The chat will start when you send the first message.
1*Ninyi watoto, watiini wazazi wenu, kwa kuwa mnaye Bwana! Kwani hivi huongoka:[#Kol. 3:20.]
2Mheshimu baba yako na mama yako!
Nalo ni agizo la kwanza lenye kiagio cha kwamba:
3Upate kukaa vema,
nazo siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi!
4Nanyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu! Ila mwakuze na kuwaonya, wamche Bwana![#5 Mose 6:7,20-25; Sh. 78:4; Fano. 19:18; Kol. 3:21.]
5Ninyi watumwa, kama mnavyomtii Kristo, watiini nao mabwana zenu wa nchini kwa kuwaogopa na kutetemeka, mkilishika mioyoni mwenu lile Neno moja tu![#Kol. 3:22-25; 1 Tim. 6:1-2; Tit. 2:9-10; 1 Petr. 2:18.]
6Msifanye kazi nzuri machoni pao tu kama watakao kuwapendeza watu, ila kama watumwa wake Kristo myafanye kwa mioyo, Mungu ayatakayo!
7Tumikeni na kuuitikia utumishi, kama sio watu, mnaowatumikia, ila kama ni Bwana, mmtumikiaye!
8Tena mjue: kila mtu akifanya kazi njema yo yote atalipwa naye Bwana, akiwa mtumwa, au akiwa mwungwana.[#2 Kor. 5:10.]
9Nanyi mabwana, mwafanyie yaleyale! Mwache kuwatisha mkijua: mbinguni yuko aliye Bwana wao na wenu, tena kwake hakuna upendeleo!*[#2 Mambo 19:7; Tume. 10:34; Kol. 4:1.]
10*Mwisho, ndugu zangu, kwa sababu m wake Kristo, mwe wenye kushupaa kwa nguvu ya uwezo wake![#Ef. 3:16; 1 Kor. 16:13; 1 Yoh. 2:14.]
11Yashikeni mata yote ya Kimungu, mweze kusimama na kuyakinga madanganyo yake msengenyaji![#2 Kor. 10:4.]
12Kwani vita vyetu, tuvipiganavyo, sivyo vya wenye damu na miili, ila ni vya kupigana nao wafalme na wenye uwezo na wenye kutawala nchini penye giza, nao wale pepo wabaya waliopo angani.[#Ef. 2:2; Luk. 22:31; Yoh. 14:30.]
13Kwa hiyo yashikeni mata ya Kimungu yote, mweze kusimama penye mapigano, siku mbaya itakapokuwapo, mpate kuyashinda mabaya yote mkiwa mmesimama vivyo hivyo!
14Simameni mkiwa mmejifunga ukweli viunoni! Vifuani vaeni wongofu, uwe kanzu yenu ya chuma![#Yes. 59:17; Luk. 12:35; 1 Tes. 5:8; 1 Petr. 1:13.]
15Miguuni vaeni viatu! Hivyo mtakuwa tayari kuutangaza utume mwema wa utengemano.
16Kuliko hayo yote kazeni kumtegemea Mungu, kuwe ngao yenu ya kuizima mishale yote yenye moto ya yule Mbaya![#1 Petr. 5:9; 1 Yoh. 5:4.]
17Kichwani vaeni wokovu, uwe kofia yenu ngumu! Kisha shikeni nao upanga wa Kiroho, ndio neno la Mungu!*[#1 Tes. 5:8.]
18Tena kwa ajili ya mambo yote mwombe na kubembeleza siku zote kwa nguvu ya Roho! Tena kesheni, myaweze hayo, mkijipingia kuwaombea watakatifu wote![#Mat. 26:41.]
19Niombeeni nami, nipate kufumbuliwa kinywa changu, niseme na kulitambulisha waziwazi fumbo la Utume mwema, ambao ninautumikia[#Tume. 4:29; Kol. 4:3; 2 Tes. 3:1.]
20namo humu kifungoni, nipate kuutangaza pasipo woga, kama inavyonipasa![#2 Kor. 5:20.]
21Lakini kusudi mpate kujua nanyi, mambo yangu yalivyo, nami mwenyewe nilivyo, yote atawasimulia Tikiko aliye ndugu yetu mpendwa na mtumishi mwelekevu wa Bwana.[#Tume. 20:4; 2 Tim. 4:12.]
22Huyu nimemtuma, aje kwenu kwa ajili hiihii, myatambue, mambo yetu yalivyo, naye aitulize mioyo yenu.[#Kol. 4:7-8.]
23Ndugu, mtengemane na kupendana, mpate hata nguvu ya kumtegemea Mungu itokayo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo!
24Upole uwakalie wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo pasipo kulegea! Amin.