu itimilikamo. Kwa sababu hii kinipendezacho kupita vingine ni kujivunia manyonge yangu, nguvu ya Kristo ipate kunikalia.

10Kwa hiyo ninaviona kuwa vema, nikiwa mnyonge au nikikorofishwa au nikihangaishwa au nikifukuzwa au nikisongwa kwa kuwa wake Kristo. Kwani ninapokuwa mnyonge, ndipo, nilipo mwenye nguvu.*[#Fil. 4:13.]

Paulo anawafuata wao wenyewe, si mali zao.

11Nimekuwa mpuzi wa kujivuna, lakini ninyi mmenishurutisha. Kwani ingefaa, mimi nisifiwe nanyi. Kwani hakuna, nishindwacho nao wale wajipao macheo yote ya utume, hata nikiwa si kitu mimi.[#2 Kor. 11:5.]

12Yamjulishayo mtu kuwa mtume yamefanyika kati yenu, kama ni uvumilivu mwingi, au kama ni vielekezo na vioja na vya nguvu.[#Tume. 19:11-12; Rom. 15:19.]

13Kuna nini, mliyopungukiwa kuliko wateule wengine, isipokuwa hii tu, ya kuwa sikuzila mali zenu ninyi? Niachilieni upotovu huu![#2 Kor. 11:9.]

14Tazameni, mara hii ni ya tatu, nikiwa tayari kuja kwenu, tena sitazila mali zenu. Kwani siyatafuti yaliyo yenu, ila nawatafuta ninyi wenyewe. Kwani haifai, watoto wawawekee wazazi wao vilimbiko, ila wazazi sharti wao wawawekee watoto.[#2 Kor. 13:1.]

15Lakini mimi yanipendezayo sana ni kutoa yaliyo yangu, kweli hata mwenyewe nitatolewa kwa ajili yenu ninyi; nikijipingia kuwapenda, itafaa nikipungukiwa kupendwa?[#Fil. 2:17.]

16Basi, kwa sababu mimi sikuwasumbua, wale husema: Kwa kuwa mwenye werevu mbaya nimewakamata kwa hila.

17Je? Nimeyatwaa yaliyo yenu ninyi kwa mikono yao wale, niliowatuma kwenu?

18Nimemwonya Tito, nikatuma pamoja naye yule ndugu. Je? Yako yenu, Tito aliyoyatwaa? Roho ituendeshayo siyo ileile moja? Nazo nyayo, tuzifuatazo, sizo zizo hizo?[#2 Kor. 8:6,16-18.]

Makosa ya Wakorinto.

19Mmeanza kale kutuwazia, ya kuwa twajikania mbele yenu. Lakini Mungu ajua: twasema kwa kuwa wake Kristo. Nayo yote tunayasema, tuwajenge ninyi, wapenzi.

20Maana naogopa, ya kuwa nitakapokuja sitawaona ninyi, kama nitakavyo kuwaona, tena ya kuwa nami hamtaniona nanyi, kama mtakavyo kuniona. Naogopa kukuta magombano na wivu na mifundo ya mioyo na machokozi na masingizio na mateto na majivuno na matukutiko.[#2 Kor. 10:2; 1 Kor. 4:6.]

21Kwa hiyo naogopa kwamba: Nitakapofika kwenu, Mungu wangu ataninyenyekeza tena, nami nitapata kusikitika kwa ajili yao wengi waliokosa kale pasipo kuyajutia mambo ya uchafu na ya ugoni na ya uasherati, waliyoyafanyiza.[#2 Kor. 2:1; 13:2.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania