Danieli 12

Kitabu cha mambo ya ufunuo kinafungwa na kutiwa muhuri.

1Siku zile atatokea Mikaeli aliye mkuu mwenyewe anayewasimimia wana wao walio ukoo wako, kwa maana zitakuwa siku za maumivu yasiyokuwa bado tangu mwanzo wa kuwapo kwa watu, wala hayatakuwa mpaka siku zile. Lakini walio ukoo wako watapona, ni wao wote watakaoonekana, ya kuwa wameandikwa katika kile kitabu.[#Dan. 10:13; 2 Mose 32:32; Mat. 24:21; Fil. 4:3.]

2Nao wengi walalao ndani ya nchi uvumbini wataamka, wengine kupata uzima wa kale na kale, wengine kutwezwa na kuchukizwa kale na kale.[#Yoh. 5:29.]

3Ndipo, wafunzi watakapoangaza kama mwangaza wa mbinguni, nao walioongoza wengi, wapate wongofu, wataangaza kama nyota kale na kale zamani zote.[#Mat. 13:43; 1 Kor. 15:41-42.]

4Nawe wewe Danieli, yafunge haya maneno, nacho kitabu kitie muhuri, mpaka siku za mwisho zitakapotimia! Ndipo, wengi watakapokichunguza, utambuzi wao uongezeke.[#Dan. 12:9; Ufu. 10:4.]

5Mimi Danieli nilipotazama nikaona wengine waliosimama hapo, mmoja upande wa huku ukingoni kwa hilo jito, mmoja upande wa huko ukingoni kwa hilo jito.

6Mmoja akamwuliza yule mume aliyevaa nguo nyeupe ya ukonge aliyesimama juu ya maji ya hilo jito: Itakuwa mpaka lini, mwisho wa maajabu hayo utakapotimia?[#Dan. 10:5.]

7Nikamsikia yule mume aliyevaa nguo nyeupe ya ukonge, aliyesimama juu ya maji ya hilo jito, akauinua mkono wake wa kuume nao wa kushoto kuielekeza mbinguni, akaapa na kumtaja yule Mwenye uzima wa kale na kale kwamba: Bado kipande cha siku na vipande vya siku na nusu; hapo nguvu za mikono yao walio wa ukoo mtakatifu zitakapokwisha kupondeka, ndipo, hayo yote yatakapotimizwa.[#Dan. 7:25; Ufu. 10:5-6.]

8Nikayasikia mimi, lakini sikuyatambua, nikamwuliza: Bwana wangu, mwisho wa mambo hayo utakuwaje?

9Akasema: Jiendee, Danieli! Kwani maneno haya yamefungwa na kutiwa muhuri, mpaka siku za mwisho zitakapotimia.

10Wengi watatakaswa na kueuliwa kwa kuyeyushwa, lakini wasiomcha Mungu watafanya maovu yao. Kwao hao hatakuwako hata mmoja atakayeyatambua hayo; ndio watakaoyatambua ni wao wenye ujuzi.

11Tangu hapo, matambiko ya kila siku yatakapoondolewa, mahali pao pawekwe mwangamizaji atapishaye, ni siku 1290.[#Dan. 11:31; Mat. 24:15.]

12Mwenye shangwe atakuwa angojeaye, afikishe siku 1335!

13Basi, wewe jiendee, uufikie mwisho! Utatulia, upate kuliinukia fungu lako, siku za mwisho zitakapotimia.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania