Danieli 9

Danieli anawaombea Waisiraeli.

1Katika mwaka wa kwanza wa Dario, mwana wa Ahaswerosi, aliyekuwa wa kizazi cha Wamedi, aliyepata kuwa mfalme wa ufalme wa Wakasidi,[#Dan. 5:31.]

2basi, katika mwaka wa kwanza wa ufalme wake, mimi Danieli niliiangalia hesabu ya miaka katika vitabu, ambayo Neno lake Bwana lilimwambia mfumbuaji Yeremia, ya kuwa miaka 70 itamalizika, Yerusalemu ikikaa kuwa mabomoko.[#Yer. 25:11-12.]

3Ndipo, nilipouelekeza uso wangu kwake Bwana Mungu, nipate kumwomba na kumlalamikia nikifunga mfungo na kuvaa gunia na kukaa majivuni.

4Nikamwomba Bwana Mungu wangu nikiungana na kusema hivyo: E Bwana, ndiwe Mungu mkuu aogopeshaye, unalishika agano la kuwahurumia wakupendao na kuyashika maagizo yako.

5Tumekosa na kukora manza, tukaacha kukucha na kukutii, tukaondoka kwenye maagizo yako na maongoi yako.

6Hatukuwasikia watumishi wako wafumbuaji waliosema kwa Jina lako kwa wafalme wetu na kwa wakuu wetu na kwa baba zetu na kwa watu wa ukoo wote wa nchi hiyo.

7Wewe Bwana u mwenye wongofu, lakini sisi nyuso zinatuiva kwa soni; ndivyo, vinavyojulika leo: sisi waume wa Yuda nao wakaao Yerusalemu nao Waisiraeli wote walioko karibu nao walioko mbali katika nchi zote, ulikowatawanyia kwa ajili ya matendo yao, waliyokutendea,

8Bwana, nyuso zinatuiva kwa soni sisi na wafalme wetu na wakuu wetu na baba zetu, kwa kuwa tumekukosea wewe.[#Yes. 43:27.]

9Lakini kwake Bwana Mungu wetu ziko huruma, atuondolee makosa, ijapo tuwe tumekataa kumtii.[#Sh. 130:4.]

10Hatukuisikia sauti ya Bwana Mungu wetu, tuyafuate Maonyo yake, aliyotupa mikononi mwa watumishi wake wafumbuaji, tuyaangalie.

11Waisiraeli wote wakapita tu penye Maonyo yako, wakaenda zao pasipo kuisikia sauti yako; kwa sababu hiyo tukamwagiwa kiapizo, kikatupata nacho kiapo kilichoandikwa katika Maonyo ya Mose, mtumwa wake Mungu, kwani tulimkosea.[#3 Mose 26:14-39; 5 Mose 28:15-68.]

12Akayatimiza maneno yake, aliyoyasema ya kututisha sisi na waamuzi wetu waliotuamua ya kwamba: Atatuletea kibaya kikubwa kisichofanyika po pote chini ya mbingu, kama kitakavyofanyika Yerusalemu.

13Vikawa, kama vilivyoandikwa katika Maonyo ya Mose; hicho kibaya chote kikatujia, lakini sisi hatukujipendekeza usoni pa Bwana Mungu wetu tukiyaacha maovu, tuliyoyafanya, tujipatie kwako utambuzi wa kweli.

14Kwa hiyo Bwana akakiangalia hicho kibaya, akifikishe kwetu, kwani Bwana Mungu wetu ni mwongofu, ayanyoshe matendo yake yote, anayoyatenda. Lakini hatukuisikia sauti yake.[#Yer. 1:12.]

15*Lakini na sasa ndiwe Bwana Mungu wetu! Uliwatoa walio ukoo wako katika nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu ukajipatia Jina, kama inavyojulika leo; nasi tukakukosea, tukaacha kukucha.

16Bwana, kwa ajili ya wongofu wako wote nakuomba: Makali yako yenye moto na yarudi nyuma, yauache mji wako wa Yerusalemu, mlima wako mtakatifu ulimo! Kwani kwa ajili ya makosa yetu na kwa ajili ya manza, baba zetu walizozikora, Yerusalemu pamoja na ukoo wako umegeuka kuwa wa kutukanwa tu kwao wote waliokaa na kutuzunguka.

17Sasa Mungu wetu, yasikie maombo ya mtumwa wako na malalamiko yake! Uangaze uso wako juu ya Patakatifu pako palipobomolewa, kwa kuwa ndiwe Bwana!

18Mungu wangu, litege sikio lako, usikie! Yafumbue macho yako, uyaone mabomoko yetu, nao mji huo ulioitwa kwa Jina lako! Kwani tukiyatoa haya malalamiko yetu usoni pako, si kwa wongofu wetu sisi, ila kwa huruma zako nyingi.*[#Sh. 115:1.]

19Sikia, e Bwana! Tuondolee makosa, e Bwana! Sikiliza, e Bwana! Yafanye pasipo kukawia kwa ajili yako, Mungu wangu! Kwani mji wako nao ukoo wako umeitwa kwa Jina lako![#Yer. 14:9.]

Ufunuo wa maana ya majuma sabini.

20Nilipokuwa ninasema bado nikiomba na kuyaungama makosa yangu na makosa yao walio ukoo wangu wa Isiraeli na kuyatoa malalamiko yangu usoni pa Bwana Mungu wangu kwa ajili ya mlima mtakatifu wa Mungu wangu,

21nilipokuwa ninasema bado na kuyaomba hayo, mara yule mtume Gaburieli, niliyemwona katika ndoto ya kwanza, akaja akiruka upesi, akanigusa saa ile, walipotolea tambiko la jioni.[#Dan. 8:16.]

22Akanifundisha akisema na mimi kwamba: Danieli, sasa nimetokea kukupatia akili zenye utambuzi.

23Ulipoanza kulalamika, ndipo, palipotolewa neno, nami nimekuja, niliseme kwako, kwani ndiwe mtu wa kupendezwa naye; sasa liangalie hilo neno, upate kulitlambua nalo lile ono!

24Majuma 70 ndiyo, waliyokatiwa walio ukoo wako na wa mji wako mtakatifu ya kuyalipa mapotovu na kuyakomesha makosa na kuzifunika manza, walizozikora, na kuleta wongofu wa kale na kale na kuyatia muhuri maono ya wafumbuaji na kupaeua Patakatifu Penyewe.

25Ujue na kuvitambua vema: Tangu hapo lilipotoka lile neno la kuujenga Yerusalemu tena, mpaka kutokea kwake mkuu aliyepakwa mafuta ni majuma 7, tena majuma 62 utajengwa tena viwanja na boma, lakini siku zile zitakuwa za kusongwa.

26Hayo majuma 62 yatakapokwisha, ndipo, yeye aliyepakwa mafuta atakapoangamizwa, naye atakuwa hanalo kosa lo lote. Kisha watu wa mkuu atakayekuja wataubomoa huo mji napo Patakatifu, nao mwisho wake utakuwa wa kufurikiwa na maji, tena mpaka mwisho yatakuwa mapigano na maangamizo, waliyotakiwa kale.[#Luk. 21:24.]

27Naye atafanyia wengi agano lenye nguvu la juma 1, kisha hilo juma litakapofika kati, atawakomesha watu, wasitoe wala ng'ombe wala vilaji vya tambiko, napo pembeni pa kutambikia atasimama mwangamizaji atapishaye, mpaka yatimie na kumfurikia yeye mwangamizaji, aliyotakiwa kale.[#Dan. 12:11; Mat. 24:15.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania