Amosi 8

Mfano wa nne wa mapatilizo ya Waisiraeli.

1Hili ndilo ono, Bwana Mungu alilonionyesha: Nimeona kikapu chenye matunda yaliyoiva. Akaniuliza:[#Amo. 7:8.]

2Unaona nini, Amosi? Niliposema: Kikapu chenye matunda yaliyoiva, Bwana akaniambia: Zimetimia siku za kuishia kwao walio ukoo wangu wa Isiraeli, sitaendelea tena kuwapita tu.

3Siku hiyo ndipo, nyimbo za majumbani zitakapokuwa vilio, kwani mizoga ya watu itakuwa mingi, mahali po pote wataitupa tu na kunyamaza kimya; ndivyo, asemavyo Bwana Mungu.[#Amo. 6:10.]

4Lisikieni hili, ninyi mfokeao maskini, mkakanyaga wanyonge wa nchi[#Amo. 2:7.]

5Mwasema: Mwezi mpya utatokea lini, tupate kuuza ngano?

Nayo siku ya mapumziko itapita lini, tupate kufungua malimbikio?

Ndipo, tutakapopunguza pishi pamoja na kuongeza bei,

tuwadanganye watu kwa mizani zilizo za uwongo.

6Ndipo, tutakaponunua wanyonge kwa fedha, wawe watumwa,

nao maskini kwa viatu viwili,

makumvi ya ngano nayo tutayauza.

7Bwana ameapa na kumtaja aliye mkuu wa Yakobo kwamba:

Sitayasahau kale na kale matendo yao yote!

8Je? Kwa ajili ya hayo nchi isitetemeke?

Asiomboleze kila mtu akaaye huku?

Nchi yote nzima itajitutumua kama mto wa Nili kwa kuchafuka,

kisha itakupwa kama lile jito la Misri.

9Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu:

Siku hiyo ndipo, nitakapoliendesha jua, lichwe mnamo saa sita,

niugeuze mwanga wa mchana kuwa giza katika nchi.

Nazo sikukuu zenu nitazigeuza kuwa za maombolezo,

10nazo nyimbo zenu zote kuwa vilio;

kisha nitawavika nyote magunia viunoni,

napo vichwani penu nyote nitatoa vipara.

Nitafanya, maombolezo yawe kama ya

kumwombolezea mwana wa pekee,

mwisho wao uwe kama siku yenye uchungu.

11*Ndivyo, asemavyo Bwana Mungu:

Mtaona, siku zikija, nitakapotuma njaa,

ije kuingia katika nchi hii,

siyo njaa ya chakula, wala siyo kiu ya maji,

ila itakuwa njaa ya kuyasikia maneno ya Bwana.

12Ndipo, watakapotangatanga, watoke baharini,

wafike kwenye bahari nyingine,

tena watoke upande wa kaskazini,

wafike upande wa maawioni kwa jua;

watazunguka po pote kwa kulitafuta Neno la Bwana,

lakini hawataliona.*

13Siku hiyo ndipo, watakapozimia kwa kiu

wanawali wazuri pamoja na wavulana.

14Ndio wao wanaoapa na kuvitaja vinyua vya Samaria

vinavyowakosesha, nao wasemao:

Hivyo, Mungu wako, Dani, alivyo mzima!

Au: Hivyo, njia ya Beri-Seba inavyotupa uzima!

wataanguka, lakini hawatainuka tena.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania