Danieli 6

Danieli pangoni mwa simba.

1Kwa mapenzi yake Dario akaweka watawala nchi 120 wa kuuangalia ufalme, wakiwa po pote katika huo ufalme.

2Hao nao akawapatia wakuu watatu, mmoja wao akawa Danieli; wale watawala nchi hawakuwa na budi kuwatolea hawa hesabu, mfalme asipotelewe na mali.

3Ndipo, huyu Danieli alipowashinda wakuu wenziwe na watawala nchi, kwa kuwa Roho iliyo kuu ilikuwa mwake, naye mfalme akafikiri kumpa ufalme wote, auangalie.[#Dan. 5:12.]

4Kwa hiyo wakuu na watawala nchi wakatafuta jambo la kumwonea Danieli kwamba: anaukosea ufalme, lakini hawakupata jambo lo lote la kumwonea kwamba: amefanya vibaya, kwa kuwa alikuwa mwelekevu, halikuonekana kwake kosa lo lote wala tendo baya.

5Ndipo, hao waume waliposema: Kwake Danieli hatutapata jambo lo lote la kumwonea, tusipomwonea kwa hivyo, anavyomcha Mungu wake.

6Kisha wale wakuu na watawala nchi wakamwendea mfalme na kumpigia shangwe, wakamwambia: Mfalme Dario na uwe mwenye uzima kale na kale![#Dan. 3:9; 5:10.]

7Liwali wote wa ufalme na wakuu na wenye amri na wasemaji wa shaurini na watawala nchi wamepiga shauri pamoja kwamba: Itolewe amri ya mfalme na kutisha watu kwa ukali wa kwamba: Kila mtu atakayemwomba mungu wo wote au mtu muda wa siku thelathini, asikuombe wewe mfalme, atatupwa pangoni mwa simba.

8Sasa, mfalme, itoe amri hii ya huo mwiko, kaiandike kitabuni, isiwezekane kugeuzwa kwa hivyo, maongozi ya Wamedi na ya Wapersia yalivyo, wala isitanguliwe.[#Dan. 6:15; Est. 1:19; 8:8.]

9Kwa sababu hiyo mfalme Dario akaiandika amri hiyo ya kutisha watu kwa ukali.

10Danieli aliposikia, ya kuwa hiyo amri imeandikwa, akaingia nyumbani mwake. Humo katika chumba cha juu yalikuwamo madirisha yaliyokuwa wazi kuuelekea Yerusalemu; ndimo, alimopigia magoti kila siku mara tatu akiomba na kumshukuru Mungu wake sawasawa, kama alivyovifanya siku za mbele.[#1 Fal. 8:48; Yer. 51:50; Sh. 55:18.]

11Kisha wale waume wakamwendea kwa kushangilia mioyoni, wakamwona Danieli, alivyomwomba Mungu wake na kumlalamikia.

12Kisha wakamkaribia mfalme, wakamwambia kwa ajili ya ile amri ya mfalme: Hukuandika amri ya kutisha watu kwamba: Kila mtu atakayemwomba mungu wo wote au mtu muda wa siku thelathini, asipokuomba wewe mfalme, atatupwa pangoni mwa simba? Mfalme akaitikia, akasema: Neno hili ni la kweli kabisa, haliwezekani kutanguliwa kwa hivyo, maongozi ya Wamedi na ya Wapersia yalivyo.[#Dan. 3:10.]

13Kisha wakamjibu mfalme na kumwambia: Danieli aliye mmoja wao Wayuda waliotekwa na kuhamishwa kuja huku, hakuchi, wala haishiki amri yako, mfalme, ya kutisha watu, uliyoiandika, ila huomba maombo yake kila siku mara tatu.

14Mfalme alipolisikia neno hili, halikumpendeza kabisa, akafikiri moyoni, jinsi atakavyomwokoa Danieli; mpaka jua likiingia, akawa akihangaikia mizungu ya kumponya.

15Ndipo, wale waume walipomwendea mfalme na kushangilia mioyoni, wakamwambia mfalme: Unajua, mfalme, ya kuwa kwa maongozi yetu Wamedi na Wapersia haiwezekani kugeuza katazo wala amri, mfalme aliyoitoa.

16Ndipo, mfalme alipoagiza, wamlete Danieli, wamtupe pangoni mwa simba. Naye akamwambia Danieli: Mungu wako, unayemtumikia pasipo kukoma, ndiye atakayekuokoa.[#Dan. 6:20.]

17Pakaletwa jiwe moja, likawekwa juu hapo pa kuliingilia lile pango, mfalme akalitia muhuri kwa pete yake yenye muhuri na kwa pete ya wakuu wake yenye muhuri, jambo la Danieli lisigeuzwe.

18Kisha mfalme akaenda jumbani mwake, akalala na kufunga mfungo, hata wakeze hakuwaingiza mwake, lakini usingizi hakuupata.

19Asubuhi mapema kulipopambazuka, mfalme akaondoka, akaenda na kulikimbilia lile pango la simba.

20Alipolifikia hilo pango karibu, akamwita Danieli na kupaza sauti kiwogawoga, yeye mfalme akasema na kumwuliza Danieli: Danieli uliye mtumishi wake Mungu aliye Mwenye uzima! Je? Mungu wako, unayemtumikia pasipo kukoma, ameweza kukuokoa katika simba?[#Dan. 3:17.]

21Ndipo, Danieli alipomjibu mfalme: Wewe mfalme, na uwe mwenye uzima kale na kale![#Dan. 6:6.]

22Mungu ametuma malaika wake, akavifumba vinywa vya simba, hawakuniumiza, kwa kuwa mbele yake nimeonekana kuwa mtu asiyekosa; hata mbele yako, mfalme, hakuna kiovu, nilichokifanya.[#Dan. 3:28; Ebr. 11:33.]

23Ndipo, mfalme alipomfurahia sanasana, akaagiza kumtoa Danieli pangoni; basi, Danieli alipokwisha kutolewa mle pangoni hamkuonekana mwilini mwake kidonda cho chote, kwani alimtumaini Mungu wake.[#Sh. 37:40.]

24Kisha mfalme akaagiza kuwaleta wale waume waliomchongea Danieli, wawatupe humo pangoni mwa simba, wao na wana wao na wake zao. Walipokuwa hawajafika pangoni chini, simba wakawakamata, wakawavunja mifupa yao yote.

25Kisha mfalme Dario akawaandikia watu wa makabila yote na wa koo zote, wao wote wenye ndimi za watu waliokaa katika nchi yote nzima, kwamba: Utengemano wenu na uwe mwingi!

26Kwangu inatoka amri hii: Katika ufalme wangu wote, ninaoutawala, watu sharti watetemeke mbele yake Mungu wa Danieli kwa kumwogopa. Kwani yeye ndiye Mungu Mwenye uzima akaaye kale na kale, ufalame wake hauangamii, kutawala kwake hakuna mwisho.[#Dan. 3:23.]

27Yeye huokoa na kuponya, hufanya vielekezo na vioja mbinguni na nchini, naye ndiye aliyemwokoa Danieli mikononi mwa simba.

28Kisha Danieli akapata kutulia siku za ufalme wa Dario, hata siku za ufalme wa Kiro aliyekuwa Mpersia.[#Dan. 1:21.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania