Danieli 7

Ndoto ya Danieli ya wafalme wanne na ya ufalme wa mwana wa mtu utakaokuwa wa kale na kale.

(Taz. Dan. 2.)

1Katika mwaka wa kwanza wa mfalme Belsasari, mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, akaona maono kwa macho yake alipolala kitandani. Kisha akaiandika hiyo ndoto na kuyasema mambo yake makuu.[#Dan. 5:1.]

2Basi, Danieli akayasimulia kwamba: Katika ndoto ya usiku nilikuwa nikitazama, mara nikaziona pepo nne za mbinguni zilivyoitokea Bahari Kubwa kwa nguvu.[#Ufu. 17:15.]

3Ndipo, nyama wakubwa wanne walipotoka baharini, kila mmoja wao alikuwa wa namna yake.[#Ufu. 13:1-2.]

4Wa kwanza alikuwa kama simba, lakini alikuwa na mabawa ya tai, nikamtazama, mpaka mabawa yake yakinyonyolewa manyoya, akachukuliwa nchini, akasimamishwa kwa miguu miwili kama mtu, akapewa hata moyo wa kimtu.[#Dan. 4:34.]

5Mara nikaona nyama mwingine, ndio wa pili, alifanana na nyegere, alisimama upande mmoja tu, namo kinywani mwake alishika mbavu tatu kwa meno yake, akaambiwa: Inuka, ule nyama nyingi!

6Baadaye nilipotazama tena, nikaona nyama mwingine aliyekuwa kama chui, lakini mgongoni mwake alikuwa na mabawa manne ya ndege, navyo vichwa vyake huyu nyama vilikuwa vinne, akapewa kutawala.

7Baadaye nilipotazama tena katika hayo maono ya usiku, mara nikaona nyama wa nne, akastusha na kutia woga kwa kuwa na nguvu kabisa; alikuwa na meno makubwa ya chuma, akala na kuvunjavunja, nayo yaliyosalia akayakanyagakanyaga kwa miguu yake, alikuwa mwingine kabisa, hakufanana nao nyama wa kwanza, tena alikuwa na pembe kumi.

8Nilipoziangalia hizo pembe, mara nikaona pembe nyingine ndogo iliyotokea katikati yao, nazo hizo pembe za kwanza kwao zikang'olewa tatu mbele yake hiyo, tena pembe hiyo ilikuwa yenye macho kama macho ya mtu na yenye kinywa kilichosema makuu.[#Dan. 11:36.]

9Nilipokuwa nikimtazama, vikaletwa viti vya kifalme; kisha mtu mwenye siku nyingi akaja kukaa, alikuwa amevaa nguo nyeupe zing'aazo kama chokaa juani, nazo nywele za kichwani pake zilikuwa kama manyoya ya kondoo yaliyotakata sana, kiti chake cha kifalme kilikuwa cha miali ya moto, nayo magurudumu ya kiti chake yalikuwa ya moto uwakao.[#Sh. 90:2.]

10Mto wa moto ukaja, ukaijiendea na kutoka mbele yake; maelfu na maelfu wakamtumikia, milioni na milioni wakasimama mbele yake, wenye hukumu wakakaa, kisha vitabu vikafunuliwa.[#Sh. 68:18; Ufu. 5:11.]

11Nikawa nikitazama hapohapo kwa ajili ya makelele makubwa, ambayo iliyapiga ile pembe isemayo; nikatazama vivyo hivyo, mpaka yule nyama akiuawa, mwili wake ukaangamizwa ukitupwa motoni, uteketezwe.[#Ufu. 19:20.]

12Kisha nao wale nyama wengine walinyang'anywa nguvu zao za kutawala, kwani walikuwa wamekatiwa wingi wa siku zao za kuwapo, wasipite wala mwaka wala siku.[#Dan. 2:21.]

13Nilipokuwa nikitazama katika hayo maono ya usiku mara nikaona, alivyokuja akichukuliwa na mawingu ya mbinguni aliyekuwa kama mwana wa mtu, akafika kwake yule mwenye siku nyingi, wakimpeleka kuja mbele yake.[#Luk. 21:27.]

14Akapewa nguvu za kutawala na macheo na ufalme, watu wa makabila yote na wa koo zote, wao wote wenye ndimi za watu wamtumikie, nguvu zake za kutawala ni za kale na kale, hazina mwisho, hata ufalme wake hautaangamia.

15Roho yangu mimi Danieli ikaumia mwilini mwangu, nayo maono ya macho yangu yakanitia woga.

16Nikamkaribia mmoja wao waliosimama hapo, nikamwomba kuniambia maana ya kweli ya hayo yote; akanijibu na kunifumbulia hayo mambo kwamba:[#Dan. 7:10.]

17Nyama wale wakubwa mno walio wanne ndio wafalme wanne watakaoinuka katika nchi.

18Kisha watakatifu wake Alioko huko juu watapata ufalme, nao wataushika ufalme kale na kale, kweli siku zitakazokuja zote za kale na kale.[#Dan. 7:22.]

19Nikamwuliza tena maana ya kweli ya nyama wa nne aliyekuwa mwingine kabisa, asifanane na wenzake wote, aliyestusha kabisa kwa kuwa mwenye meno ya chuma na mwenye kucha za shaba, aliyekula na kuvunjavunja, nayo yaliyosalia aliyakanyagakanyaga kwa miguu yake.[#Dan. 7:7.]

20Nikauliza nayo maana ya zile pembe kumi za kichwani pake, nayo maana ya ile pembe nyingine, ambayo mbele yake zikang'oka pembe tatu, iliyokuwa yenye macho kama ya mtu, tena yenye kinywa kilichosema makuu; naye alionekana kuwa mkubwa kuliko wenziwe.

21Nami nilikuwa nimeona, pembe hiyo ilivyofanya vita na watakatifu na kuwashinda,[#Ufu. 13:7.]

22mpaka yule mwenye siku nyingi alipokuja; ndipo, watakatifu wake Alioko huko juu walipopewa kuhukumu, ndipo, siku zao watakatifu zilipotimia za kuushika ufalme.

23Akaniambia haya: Huyo nyama wa nne ndio ufalme wa nne utakaokuwa katika nchi, nao utakuwa mwingine, usifanane na ufalme wote, utaila nchi yote nzima, utaiponda kwa kuikanyagakanyaga.

24Nazo zile pembe kumi ni kwamba: Katika ufalme huo watainuka wafalme kumi; nyuma yao atainuka mwingine asiyefanana na wenzake waliokuwa mbele yake, naye ataangusha chini wafalme watatu.[#Ufu. 17:12.]

25Tena atasema maneno ya kumbeza Alioko huko juu, nao watakatifu wake Alioko huko juu atawapondaponda; tena atajipa moyo wa kuzigauza sikukuu, atoe nyingine, hata maongozi, atoe mengine. Nao watakatifu watatiwa mikononi mwake kipande cha siku na vipande viwili vya siku na nusu ya kipande cha siku.[#Dan. 4:16; 12:7; Ufu. 13:5-6.]

26Zitakapokwisha atahukumiwa, wamnyang'anye nguvu zake za kutawala, wazitoweshe na kumwangamiza kabisa.

27Ndipo, ufalme na nguvu za kutawala na ukuu wa ufalme wote ulioko chini ya mbingu utakapopewa ukoo wa watakatifu wake Alioko huko juu, ufalme wake ni wa kale na kale, nazo nguvu zote zitawalazo zitamtumikia na kumtii.

28Huu ndio mwisho wa hilo jambo. Mimi Danieli mawazo yangu yakanitisha sana, nao uso wangu ukawa mwingine, nikaliweka jambo hilo moyoni mwangu.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania