Danieli 4

Ndoto nyingine ya mfalme Nebukadinesari na maana yake.

1Mfalme Nebukadinesari akawaandikia makabila na koo zote, wao wote wenye ndimi za watu wanaokaa katika nchi yote nzima, kwamba: Utengemano wenu na uwe mwingi!

2Vielekezo na vioja, Mungu Alioko huko juu alivyonifanyia, imenipendeza kuvieleza.

3Vistaajabuni vielekezo vyake vilivyo vikuu! Navyo vioja vyake vilivyo vya nguvu! Ufalme wake ni ufalme wa kale na kale, nayo enzi yake ni ya vizazi na vizazi.[#Dan. 6:26.]

4Mimi Nebukadinesari nalitulia nyumbani mwangu, nikawapo na kufanikiwa katika jumba langu kuu.

5Nikaota ndoto iliyonistusha, nayo mawazo yaliyonijia, nilipolala kitandani, nayo maono ya macho yangu yakanitia woga.

6Amri ikatoka kwangu ya kuniletea wajuzi wote wa Babeli, wanijulishe maana ya ndoto.

7Kwa hiyo wakaniletea waandishi na waaguaji na Wakasidi na wachunguza nyota, mimi nikawaambia ndoto, lakini hawakunijulisha maana yake.[#Dan. 2:2.]

8Mwisho akatokea mbele yangu Danieli aliyeitwa Beltesasari kwa jina la mungu wangu, namo mwake imo roho ya miungu mitakatifu, nikamwambia ndoto nikisema:[#Dan. 5:11,14.]

9Beltesasari, mkuu wa waandishi, mimi ninakujua, ya kuwa roho ya miungu mitakatifu imo mwako, hakuna fumbo linalokusumbua; hii ni ndoto, niliyoiota, niambie maana yake![#Ez. 28:3.]

10Maono niliyoyaona kwa macho yangu, nilipolala kitandani, ni haya: nilikuwa nikitazama, mara nikaona mti katika nchi, uliokuwa mrefu sana kwa kimo chake.[#Ez. 31:3-14.]

11Mti huo ukaendelea kukua na kupata nguvu, mpaka kilele chake kifike mbinguni, ukaonekana hata mapeoni kwa nchi.

12Majani yake yalikuwa mazuri, matunda yake yakawa mengi, vyakula vilivyopatikana kwake vikawatoshea watu wote pia, chini yake kivulini wakatua nyama wote wa porini, katika matawi yake ndege wa angani wakajenga viota vyao; hivyo wote wenye miili wakaushiba.[#Dan. 4:21; Ez. 17:23.]

13Nilipokuwa ninautazama katika maono, niliyoyaona kwa macho yangu nilipolala kitandani, mara nikaona, mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni.

14Akaita kwa sauti ya nguvu kwamba: Ukateni mti huu! Yachanjeni matawi yake! Majani yake yapukuseni! Matunda yake yatapanyeni, nyama wakimbie chini yake, hata ndege waondoke katika matawi yake! Majani yake yapukuseni! Matunda yake yatapanyeni, nyama wakimbie chini yake, hata ndege waondoke katika matawi yake![#Dan. 4:23.]

15Lakini shina lenye mizizi yake liacheni mchangani, likiwa limefungwa kwa vyuma na kwa shaba katika mbuga yenye majani mabichi, liloweshwe na umande wa mbinguni, yale majani ya nchi yawe fungu lake, nalo lao nyama.

16Moyo wake utageuzwa, usiwe wa kimtu tena, apewe moyo wa kinyama, mpaka miaka saba ipite, akiwa hivyo.[#Dan. 7:25.]

17Kwa shauri la walinzi imekuja amri hii, yakafanyika kwa agizo lao watakatifu, kusudi walioko uzimani watambue kwamba: Yule Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye humpa ampendaye, naye aliye mnyenyekevu kwa watu humwinua, aupate.[#Dan. 2:21.]

18Ndoto hii nimeiota mimi mfalme Nebukadinesari, nawe Beltesasari iseme maana yake, kwa kuwa wajuzi wote wa ufalme wangu hawakuweza kunijulisha maana yake lakini wewe utaweza, kwani roho ya miungu mitakatifu imo mwako.

19Kisha Danieli aliyeitwa jina lake Beltesasari akapigwa bumbuazi kitambo kidogo, mawazo yake yakamstusha; ndipo, mfalme alipomwambia Beltesasari kwamba: Ndoto na maana yake isikustushe! Beltesasari akamjibu akasema: Bwana wangu, ningependa, ndoto hii iwe yao wakuchukiao, nayo maana yake iwapate wakuinukiao!

20Umeona mti uliokuwa mkubwa na wenye nguvu, uliofika hata mbinguni kwa kilele chake, uliooneka katika nchi yote nzima;

21majani yake mazuri na matunda yake yakawa mengi, vyakula vilivyopatikana kwake vikawatoshea watu wote pia, chini yake kivulini wakapanga nyama wote wa porini, katika matawi yake wakakaa ndege wa angani.

22Wewe mfalme ndiwe mti huo, kwani u mkuu mwenye nguvu, ukuu wako umekua, ukafika hata mbinguni, ukatawala mpaka kwenye mapeo ya nchi.

23Tena mfalme ameona, mlinzi mtakatifu akishuka kutoka mbinguni, akasema: Ukateni mti huu na kuuangamiza! Lakini shina lenye mizizi yake liacheni mchangani, likiwa limefungwa kwa vyuma na kwa shaba katika mbuga yenye majani mabichi, liloweshwe na umande wa mbinguni, fungu lake liwe lao nyama wa porini, mpaka miaka saba ipite, akiwa hivyo.

24Hii ndiyo maana yake, mfalme: ni shauri lake Alioko huko juu, alilomkatia bwana wangu mfalme.

25Watakufukuza kwenye watu, ukae pamoja na nyama wa porini, tena watakulisha majani kama ng'ombe, nao umande wa mbinguni utakulowesha, miaka saba ipite, ukiwa hivyo, mpaka utakapotambua kwamba: Yule Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye humpa ampendaye.

26Hapo wakisema, waliache shina lenye mizizi yake huo mti, ni kwamba: Ufalme wako utakurudia tena hapo, utakapojua, ya kuwa mbingu ndizo zitawalazo.

27Kwa hiyo, mfalme, shauri langu likupendeze: makosa yako yalipe kwa kutenda wongofu! Nayo maovu, uliyoyafanya, yalipe kwa kuwahurumia wanyonge! Hivyo utulivu wako utakuwa wa siku nyingi.[#Fano. 19:17; Mat. 5:7; 19:21.]

Mfalme Nebukadinesari anaingiwa na kichaa; alipopona anamsifu Mungu.

28Hayo yote yakampata mfalme Nebukadinesari.

29miezi kumi na miwili ilipopita, siku moja alipotembea huko Babeli jumbani mwake mwa kifalme juu,

30ndipo, mfalme aliposema kwamba: Kumbe huu sio mji mkubwa wa Babeli, nilioujenga mimi kuwa kao la kifalme kwa nguvu ya uwezo wangu, utukufu wangu utukuzwe![#Fano. 16:18; Tume. 12:23.]

31Neno hili lilipokuwa lingalimo kinywani mwa mfalme, sauti ikatoka mbinguni kwamba: Wewe mfalme Nebukadinesari, unapashwa habari, ya kuwa ufalme umekwisha kuondoka kwako.

32Watakufukuza kwenye watu, ukae pamoja na nyama wa porini, tena watakulisha majani kama ng'ombe; miaka saba itapita, ukiwa hivyo, mpaka utakapotambua kwamba: Yule Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye humpa ampendaye.[#Dan. 5:21.]

33Papo hapo neno hilo likamtimilikia Nebukadinesari: akafukuzwa kwenye watu, akalishwa majani kama ng'ombe, mwili wake ukaloweshwa na umande wa mbinguni, mpaka nywele zake zikawa ndefu kama manyoya ya tai, nazo kucha zake zikawa ndefu kama za ndege.

34Siku hizo zilipopita, ndipo, mimi Nebukadinesari nilipoyaelekeza macho yangu mbinguni; ndipo, akili zangu ziliporudi kwangu, nikamtukuza yule Alioko huko juu, nikamsifu na kumheshimu aliye Mwenye uzima wa kale na kale, ukuu wake wa kutawala ni wa kale na kale, nao ufalme wake ni wa vizazi na vizazi.[#Dan. 3:23.]

35Wote wakaao nchini huwaziwa kuwa si kitu, yampendezayo huyafanya kwa vikosi vya mbinguni nako kwao wakaao nchini, tena hakuna awezaye kuuzuia mkono wake na kumwuliza: Unafanya nini?

36Papo hapo, akili zangu ziliporudi kwangu, nikapewa enzi yangu na utukufu wangu, ufalme wangu upate kutukuzwa. Wasemaji wangu wa shaurini na wakuu wangu wakanitafuta, nikarudishwa katika ufalme wangu, ukuu wangu ukaongezwa, ukazidi sana.

37Sasa mimi Nebukadinesari ninamsifu mfalme wa mbinguni na kumkuza na kumtukuza, kwani matendo yake yote ni ya kweli, njia zake ni za wongofu, nao waendeleao kujikuza anaweza kuwanyenyekeza.[#Dan. 5:20; Luk. 1:51; 18:14.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania