2 Wakorinto 5

Jengo letu la mbinguni.

1Kwani twajua, ya kuwa hivi vijumba vyetu, tupangamo nchini, vitakapobomolewa, tunayo majengo yaliyojengwa na Mungu, ni nyumba zisizojengwa na mikono ya watu, nazo hukaa kale na kale huko mbinguni.[#Iy. 4:19; 2 Petr. 1:13-14.]

2Kwani hii ndiyo itupigishayo kite, tukitunukia, tuvikwe makao yetu yatokayo mbinguni;[#Rom. 8:23.]

3maana tukiwa tumeyavika hatutaonekana kuwa wenye uchi.

4Kwani sisi tuliomo humu kibandani hupiga kite kwa kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa, ila hutaka kuvikwa, maana iliyo yenye kufa imezwe nayo yenye uzima.[#1 Kor. 15:51-53.]

5Lakini aliyetutengenezea yaya haya ndiye Mungu aliyetupa Roho, awe rehani yetu.[#2 Kor. 1:22; Rom. 8:16,23; Ef. 1:13-14.]

6Kwa hiyo yako, tunayoyatazamia siku zote tukijua, ya kuwa tukiwa mwetu miilini twamkalia Bwana mbali.[#Ebr. 11:13.]

7Kwani sisi hufanya mwendo kwa kumtegemea Mungu, siko kwa kuona.[#1 Kor. 13:12.]

8Lakini kwa hayo, tunayoyatazamia, hupenda sana kuhama miilini, tupate kukaa kwetu kwa Bwana.[#Fil. 1:23.]

9Kwa sababu hii twajihimiza, tumpendeze yeye, ikiwa tuwe bado mwetu miilini, au tuwe tumekwisha kuitoka.*[#Sh. 39:13.]

10Kwani sisi sote sharti tutokee mbele ya kiti cha uamuzi cha Kristo, kila mmoja alipwe, aliyoyafanyiza alipokuwa mwilini, yakiwa mema au maovu.[#Yoh. 5:29; Tume. 17:31; Rom. 2:16; 14:10.]

Mapatano ya Kimungu.

11Kwa sababu twajua, ya kuwa Bwana huogofya, twawaonya watu, lakini Mungu ndiye, tumtokeaye hivyo, tulivyo. Lakini ninacho kingojeo cha kwamba: Mioyo yenu inajua, ya kuwa nayo tumeitokea hivyo, tulivyo.

12Hatujisifu tena mbele yenu, ila twataka kuwapa ninyi sababu ya kujivuna kwa ajili yetu, mpate kuwajibu wale wanaojivunia yaliyo machoni tu, yasiyo namo mioyoni.[#2 Kor. 3:1.]

13Kwani tulipokuwa kama wenye wazimu, ni kwa ajili ya Mungu; tena tunapoerevuka, ni kwa ajili yenu.[#2 Kor. 12:2; 1 Kor. 14:19.]

14*Kwani upendo wa Kristo hutuhimiza sisi, tukawaza hivyo: Mmoja alipokufa kwa ajili yao wote, kwa hiyo wote wamekwisha kufa.

15Naye alipokufa kwa ajili yao wote alitaka, walio hai wasijikalie wenyewe, ila wamkalie yeye aliyekufa kwa ajili yao, kisha akafufuliwa.[#Rom. 14:7-8; 1 Tim. 2:6.]

16Kwa hiyo tangu sasa hakuna, tunayemjua kimwili. Ikiwa tulimtambua Kristo kimwili, sasa hatumtambui tena hivyo.[#Mat. 12:46-50.]

17Kwa hiyo mtu akiwa anaye Kristo, amekuwa kiumbe kipya. Yake ya kale yamepita; ukimtazama, yote yamekuwa mapya.[#Rom. 8:1,10; Gal. 2:20; 6:15; Ufu. 21:5.]

18Nayo yote hutoka kwa Mungu; ndiye aliyetupatanisha sisi naye yeye, Kristo alipojitoa. Kisha akatupa kuyatumikia hayo mapatano[#Rom. 5:10.]

19kwamba: Mungu alikuwa katika Kristo, akawapatanisha wa ulimwengu naye yeye, asiwahesabie maanguko yao; akaweka kwetu wenye kuyatangaza hayo mapatano.[#Rom. 3:24-25; Kol. 1:19-20.]

20Hivyo sisi tu wajumbe mahali pake Kristo; ndivyo Mungu mwenyewe anavyowaonya kwa vinywa vyetu sisi. Maana twawabembeleza mahali pa Kristo: Yapokeeni hayo mapatano yake Mungu![#Yes. 52:7; Luk. 10:16.]

21Asiyetambua kosa alimgeuza kuwa mwenye makosa kwa ajili yetu, sisi tugeuzwe naye kuwa wenye wongofu wa Kimungu.*[#Yes. 53:4-5,8; Yoh. 8:46; 1 Kor. 1:30; Gal. 3:13; Fil. 3:9; Ebr. 4:15.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania