The chat will start when you send the first message.
1Katika mwaka wa tatu wa Kiro, mfalme wa Wapersia, Danieli aliyeitwa jina lake Beltesasari akafunuliwa neno; hilo neno ni la kweli, masumbufu yatakuwa makubwa. Naye akalitambua hilo neno, akayatambua nayo, aliyoyaona.[#Dan. 1:7,21.]
2Siku zile mimi Danieli nilikuwa nikikaa matanga siku za majuma matatu.
3Sikula chakula kilichopendeza, wala nyama, wala mvinyo haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta, mpaka siku za majuma matatua ziishe.
4Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza mimi Danieli nilikuwa penye ukingo wa jito kubwa, nalo ndilo Hidekeli.
5Nilipoyainua macho yangu na kutazama, mara nikaona mwanamume mmoja aliyevaa nguo nyeupe ya ukonge, namo viunoni pake alikuwa amefunga mshipi wa dhahabu ya Ufazi.[#Ez. 9:2; Ufu. 1:13-15.]
6Mwili wake ulikuwa kama kito cha Tarsisi, uso wake ulionekana kuwa kama umeme, nayo macho yake yalikuwa kama mienge ya moto, mikono yake na miguu yake ilimerimeta kama shaba iliyokatuliwa, sauti ya kusema kwake ikawa kama uvumi wa watu wengi.
7Mimi Danieli nikayaona peke yangu hayo yaliyooneka hapo, lakini mwenzangu waliokuwa nami hawakuyaona hayo kwa kupigwa na bumbuazi kabisa; ndipo, walipokimbia, wajifiche.
8Mimi nikasalia peke yangu, nami nilipoyaona hayo makuu, yalivyooneka, haikusalia nguvu mwangu, nayo yaliyokuwa mazuri kwangu yakageuka kuwa mabaya, nguvu zangu zikanipotea kabisa.
9Nikasika sauti ya maneno yake, tena papo hapo, nilipoisikia sauti ya maneno yake, nikashikwa na usingizi kabisa, nikaanguka kifudifudi, uso wangu ukaelekea chini.[#Dan. 8:17-18.]
10Mara mkono ukanigusa, ukanisaidia kuinuka, kwa kuwa magoti na viganja vya mikono vilikuwa vikitetemeka.
11Kisha akaniambia: Danieli, ndiwe mtu wa kupendezwa naye; yatambue hayo maneno, mimi nitakayokuambia, ukisimama hapohapo, unaposimama! kwani nimetumwa kwako. Aliponiambia neno hili, nikainuka na kutetemeka.
12Akaniambia: Usiogope, Danieli! Kwani tangu siku ya kwanza, ulipojipa moyo wa kutaka utambuzi kwa kujinyenyekeza mbele ya Mungu wako, maneno yako yamesikiwa, nami nimekuja kwa hayo maneno yako.
13Lakini mkuu wa ufalme wa Persia akasimama mbele yangu na kunipingia siku ishirini na moja; mara Mikaeli aliye miongoni mwao wakuu wenyewe akaja kunisaidia, nilipokuwa nimeachwa peke yangu kushindana nao wafalme wa Persia.[#Dan. 10:20-21.]
14Sasa nimekuja, nikutambulishe, yatakayowapata walio ukoo wako siku za mwisho; kwani ono hili ni la siku zisizotimia bado.[#Dan. 9:22.]
15Aliponiambia maneno haya, nikauelekeza uso wangu chini, maana sikuweza kusema.
16Mara yeye aliyefanana na wana wa watu akaigusa midomo yangu na kukifumbua kinywa changu; ndipo, nilipoweza kusema tena, nikamwambia aliyesimama mbele yangu: Bwana wangu, kwa hayo niliyoyaona, mastusho yakaniguia, nikageuka, nguvu zangu zikanipotea kabisa.[#Yes. 6:7; Yer. 1:9.]
17Mimi niliye mtumwa wa Bwana wangu nitawezaje kusema na wewe uliye Bwana wangu? Kwani kwangu mimi hakuna nguvu zilizoko bado, wala pumzi haikusalia mwangu.
18Ndipo, yeye aliyefanana na mtu aliponigusa tena, akanitia nguvu,
19akaniambia: Usiogope! Ndiwe mtu wa kupendezwa naye; tulia tu na kujipa moyo, nguvu zikurudie! Aliponiambia haya, ndipo, nilipopata nguvu, nikamwambia: Bwana wangu na aseme! Kwani umenitia nguvu.[#Ufu. 1:17.]
20Akauliza: Unajua, kama ni kwa sababu gani, nikikujia? Sasa nitarudi kupigana naye mkuu wa Persia. Hapo, nitakapotoka kwake, papo hapo atakuja mkuu wa Ugriki.[#Dan. 10:13.]
21Lakini kwanza nitakueleza yaliyoandikwa katika kitabu cha kweli. Hakuna hata mmoja ajipaye moyo wa kunisaidia kupigana nao hao, ila mkuu wenu Mikaeli.