5 Mose 28

Mbaraka itakayowapata Waisiraeli.

(Taz. 3 Mose 26.)

1Utakapoisikia sauti ya Bwana Mungu wako, uyaangalie na kuyafanya maagizo yake yote, mimi ninayokuagiza leo, Bwana Mungu wako atakufanya kuwa mkuu kuliko mataifa yote ya huku nchini.[#5 Mose 26:19.]

2Ndipo, zitakapokujia hizi mbaraka zote na kukupata, utakapoisikia sauti ya Bwana Mungu wako.

3Utakuwa umebarikiwa mjini, nako shambani utakuwa umebarikiwa.

4Yatakuwa yamebarikiwa mazao ya tumbo lako na mazao ya nchi yako na mazao ya nyama wako wa kufuga na ndama wako na wana kondoo wako.

5Litakuwa limebarikiwa nalo kapu lako na bakuli lako la kutengenezea mikate.

6Utakuwa umebarikiwa wewe utakapoingia, tena utakuwa umebarikiwa wewe utakapotoka.[#Sh. 121:8.]

7Adui zako watakapokuinukia, Bwana atawatoa, wapigwe mbele yako: kwa njia moja watatoka kukuendea, lakini kwa njia saba watakukimbia.

8Bwana atakuagizia mbaraka, uipate chanjani mwako na katika kazi zote za mikono yako, maana atakubariki katika hiyo nchi, Bwana Mungu wako atakayokupa.[#3 Mose 25:21.]

9Bwana atakuweka kuwa ukoo wake mtakatifu, kama alivyokuapia, utakapoyaangalia maagizo yake Bwana Mungu wako na kuzishika njia zake.[#2 Mose 19:5-6.]

10Ndipo, makabila yote ya huku nchini yatakapoona, ya kuwa umeitwa kwa Jina la Bwana, kisha watakuogopa.

11Naye Bwana atakufurikishia mema: mazao ya tumbo lako na mazao ya nyama wako wa kufuga na mazao ya mashamba yako katika hiyo nchi, Bwana aliyowaapia baba zako kukupa wewe.

12Nayo malimbiko yake mema ya mbinguni Bwana atakufunulia, ainyeshee nchi yako mvua, siku zake zitakapotimia, azibariki kazi zote za mikono yako, upate kukopesha mataifa mengi, lakini wewe hutakopa kabisa.[#5 Mose 15:6.]

13Yeye Bwana atakufanya kuwa kichwa, usiwe mkia, upate kuwa juu tu, usilale chini ya wengine, utakapoyasikia maagizo ya Bwana Mungu wako, mimi ninayokuagiza leo kuyaangalia na kuyafanya.

14Haya maneno yote, mimi ninayokuagiza leo, usiyaache na kujiendea wala kuumeni wala kushotoni kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.[#5 Mose 5:32.]

Maapizo yatakayowapata Waisiraeli, wasipotii.

15Lakini usipoisikia sauti ya Bwana Mungu wako, usiyaangalie na kuyafanya maagizo yake yote na maongozi yake yote, mimi ninayokuagiza leo, ndipo, yatakapokujia haya maapizo yote na kukupata.[#Dan. 9:11.]

16Utakuwa umeapizwa mjini, nako shambani utakuwa umeapizwa.

17Litakuwa limeapizwa kapu lako nalo bakuli lako la kutengenezea mikate.

18Yatakuwa yameapizwa mazao ya tumbo lako na mazao ya nchi yako na ndama wako na wana kondoo wako.

19Utakuwa umeapizwa wewe utakapoingia, tena utakuwa umeapizwa wewe utakapotoka.

20Bwana atatuma kwako maapizo na mahangaiko na matisho katika kazi zote, mikono yako itakazozifanya, mpaka uangamizwe kwa kupotea upesi kwa ajili ya ubaya wa matendo yako, kwa kuwa umeniacha.

21Bwana atakugandamanisha na magonjwa ya moyo, mpaka amalize kukuondoa katika hiyo nchi, utakayoiingia kuichukua, iwe yako.

22Bwana atakupiga kwa kifua kikuu na kwa homa na kwa kidingapopo na kwa kipindu na kwa upanga na kwa jua kali na kwa kunyausha ngano; haya yatakuhangaisha wewe, hata uangamie.[#1 Fal. 17:7.]

23Nayo mbingu iliyoko juu yako itakuwa kama shaba, nayo nchi iliyoko chini yako itakuwa kama chuma.[#5 Mose 11:17.]

24Mvua ya nchi yako Bwana ataigeuza kuwa vumbi na mchanga mwembamba, ikuguie toka mbinguni, hata uangamizwe.

25Bwana atakutoa, upigwe mbele ya adui zako: utatoka kwa njia moja kuwaendea, lakini utawakimbia kwa njia saba, kisha utatupwa huko na huko katika nchi zote zenye wafalme.

26Mzoga wako utaliwa na ndege wote wa angani na nyama wa huku nchini, nao hawataona atakayewaamia.

27Bwana atakupiga kwa matende ya Misri na kwa majipu mabaya na kwa buba na kwa upele usiowezekana kuponywa.[#2 Mose 9:9.]

28Bwana atakupiga kwa kichaa na kwa upofu na kwa bumbuazi la moyo.

29Nawe utakuwa ukipapasapapasa na mchana, kama kipofu anavyopapasa gizani, lakini hutafanikiwa katika njia zako, utakaa siku zote ukikorofishwa na kunyang'anywa pasipo kuona mwokozi.

30Utakapoposa mke, mwingine atalala naye; utakapojenga nyumba hutakaa humo; utakapopanda mizabibu hutayala matunda yao.[#Yes. 65:22; 5 Mose 20:6.]

31Ng'ombe wako atakapochinjwa machoni pako, hutaila nyama yake; punda wako atakapopokonywa machoni pako hatarudi kwako; adui zako watakapopewa mbuzi na kondoo wako, hutaona mwokozi.

32Watu wa kabila jingine watakapopewa wanao wa kiume na wa kike, macho yako yataviona na kuzimia kwa kuwatunukia mchana kutwa, lakini hakuna, mkono wako utakachoweza kukifanya.

33Mazao ya nchi yako nayo yote, uliyoyasumbukia, yataliwa na watu wageni, usiowajua, nawe utakaa tu kwa kukorofishwa na kupondwa siku zote.[#Amu. 6:3.]

34Nawe utakuwa mwenye wazimu kwa kuyaona hayo kwa roho yako, utakayoyaona.

35Bwana atakupiga kwa matende magotini na mapajani yasiyowezekana kuponywa, yakutokee toka wayo wa mguu wako mpaka utosini.

36Bwana atakupeleka wewe pamoja na mfalme wako, utakayejiwekea, kwa taifa, usilolijua wala wewe wala baba zako; huko utatumikia miungu mingine iliyo miti na mawe tu.[#5 Mose 4:28.]

37Ndipo, utakapozomewa kwa mafumbo na kwa masimango katika makabila yote, ambayo Bwana atakakupeleka kwao.[#1 Fal. 9:7.]

38Mbegu nyingi utatoa nyumbani kupanda shambani, lakini utavuna machache tu, kwani nzige watazila.[#Yer. 12:13; Mika 6:15.]

39Utapanda mizabibu na kuilimia vema, lakini hutakunywa mvinyo, wala hutaichuma, kwani vimatu wataila.

40Utakuwa na michekele katika mipaka yako yote, lakini hutajipaka mafuta, kwani michekele yako itapukutisha mapooza tu.

41Utazaa wana wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa wako, kwa kuwa watatekwa.

42Miti yako yote nayo mazao ya nchi yako yatakuwa yao mabumundu.

43Mgeni atakayekuwa katikati yako atapaa juu zaidi, hata awe mkuu wako, lakini wewe utashuka kuwa chini zaidi.

44Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha; yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.[#5 Mose 28:12-13.]

45Haya maapizo yote yatakujia, yakuhangaishe; lakini yatakupata, hata uangamizwe, kwa kuwa hukuisikia sauti ya Bwana Mungu wako na kuyaangalia maagizo yake na maongozi yake, aliyokuagiza.

46Kwa hiyo haya maapizo yatakuwa kielekezo na kioja kwako wewe nako kwao walio wa uzao wako kale na kale.

Maapizo mengine yatakayowapata Waisiraeli.

47Kwa kuwa hukumtumikia Bwana Mungu wako kwa furaha na kwa moyo wa kumshukuru kwa hivyo, alivyokufurikishia vyote,

48kwa sababu hii utawatumikia adui zako, Bwana atakaowatuma kwako, nawe utakuwa mwenye njaa na kiu, mwenye uchi na ukosefu wote, kisha atakutia kongwa la chuma shingoni pako, hata akuangamize.

49Bwana atakuletea taifa, atakalolitoa mbali kwenye mapeo ya nchi, warukao kama tai, usiowasikia msemo wao.[#Yer. 5:15; Yes. 33:19.]

50Ndio watu wenye ukali usoni, hawautazami uso wa mzee, wala hawamhurumii kijana.[#Dan. 8:23; Omb. 5:12.]

51Wao ndio watakaoyala mazao ya nyama wako wa kufuga nayo mazao ya mashamba yako, hata uangamizwe; maana hawatakusazia wala ngano wala mvinyo mbichi wala mafuta wala ndama wako wala wana kondoo wako, hata wakuangamize kabisa.

52Nao watakusonga malangoni pako pote, hata ziangushwe hizo kuta ndefu zenye nguvu za maboma yako, unazozijetea katika nchi yako yote; ndipo, utakaposongeka malangoni pako pote katika nchi yako yote, Bwana Mungu wako atakayokupa.

53Nawe kwa kusongeka na kwa kuhangaika utayala mazao ya tumbo lako, maana nyama zao wanao wa kiume na wa kike, Bwana Mungu wako atakaokupa; itakuwa hapo, adui zako watakapokuhangaisha.[#2 Fal. 6:28-29; Omb. 2:20; 4:10.]

54Ndipo, nayo macho yake mtu mwanana wa kwenu aliyejizoeza kula vya urembo tu yatakapokuwa mabaya, atakapowaona ndugu zake na mkewe wa kifuani pake na wanawe waliosalia, aliowasaza bado;

55kwani ataona choyo cha kuwagawia mmoja wao tu nyama za wanawe, anazozila, kwani atakuwa hanacho cho chote, alichojisazia kwa kusongeka na kwa kuhangaika, adui zako watakapokuhangaisha malangoni pako pote.

56Naye mwanamke mwanana wa kwenu aliyejizoeza kula vya urembo tu, asiyejaribu kale kuikanyaga nchi kwa wayo wa mguu wake, kwani alijizoeza kutumia vitu vya urembo tu kwa kuwa mwanana, basi, ndipo, macho yake nayo yatakapokuwa mabaya, atakapomwona mumewe wa kifuani pake na mwanawe wa kiume naye wa kike;

57maana atataka kuwanyima hata kondo ya nyuma iliyotoka katikati ya miguu yake na nyama za wanawe, aliowazaa, kwani anataka kuzila fichoni kwa kukosa chakula chote; haya atayafanya kwa kusongeka na kwa kuhangaika, adui zako watakapokuhangaisha malangoni pako.

58Usipoyaangalia na kuyafanya maneno yote ya Maonyo haya yaliyoandikwa humu kitabuni, upate kuliogopa hilo Jina tukufu litishalo la Bwana Mungu wako,

59Bwana atakupiga wewe nao wa uzao wako hayo mapigo ya kustaajabisha, nayo yatakuwa mapigo makubwa yatakayokaa sana, tena magonjwa mabaya yatakayokaa sana nayo.

60Atakurudishia maradhi yote ya Misri, uliyoyastuka, nayo yatagandamana na wewe.[#5 Mose 28:27.]

61Nayo magonjwa yote na mapigo yote yasiyoandikwa katika kitabu cha Maonyo haya Bwana atakupatia, hata uangamizwe.

62Mtasazwa waume wachache tu, ninyi mliokuwa wengi kama nyota za mbinguni, kwa kuwa hukuisikia sauti ya Bwana Mungu wako.[#5 Mose 1:10.]

63Kama Bwana alivyofurahia kuwafanyizia mema na kuwafanya kuwa wengi, ndivyo, Bwana atakavyofurahia kuwapoteza ninyi na kuwaangamiza, mng'olewe katika hiyo nchi, wewe unakokwenda sasa kuichukua, iwe yako.[#Fano. 1:26.]

64Kisha Bwana atakutawanya katika makabila yote toka mapeo ya nchi ya huku kuyafikia mapeo ya nchi ya huko, nako ndiko, utakakotumikia miungu mingine, usiyoijua wewe wala baba zako, iliyo miti na mawe tu.

65Lakini hutapata kutulia kwao wamizimu hao, wala wayo wa mguu wako hautaona kituo, kwani Bwana atakupa moyo utakaotapatapa tu, nayo macho yatakayopenda kuzimia tu, nayo roho itakayotunukia kukatika tu.

66Kwani uzima wako utakuwa, kama umening'inishwa kwa uzi mbele yako, kwa hiyo utakaa kiwogawoga usiku na mchana, kwa kuwa hutayategemea, ya kama utakaa uzimani.

67Asubuhi utasema: Laiti iwe jioni! napo jioni utasema: Laiti iwe asubuhi! Kwani moyo wako utakaa kiwogawoga kwa ajili ya hayo, utakayoyaogopa, na kuyaona yale mambo, macho yako yatakayoyaona.

68Kisha Bwana atakurudisha Misri kwa merikebu, uishike ile njia, niliyokuambia: Hutaiona tena. Huko mtauzwa kwa adui zenu kuwa watumwa na vijakazi, lakini hatakuwako atakayewanunua.[#5 Mose 17:16; Hos. 8:13.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania