The chat will start when you send the first message.
1Kisha tukageuka, tukapanda na kushika njia ya Basani. Naye Ogi, mfalme wa Basani, akatoka, atujie yeye pamoja na watu wake wote, wapigane nasi kule Edirei.[#4 Mose 21:33-35.]
2Lakini Bwana akaniambia: Usimwogope! Kwani nimemtia mikononi mwako pamoja na watu wake wote na nchi yake. Nawe umfanyizie, kama ulivyomfanyizia Sihoni, mfalme wa Waamori, aliyekaa Hesiboni.
3Kisha Bwana Mungu wetu akamtia mikononi mwetu huyo Ogi, mfalme wa Basani, pamoja na watu wake wote, tukampiga, hatukusaza kwake hata mmoja aliyeweza kukimbia.
4Tukaiteka miji yake yote siku hizo, haukuwako mji kwao, tusiouchukua: miji 60 nacho hicho kipande kizima cha Argobu, ndio ufalme wote wa Ogiwa Basani.
5Miji hiyo yote ilikuwa yenye maboma magumu na marefu na malango na makomeo; tena tukapata miji mingi sana iliyokuwa wazi.
6Tukawatia mwiko wa kuwapo, kama tulivyomfanyizia Sihoni, mfalme wa Hesiboni, tulipowatia mwiko wa kuwapo wote pia waliokuwamo mijini, wanawaume na wanawake na watoto.
7Lakini nyama wa kufuga wote na nyara za miji tukajichukulia.[#5 Mose 20:14.]
8Ndivyo, tulivyozichukua siku hizo nchi za wafalme wawili wa Waamori waliokaa ng'ambo ya huku ya Yordani toka kijito cha Arnoni mpaka milimani kwa Hermoni.
9Wasidoni waliita milima ya Hermoni Sirioni, nao Waamori waliiita Seniri.[#5 Mose 4:48; 1 Mambo 5:23; Sh. 29:6.]
10Nasi tukaichukua miji yote ya nchi ya tambarare na nchi yote ya Gileadi na ya Basani mpaka Salka na Edirei, iliyokuwa miji ya ufalme wa Ogi kule Basani.
11Yeye ogi, mfalme wa Basani, alikuwa amesalia peke yake kwa masao ya Majitu; mkikitazama kitanda chake, ni kitanda cha chuma, nacho kingaliko katika mji wa Raba wa wana wa Amoni, urefu wake ni mikono tisa, nao upana wake ni mikoni minne, mkipima kwa mikono wa mtu.
12Siku hizo tukaichukua nchi hiyo, iwe yetu toka Aroeri ulioko kwenye kijito cha Arnoni. Nusu ya milima ya Gileadi pamoja na miji yake ikawapa Warubeni na Wagadi.[#4 Mose 32:33-42.]
13Kipande cha Gileadi kilichosalia na Basani yote iliyokuwa ufalme wa Ogi nikawapa wao wa nusu ya shina la Manase, ni kipande chote cha Argobu pamoja na Basani yote inayoitwa nchi ya Majitu.
14Yairi, mwana wa Manase, alikichukua kile kipande chote cha Argobu hata mpakani kwa Wagesuri na Wamakati, akaziita hizo nchi za Basani kwa jina lake Mahema ya Yairi; ndivyo, zinavyoitwa hata leo.
15Makiri nikampa Gileadi.
16Warubeni na Wagadi nikawapa kipande cha Gileadi mpaka kijito cha Arnoni, mpaka uwe mtoni katikati; tena mpaka ukafika kijito cha Yakobo ulio mpaka wa wana wa Amoni.
17Tena nyika inayopakana na Yordani toka Kinereti hata kwenye bahari ya nyikani, ndio Bahari ya Chumvi chini ya matelemko ya Pisiga upande wa maawioni kwa jua.
18Siku hizo nikawagiza ninyi kwamba: Bwana Mungu wenu amewapa nchi hii, mwichukue, iwe yenu; kwa hiyo wa kwenu wote walio wenye nguvu na washike mata ya vita, mvuke mbele ya ndugu zenu hao wana wa Isiraeli.
19Wanawake na watoto wenu na makundi yenu tu na wakae katika miji yenu, kwani najua, ya kuwa mnayo makundi mengi.
20Hapo, Bwana atakapowapatia ndugu zenu kutulia kama ninyi, nao watakapokwisha kuichukua nchi, Bwana Mungu wenu atakayowapa ng'ambo ya huko ya Yordani, ndipo, mtakaporudi kila mtu kwenye nchi yake, aliyoichukua, iwe yake, niliyowapa ninyi.
21Naye Yosua nikamwagiza siku hizo kwamba: Macho yako yameyaona yote, Bwama Mungu wetu aliyowafanyizia hao wafalme wawili; hivyo ndivyo, Bwana atakavyozifanyizia nchi zote za kifalme, utakazoziingia wewe.[#4 Mose 27:18,22.]
22Msiwaogope! Kwani Bwana Mungu wenu ndiye atakayewapigia vita.[#5 Mose 1:30.]
23Siku hizo nikambembeleza Bwana kwamba:
24Bwana Mungu wangu, wewe umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukuu wako na nguvu za mkono wako; kwani yuko Mungu gani mbinguni na duniani anayeweza kufanya matendo, kama hayo ya uwezo wako mwingi?
25Nipe ruhusa, nivuke, niione nchi hiyo njema iliyoko ng'ambo ya Yordani, hiyo milima mizuri, nayo ya Libanoni.
26Lakini Bwana alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, kwa hiyo Bwana hakunisika, akaniambia: Acha tu! Usiseme tena na mimi kwa ajili ya shauri hili![#4 Mose 20:12.]
27Panda juu mlimani kwa Pisiga, uyainue macho yako na kuyaelekeza upande wa baharini na wa kaskazini na wa kusini na wa maawioni kwa jua, uitazame hiyo nchi kwa macho yako. Kwani hutauvuka mto huu wa Yordani.
28Mwagizie Yosua mambo yako! Mtie nguvu na kumshikiza moyo! Kwani yeye ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, naye ndiye atakayewagawia nchi hiyo, utakayoiona, iwe yao.[#5 Mose 31:3,7.]
29Kisha tukakaa bondeni na kuelekea Beti-Peori.