2 Samweli 11

Ugoni na uuaji wake Dawidi.

1Ikawa, mwaka ulipopita, siku hizo wafalme wanapozoea kwenda vitani, ndipo, Dawidi alipomtuma Yoabu na watumishi wake pamoja naye na Waisiraeli wote, wakawaangamiza wana wa Amoni, wakausonga mji wa Raba kwa kuuzinga, lakini Dawidi alikuwa anakaa Yerusalemu.[#1 Mambo 20:1.]

2Siku moja saa za jioni Dawidi akaondoka kitandani pake, akatembea darini juu ya nyumba ya mfalme. Toka huko juu darini akaona mwanamke aliyeoga, naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana wa kumtazama.[#Mat. 5:28-29.]

3Dawidi akatuma mtu kuuliza, huyo mwanamke kama ni wa nani, akaambiwa: Huyo siye Bati-Seba, binti Eliamu, mkewe Mhiti Uria?[#2 Sam. 23:39.]

4Kisha Dawidi akatuma wajumbe, akamchukua; alipofika kwake, akalala naye. Naye huyu alipokwisha kujieua kwa ajili ya huo uchafu wake akarudi nyumbani mwake.[#3 Mose 15:18.]

5Huyu mwanamke alipopata mimba akatuma kumpasha Dawidi habari kwamba: Mimi ni mwenye mimba.

6Ndipo, Dawidi alipotuma kwa Yoabu kwamba: Mtume Mhiti Uria, aje kwangu! Naye Yoabu akamtuma Uria kwake Dawidi.

7Uria alipofika kwake Dawidi akamwuliza, kama Yoabu hajambo, kama watu hawajambo, tena jinsi vita vinavyoendelea.

8Kisha Dawidi akamwambia Uria: Shuka kwenda nyumbani mwako kuiosha miguu yako! Uria alipotoka nyumbani mwa mfalme, chakula cha kifalme kikatoka nacho kumfuata.

9Lakini Uria akalala mlangoni penye nyumba ya mfalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, hakushuka kwenda nyumbani mwake.

10Watu walipompasha Dawidi habari hizo kwamba: Uria hakushuka kwenda nyumbani mwake, Dawidi akamwuliza Uria: Je? Hukutoka njiani? Mbona hushuki kwenda nyumbani mwako?

11Ndipo, Uria alipomwambia Dawidi: Lile Sanduku na Waisiraeli na Wayuda wanakaa vibandani; naye bwana wangu Yoabu na watumishi wa bwana wangu wanalala porini; basi, mimi nitawezaje kuingia nyumbani mwangu, nile, ninywe, kisha nilale na mke wangu? Hivyo, ulivyo mzima, tena hivyo, roho yako ilivyo nzima, sitafanya kabisa jambo kama hilo.[#1 Sam. 4:4.]

12Dawidi akamwambia Uria: Kaa huku hata leo! Kesho nitakupa ruhusa, uende zako. Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku hiyo. Kesho yake,

13Dawidi alipomwita, akala, akanywa kwake; ndipo, alipomlewesha. Jioni akatoka kulala penye kilalo chake pamoja na watumishi wa bwana wake, asishuke kwenda nyumbani mwake.

14Kulipokucha, Dawidi akamwandikia Yoabu barua, akaipeleka mkononi mwa Uria.

15Namo katika barua ameandika kwamba: Mwekeni Uria mahali pa mbele, mapigano yanapozidi kuwa makali! Kisha rudini nyuma na kumwacha, apigwe, afe!

16Yoabu alipoyaangalia mambo ya huo mji, akamweka Uria mahali, alipopajua, ya kuwa hapo watatokea watu wenye nguvu.

17Watu wa huo mji walipotoka kupigana na Yoabu, wakauawa watu miongoni mwao walio watu wake na watumishi wa Dawidi, hata yule Mhiti Uria akafa naye.

18Kisha Yoabu akatuma kumpasha Dawidi habari za mambo yote ya vita.

19Akamwagiza yule mjumbe kwamba: Utakapokwisha kumwambia mfalme habari zote za vita,

20labda machafuko yatampata mfalme, akuulize: Mbona mmeukaribia huo mji kupigana nao? Hamkujua, ya kuwa watapiga mishale toka juu ukutani?

21Ni nani aliyempiga Abimeleki, mwana wa Yerubeseti? Siye mwanamke aliyemtupia jiwe la sago toka juu ukutani, afe huko Tebesi? Mbona mmeukaribia mji hivyo? Basi, ndipo, utakapomwambia: Hata mtumishi wako yule Mhiti Uria, amekufa naye.[#Amu. 9:53.]

22Kisha yule mjumbe akaenda, akaja kumpasha Dawidi habari hizo zote, Yoabu alizomtuma.

23Huyo mjumbe akamwambia Dawidi: Wale watu wakatutolea nguvu na kututokea kwetu porini, nasi tukawaendea hata hapo pa kuliingilia lango la mji.

24Ndipo, wapiga mishale walipowapiga watumishi wako toka juu ukutani, watu wakafa miongoni mwa watumishi wa mfalme, hata mtumishi wako, yule Mhiti Uria, akafa.

25Naye Dawidi akamwambia huyo mjumbe: Hivyo umwambie Yoabu: Jambo hili lisiwe baya machoni pako! Kwani upanga hula huku na huko; jipe moyo, upigane na huo mji, mpaka uubomoe! Hivyo ndivyo, umshikize moyo.

26Mkewe Uria aliposikia, ya kuwa mumewe Uria amekufa, akamwombolezea bwana wake.

27Siku za matanga zilipopita, Dawidi akatuma kumchukua nyumbani mwake, akawa mkewe, akamzalia mwana. Lakini jambo hili, Dawidi alilolifanya, likawa baya machoni pake Bwana.[#2 Mose 20:13-14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania