The chat will start when you send the first message.
1Lakini nami nalisimama upande wake katika mwaka wa kwanza wa Mmedi Dario, nikamsaidia kwa kumtia nguvu.
2Sasa nitakuonyesha yatakayokuwa kweli: Tazama, watandokea bado wafalme watatu wa Persia, wa nne atakuwa mwenye mali nyingi sana kuliko wote; kwa hizo nguvu zake, atakazozipata kwa mali zake nyingi, atawainua wote kuuendea ufalme wa Ugriki.[#Dan. 10:21.]
3Kisha ataondokea mfalme mwenye nguvu za kupiga vita, naye atatawala kwa uwezo mwingi, atafanya yatakayompendeza.
4Lakini hapo, atakapokwisha kuondokea, ufalme wake utavunjika, ukatwe vipande kwenye pepo zote nne za mbinguni; lakini hautakuwa wao walio uzao wake, wala hapatakuwa atakayetawala, kama yeye alivyotawala, kwani ufalme wake utang'olewa, uwe wa wengine, wale wasiupate.[#Dan. 8:8,22.]
5Kisha mfalme wa kusini atapata nguvu, lakini mmoja wa wakuu wake atapata nguvu kumshinda mwenyewe, kisha atatawala kwa uwezo, nao ufalme wake utakuwa mkubwa.
6Miaka itakapopita, watafanya mapatano, naye binti mfalme wa kusini atakwenda kwake mfalme wa kaskazini kutengeneza matengenezo, lakini naye yule binti mfalme nguvu za mkono wake zitampotea, yule mfalme asikae na nguvu za mkono; ndipo, yule binti mfalme atakapotolewa pamoja nao waliompeleka na mzazi wake naye aliyemtia nguvu siku zile.
7Kisha pataondokea mahali pake chipukizi la shina lake; yeye atamwendea mwenye vile vikosi, aingie bomani mwa mfalme wa kaskazini na kumfanyizia vita, nazo nguvu zake zitamshinda yule.
8Ndipo, atakapoichukua miungu yao na vinyago vyao na vyombo vyao viwapendezavyo vya fedha na vya dhahabu, ataviteka na kuvipeleka Misri, kisha atakaa miaka na miaka, asimwendee tena mfalme wa kaskazini.
9Lakini yule atakuja, auingie ufalme wa mfalme wa kusini, kisha atarudi katika nchi yake.
10Lakini wanawe watatengeneza vita wakikusanya vikosi vingi mno vivumavyo; kisha mmoja atakwenda kuifurikia na kuieneza hiyo nchi, katika safari ya pili atapeleka vita mpaka bomani kwake.
11Ndipo, mfalme wa kusini atakapochafuka kwa uchungu, atoke kupigana naye mfalme wa kaskazini; yule ataleta vikosi vingi, lakini vitatiwa mkononi mwake huyu;
12ndipo, vitakapochukuliwa, ingawa viwe vingi. Naye moyo wake utajikuza, lakini hatashinda kabisa, ijapo aangushe maelfu na maelfu.
13Mfalme wa kaskazini atarudi na kuleta vikosi vilivyo vingi kuliko vile vya kwanza. Siku nyingi na miaka itakapopita, atakuja navyo hivyo vikosi vikubwa vyenye mata mengi.
14Siku hizo wengi watamwinukia mfalme wa kusini, hata wana wao walio ukoo wako wenye ukorofi watainuka, wayatimize mambo uliyoyaona, lakini watajikwaa, waanguke.
15Ndipo, mfalme wa kaskazini atakapokuja, atamzungushia ukingo wa mchanga, auteke mji wake ulio na boma. Ndipo, itakapokuwa, mikono yao wakusini isishupae, hata mafundi wake wa vita wasiwe na nguvu za kusimama.
16Naye yeye amjiaye atafanya, kama anavyopendezwa, kwani hatakuwako atakayesimama mbele yake. Hata katika nchi hiyo yenye utukufu atakaa, mikono yake ikiiangamiza.[#Dan. 8:9.]
17Kisha atauelekeza uso wake kuja huko na enzi yote ya ufalme wake, afanye mapatano naye akimpa mwanawe, awe mkewe, aiangamize nchi hiyo, lakini jambo hili halitakuwa, hatafanikiwa.
18Kisha atauelekeza uso wake kwenda kupiga vita katika nchi za baharini, nazo nyingi ataziteka. Lakini huko kutakuwa na mpiga vita atakayeyakomesha matusi yake, asitukane tena, akimlipisha hayo matusi.
19Kisha atauelekeza uso wake kwenda kuiteka miji yenye maboma katika nchi yake; ndipo, atakapojikwaa na kuanguka, asionekane tena.
20Mahali pake ataondokea mwingine atakayetuma mtoza kodi penye utukufu wa ufalme wake; lakini kwa muda wa siku chache atavunjwa, lakini haitakuwa kwa ukali wa mtu wala kwa mapigano.
21Mahali pake ataondokea mtu abezwaye, wasiyempa macheo ya ufalme; naye atauingia kwa kuja kwa upole, aushike ufalme kwa kujitendekeza na kusema maneno matamu.[#Dan. 8:23.]
22Kisha wale wenye mikono ya nguvu waliokuja kumfurikia watafurikiwa naye na kuvunjwa, vilevile naye mkuu aliyefanya maagano naye.
23Papo hapo atakapokwisha kufanya urafiki naye, atamdanganya akimjia na kumshinda, ijapo awe na watu wachache tu.
24Kwa upole ataziingia nchi zenye manono, afanye mambo, wasiyoyafanya baba zake wala baba za baba zake, akitapanya kwao mapokonyo na mateka na mali zo zote, miji yenye maboma akiiwazia mizungu ya kuipata, lakini vitakuwa siku hizo tu zilizokatwa.
25Kisha ataviinua vikosi vyake kwa kujipa moyo wa kumwendea mfalme wa kusini kwa hizo nguvu kuu za vikosi vyake. Naye mfalme wa kusini atatengeneza vita na kuvipanga vikosi vyake vikubwa vilivyo vyenye nguvu kabisa, lakini hatashinda; kwani watakaomwazia mawazo ya njama
26ndio wanaokula naye vilaji vyake vya urembo; wao ndio watakaomvunja, vikosi vyake navyo vitatawanyika po pote, wengi wao watakufa kwa kuumizwa.
27Kisha hao wafalme wawili wataielekeza mioyo yao kufanyiana mabaya, wataambiana maneno ya uwongo wakikaa mezani pamoja, lakini hawatafanikiwa, kwani mwisho utakuja siku zilezile zilizokwisha kukatwa.
28Kisha atarudi katika nchi yake na kuchukua mali nyingi, lakini moyo wake utataka kulitengua Agano takatifu, naye atafanya, kisha atarudi katika nchi yake.
29Siku zilizokatwa zitakapotimia, atairudia nchi ya kusini, lakini safari hii ya pili haitakuwa, kama ya kwanza ilivyokuwa.
30Kwani merikebu za Wakiti zitamjia; ndipo, moyo utakapompotea. Basi, atarudi, alitolee Agano takatifu makali yake, kisha atarudi akiwatazamia walioliacha hilo Agano takatifu.
31Kisha mikono yao, aliowaweka huko, itapachafua Patakatifu palipokuwa boma la nguvu, watayakomesha matambiko ya kila siku, kisha wataweka hapo mwangamizaji atapishaye.[#Dan. 9:27; 12:11; Mat. 24:15.]
32Nao walioacha kulicha lile Agano atawashurutisha kwa maneno madanganyifu, wamwache naye Mungu, lakini hao wamjuao Mungu wao watajipatia nguvu za kufanya yawapasayo.
33Kisha hao wenye ujuzi huo watatambulisha wengine wengi, ijapo waumizwe vibaya siku nyingi kwa panga na kwa mioto na kwa mafungo ya kuhamishwa na kwa kunyang'anywa.[#Dan. 12:3.]
34Watakapoumizwa hivyo watasaidiwa kidogo tu, kwani wengi wataandamana nao kwa kujitendekeza tu.
35Namo miongoni mwao hao wenye ujuzi wengine watajikwaa, wapate kuyeyushwa, kusudi watakaswe na kueuliwa, mpaka siku za mwisho zitakapotimia, nao utakuja siku zilezile zilizokwisha kukatwa.
36Mfalme yule atafanya, kama anavyopendezwa, atajivuna na kujiwazia kuwa mkuu kuliko mungu wo wote, aseme maneno ya kustaajabisha kwa kumbeza naye Mungu aishindaye miungu; naye atayaendesha mambo hayo, mpaka siku za makali zitakapotimia, k kwani aliyotakiwa hayana budi kufanyika.[#Dan. 7:8,25; 2 Tes. 2:4; Ufu. 13:5-6.]
37Nayo miungu ya baba zake haiangalii, wala mungu wa kike upendezao wanawake, wala mungu wo wote mwingine hamwangalii, kwani anajiwazia kuwa mkuu kuliko yote.[#1 Tim. 4:3.]
38Mahali pao atamheshimu mungu wa maboma nao mungu, baba zake wasiyemjua, atamheshimu kwa kumtolea dhahabu na fedha na vito na vitu vingine vipendezavyo.
39Katika miji yenye maboma atafanya hivyo kwa ajili ya huyo mungu mgeni: atakayemwungama atampa macheo mengi, tena atampa watu wengi kuwatawala, nayo nchi atamgawia kuwa malipo yake.
40Siku za mwisho mfalme wa kusini atapigana naye; ndipo, naye mfalme wa kaskazini atakapomkimbilia kama upepo wa kimbunga kwa magari pamoja na wapanda farasi na kwa merikebu nyingi, aziingie hizo nchi na kuzifurikia na kuzieneza.
41Kisha ataiingia nayo hiyo nchi yenye utukufu; ndipo, nchi nyingi zitakapoangamizwa; zitakazopona mikoni mwake ni za Edomu na za Moabu na wakuu wao wana wa Amoni.[#Dan. 11:16.]
42Kisha ataukunjua mkono wake, aziteke hizo nchi; hapo nchi ya Misri nayo haitapata kupona.
43Namo mikononi mwake mwenye nguvu vitakuwamo vilimbiko vya dhahabu na vya fedha na vyombo vyote vya Misri vipendezavyo; kwa hiyo nao Walibia na Wanubi watamfuata.
44Lakini habari zitokazo upande wa maawioni kwa jua na wa kaskazini zitamstusha; ndipo, atakapoondoka kwa makali makubwa yenye moto, aje kuangamiza na kutowesha wengi.
45Atalipiga hema lake la kifalme katikati ya bahari na ya mlima wenye utukufu na utakatifu; ndipo, mwisho wake utakapokuja, lakini hatakuwako atakayemsaidia.