The chat will start when you send the first message.
1Mfalme Belsasari aliwafanyia wakuu wake elfu karamu kubwa, akanywa mvinyo mbele yao hao elfu.[#Dan. 7:1.]
2Belsasari alipokwisha kuonjaonja mvinyo akaagiza, wavilete vile vyombo vya dhahabu na vya fedha, baba yake Nebukadinesari alivyovichukua katika Jumba takatifu huko Yerusalemu, kwamba mfalme na wakuu wake na wakeze na masuria zake wanywee mumo humo.[#Dan. 1:2; 2 Mambo 36:10.]
3Kwa hiyo wakavileta vile vyombo vya dhahabu, walivyovichukua katika Jumba takatifu la Mungu huko Yerusalemu, mfalme na wakuu wake na wakeze na masuria zake wakanywea mumo humo.
4Walipokunywa mvinyo wakaisifu miungu ya dhahabu na ya fedha na ya shaba na ya chuma na ya miti na ya mawe.
5Mara vikatokea vidole vya mkono wa mtu, vikaandika mwangani pa taa penye chokaa ukutani mle jumbani mwa mfalme, mfalme akiuona mgongo wa mkono ulioandika.
6Ndipo, uso wake mfalme ulipokuwa mwingine, mawazo yake yakamstusha, maungo ya viuno vyake yakalegea, nayo magoti yake yakagonganagongana.
7Mfalme akalia kwa sauti kuu, wamletee waaguaji na Wakasidi na wachunguza nyota, kisha mfalme akawaambia hao wajuzi wa Babeli akisema: Mtu ye yote atakayeyasoma maandiko haya na kunieleza maana yake atavikwa nguo za kifalme, napo shingoni pake atapata mkufu wa dhahabu, naye atakuwa mwenye kutawala wa tatu katika ufalme.[#Dan. 2:2; 4:6.]
8Basi, wakaingia wajuzi wote wa Babeli, lakini hawakuweza kuyasoma hayo maandiko wala kumjulisha mfalme maana yake.
9Ndipo, mfalme Belsasari alipozidi kustuka, nao uso wake ukawa mwingine kabisa, nao wakuu wake wakapotelewa na mizungu.
10Kwa ajili ya hayo maneno ya mfalme na ya wakuu wake mamake mfalme akaja mle chumbani, walimonywea, kisha mamake mfalme akasema kwamba: Wewe mfalme na uwe mwenye uzima kale na kale! Mawazo yako yasikustushe, wala uso wako usiwe mwingine!
11Katika ufalme wako yuko mtu mwenye roho ya miungu mitakatifu, hata siku za baba yako kwake yeye ulioneka mwangaza na utambuzi na ujuzi uliofanana na ujuzi wa miungu, baba yako Nebukadinesari akamweka kuwa mkuu wao waandishi na waaguaji na Wakasidi na wachunguza nyota, kweli baba yako mfalme aliyafanya.[#Dan. 4:8.]
12Kwani mwake imo roho kuu na akili na utambuzi wa kutambua maana ya ndoto na wa kufumbua mafumbo na wa kuvumbua njia zilizo ngumu za kuziona; roho hiyo imo mwake Danieli, mfalme aliyemwita jina lake Beltesasari. Basi, huyo Danieli na aitwe, yeye ataifumbua maana.[#Ez. 28:3.]
13Kisha Danieli akapelekwa mbele yake mfalme, mfalme akamwuliza Danieli akisema: Wewe ndiwe Danieli, mmoja wao Wayuda, baba yangu mfalme aliowateka na kuwahamisha kuja huku akiwatoa katika nchi ya Yuda?
14Nimesikia habari zako, ya kuwa roho ya miungu imo mwako, kwa hiyo mwako unaoneka mwangaza na utambuzi na ujuzi mwingi sana!
15Sasa hapa wajuzi na waaguaji wameletwa mbele yangu, wayasome maandiko haya, wanijulishe maana yake, lakini hawawezi kuifumbua maana yake hilo jambo.
16Lakini habari zako wewe nimesikia, ya kuwa unaweza kusema maana na kuyavumbua yaliyofunikwa; basi, kama unaweza kuyasoma maandiko haya na kunijulisha maana yao, utavikwa nguo za kifalme, napo shingoni pako utapata mkufu wa dhahabu, tena utakuwa mwenye kutawala wa tatu katika ufalme.
17Kisha Danieli akamjibu mfalme akisema: Kaa na vipaji vyako! Umpe mwingine matunzo yako! Lakini haya maandiko nitamsomea mfalme, nayo maana yao nitamjulisha.
18Wewe mfalme, Mungu Alioko huko juu alimpa baba yako Nebukadinesari ufalme na ukuu na enzi na utukufu.[#Dan. 2:37; 4:25.]
19Kwa ajili ya ukuu, aliompa, watu wa makabila yote na wa koo zote, wao wote wenye ndimi za watu walitetemeka mbele yake kwa kumwogopa, kwani aliyetaka kumwua, akamwua; naye aliyetaka kumwacha, akamwacha kuwa mzima, naye aliyetaka kumkweza, akamkweza, naye aliyetaka kumnyenyekeza, akamnyenyekeza.
20Lakini moyo wake ulipojikuza, nayo roho yake ilipojisifu na kujivuna vibaya, ndipo, alipokumbwa katika kiti chake cha kifalme, wakamvua nao utukufu wake.[#Tume. 12:23.]
21Akafukuzwa kwenye watu, wakauwazia moyo wake kuwa kama wa nyama wa porini, akakaa pamoja na punda wa mwituni, wakamlisha majani kama ng'ombe, mwili wake ukaloweshwa na umande wa mbinguni, mpaka alipotambua, ya kuwa Mungu Alioko huko juu ndiye autawalaye ufalme wa watu, naye ampendaye humkweza, aupate.[#Dan. 4:35.]
22Nawe Belsasari u mwanawe, lakini hukuunyenyekeza moyo wako, ingawa uliyajua hayo yote.
23Ukamwinukia Bwana wa mbinguni, ukavitaka hivi vyombo vya Nyumba yake, wakutolee, wewe unywee mumo humo mvinyo pamoja na wake zako na masuria zako na wakuu wako, mkaisifu miungu ya fedha na ya dhahabu na ya shaba na ya chuma na ya miti na ya mawe isiyoona, isiyosikia, isiyojua kitu; lakini hukumtukuza Mungu azishikaye pumzi zako mkononi mwake, naye ndiye azilinganyaye njia zako zote.[#Dan. 5:2; Sh. 115:4-7.]
24Kwa hiyo ukatumwa naye huo mgongo wa mkono na haya maandiko yaliyoandikwa hapa.
25Nayo haya maandiko yaliyoandikwa hapa ni kwamba: Mene, Mene, Tekel, U-parsin
26Maana yao ni hii: Mene ni kwamba: Mungu amezihesabu siku za ufalme wako, akaukomesha
27Tekel ni kwamba: Umepimwa kwa mizani, ukaoneka kuwa mwepesi.
28Peresi ni kwamba: Ufalme wako umegawanyika, wakapewa Wamedi na Wapersia.
29Kisha Belsasari akatoa amri, wakamvika Danieli nguo za kifalme na mkufu wa dhahabu shingoni, wakatangaza, ya kuwa atakuwa mwenye kutawala wa tatu katika ufalme.[#Dan. 2:48; 1 Mose 41:42-43.]
30Usiku uleule Belsasari, mfalme wa Wakasidi, akauawa.
31Ufalme wake akauchukua Mmedi Dario, naye alikuwa mwenye miaka kama 62.[#Dan. 9:1; Yes. 13:17.]