Amosi 9

Mapatilizo mabaya ya Waisiraeli.

1Nimemwona Bwana, akisimama penye kutambikia na kusema:

Zipige nguzo pembeni juu, vizingiti vya juu vitikisike!

Kisha uviponde, viwaangukie vichwani pao wote!

nao watakaosalia nitawaua kwa upanga,

pasiwe hata mmoja kwao, atakayekimbia,

wala mmoja wao atakayepona.

2Ingawa wapenyelee kuzimuni, huko nako mkono wangu utawatoa;

ingawa wapande mbinguni, huko nako nitawabwaga chini.

3Ingawa wajifiche mlimani kwa Karmeli juu,

huko nako nitawakamata na kuwachukua;

ingawa wajitoweshe machoni pangu baharini chini kabisa,

huko nako nitawaagizia nyoka, awaume.

4Ingawa waje mbele ya adui zao wakihamishwa kwenda

utumwani,

huko nako nitawaagizia upanga, uwaue;

ndipo, nitakapowaelekezea macho yangu,

niwapatie mabaya, nisiwapatie mema.

5Hapo, Bwana Mungu Mwenye vikosi atakapoigusa nchi,

itayeyuka papo hapo, wote wakaao huko waomboleze;

ndipo, nchi yote itakapojitutumua kama mto wa Nili,

kisha itakupwa kama lile jito la Misri.

6Ndiye aliyepajenga pake mbinguni kuwa dari yake,

nayo misingi ya kao lake aliiweka chini;

ndiye anayeyaita maji ya baharini, ayafurikishe juu ya

nchi kavu.

Bwana ni Jina lake!

7Ndivyo, yeye Bwana asemavyo:

Ham sawasawa kama wana wa Kinubi, ninyi wana wa Isiraeli?

Waisiraeli sikuwatoa katika nchi ya Misri?

Nao Wafilisti kule Kafutori? Nao Washami kule Kiri?

8Mtaona, macho yangu Bwana Mungu yakiutazama ufalme uliokosa

niutoweshe juu ya nchi,

lakini sitautowesha mlango wa Yakobo wote mzima;

ndivyo, asemavyo Bwana.

9Kwani mtaona, nikitoa amri, niwapepete walio mlango wa Isiraeli

na kuwatapanya kwa mataifa yote,

kama ngano zinavyopepetwa katika ungo,

pasipatikane hata chembe moja itakayoanguka chini.

10Wakosaji tu wa ukoo wangu watauawa wote kwa panga,

ndio waliosema: Mabaya hayatatufikia, wala hayatatupata.

Kiagio cha siku, huruma zitakapotokea.

11Siku hiyo ndipo, nitakapokisimamisha

kibanda cha Dawidi kilichoanguka,

na kuziziba nyufa zake

na kuyasimamisha mabomoko yake,

nikijenge, kiwe kama siku za kale,

12wayatwae masao ya Edomu na wamizimu wote

waliotangaziwa Jina langu;

ndivyo, asemavyo Bwana, naye atayafanya haya.

13Ndivyo, asemavyo Bwana: Mtaona, siku zikija,

mwenye kulima atakaposhikamana na mvunaji,

vile vile mwenye kuzikamua zabibu na mpanda mbegu.

Ndipo, milima itakapochuruzika pombe mbichi,

vilima vyote vifurikwe nazo.

14Ndipo, nitakapoyafungua mafungo yao walio ukoo wangu wa

Isiraeli,

waijenge miji yao iliyoangamizwa,

waipande mizabibu yao, wapate kunywa mvinyo zao.

15Ndipo, nitakapowapanda katika nchi yao,

wasing'olewe tena katika nchi yao, niliyowapa.

Bwana Mungu wako ameyasema.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania