The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose: Jichongee mbao mbili za mawe, kama zile za kwanza zilivyokuwa! Nami nitaziandika hizo mbao maneno yale yaliyokuwa katika zile mbao za kwanza, ulizozivunja.[#2 Mose 32:19.]
2Uwe tayari asubuhi, upate kupanda asubuhi mlimani kwa Sinai, usimame kwangu mlimani kwa Sinai.
3Asipande mtu pamoja na wewe, wala asionekane mtu mlimani po pote, wala kondoo wala mbuzi wala ng'ombe wasilishe penye mlima huu!
4Ndipo, alipochonga mbao mbili za mawe, kama zile za kwanza zilivyokuwa, Kisha Mose akajidamka asubuhi, akapanda mlimani kwa Sinai, kama Bwana alivyomwagiza, akizishika hizo mbao mbili mkononi mwake.
5Ndipo, Bwana aliposhuka winguni, akaja kusimama naye huko, akalitamka Jina la Bwana kwa sauti kuu,[#2 Mose 33:19.]
6kisha Bwana akapita machoni pake na kutangaza: Bwana, Bwana ni Mungu mwenye huruma na utu, tena ni mwenye uvumilivu na upole na welekevu mwingi.[#4 Mose 14:18; Sh. 103:8; 1 Yoh. 4:16.]
7Huwekea watu maelfu na maelfu magawio, huondoa manza na mapotovu na makosa, mbele yake hakuna asiye mkosaji; nazo manza, baba walizozikora, huzilipisha watoto na watoto wa watoto, akifikishe kizazi cha tatu na cha nne.
8Ndipo, Mose alipoinama chini upesi na kujiangusha usoni,
9akasema: Bwana wangu, kama nimeona upendeleo machoni pako, Bwana wangu na aende katikati yetu! Kwani watu hawa ni wenye kosi ngumu. Nawe tuondolee manza zetu na makosa yetu na kutupokea kuwa wako!
10Bwana akasema: Tazama, na nifanye agano mbele yao wote walio ukoo wako, nifanye vioja visivyofanyika katika nchi zote na kwa mataifa yote. Ndipo, watu wote, ambao uko katikati yao, watakapoyaona matendo ya Bwana, kwani hayo, nitakayoyafanya kwako, yatatisha.
11Yaangalie tu, ninayokuagiza leo! Utaniona, nikiwafukuza mbele yako Waamori na Wakanaani na Wahiti na Waperizi na Wahiwi na Wayebusi.
12Jiangalie, usifanye agano na wenyeji wa nchi ile, utakayoiingia, wasiwe katikati yenu kama matanzi![#2 Mose 23:32-33.]
13Pao pa kutambikia sharti upabomoe, nazo nguzo zao za kutambikia sharti uzivunje, nayo miti yao ya Ashera sharti uikate![#2 Mose 23:24.]
14Usiangukie mungu mwingine! Kwani Bwana huitwa mwenye wivu, naye ni Mungu mwenye wivu kweli.[#2 Mose 20:3,5.]
15Kwa hiyo usifanye agano na wenyeji wa nchi hiyo! Wao wakiifuata miungu yao pamoja na kufanya ugoni, tena wakiichinjia miungu yao ng'ombe za tambiko, wasikualike kula nyama za ng'ombe za tambiko.
16Wala usiwachukulie wanao wa kiume wake kwa wana wao wa kike, nao wangewafanyisha wanao ugoni wa kuifuata miungu yao, wao wakiifuata miungu yao kufanya ugoni.[#5 Mose 7:3; Amu. 3:6; 1 Fal. 11:2.]
(18-26: 2 Mose 23:14-19.)17Usijifanyizie miungu kwa kuyeyusha yo yote.[#2 Mose 20:23.]
18Sikukuu ya Mikate isiyochachwa uiangalie: siku saba ule mikate isiyochachwa, kama nilivyokuagiza; nazo siku zake zilizowekwa ni za mwezi wa Abibu, kwani katika mwezi wa Abibu ulitoka Misri.
19Kila aliye mwana wa kwanza wa mama yake awe wangu, hata kwa nyama wako wa kufuga kila mwana wa kiume wa kwanza ni wangu, kama ni ng'ombe au kondoo.
20Mwana wa kwanza wa punda utamkomboa kwa mwana kondoo; usipomkomboa, umvunje shingo! Wana wa kwanza wote watakaozaliwa na wanao sharti uwakomboe. Watu wasinitokee mikono mitupu![#2 Mose 13:12-16.]
21Siku sita sharti ufanye kazi, lakini siku ya saba sharti upumzike, ijapo siku ziwe za kulima au za kuvuna, sharti upumzike.
22Nayo sikukuu ya Majuma saba (Pentekote) ishike kwako kuwa sikukuu ya Malimbuko ya ngano, nayo sikukuu ya kukusanya mapato ya mashambani mwisho wa mwaka uishike!
23Kila mwaka mara tatu waume wako wote sharti watokee mbele ya Bwana Mungu aliye Mungu wa Isiraeli.
24Kwani nitawafukuza wamizimu mbele yako, niipanue mipaka yako; hatakuwako mtu atakayeitamani nchi yako, utakapopanda kutokea mbele ya Bwana Mungu wako mara tatu kila mwaka.
25Usichinje, ng'ombe yangu ya tambiko, damu yake ikimiminikia panapo chachu yo yote, wala nyama za ng'ombe ya tambiko ya sikukuu ya Pasaka zisilale mpaka kesho.
26Malimbuko ya kwanza ya mashamba yako sharti uyapeleke Nyumbani mwa Bwana Mungu wako. Kitoto cha mbuzi usikipike katika maziwa ya mama yake.[#2 Mose 23:19.]
27Bwana akamwambia Mose: Yaandike maneno haya yote! Kwani kwa maneno haya nimefanya agano na wewe nao wana wa Isiraeli.[#2 Mose 24:4.]
28Akawa huko pamoja na Bwana siku 40 mchana na usiku, hakula chakula, wala hakunywa maji, akaandika katika zile mbao mbili maneno ya Agano hili, ndiyo yale maagizo kumi.[#2 Mose 24:18; 31:18; 34:1; Mat. 4:2.]
29Ikawa, Mose aliposhuka mlimani kwa Sinai alizishika hizo mbao mbili za Ushahidi mkononi mwake na kushuka mlimani kwa Sinai; hapo yeye Mose alikuwa hajui, ya kama ngozi ya uso wake inaangaza kwa kusema na Bwana.
30Haroni na wana wa Isiraeli walipomwona Mose, mara wakaona, ya kama ngozi ya uso wake inaangaza; ndipo, walipoogopa kumkaribia.[#2 Kor. 3:7-18.]
31Mose alipowaita, wakarudi kwake, Haroni nao watu wote walio wakuu penye mkutano wakarudi kwake, naye Mose akasema nao.
32Baadaye wana wote wa Isiraeli wakamkaribia, akawaagiza yote, Bwana aliyomwambia mlimani kwa Sinai.
33Mose alipokwisha kusema nao akaufunika uso wake kwa mharuma.
34Lakini Mose alipomtokea Bwana kusema naye akauondoa huo mharuma, mpaka atoke kwake. Naye alipotoka kwake, aseme na wana wa Isiraeli na kuwaambia aliyoagizwa,[#2 Mose 33:8-9.]
35wana wa Isiraeli wakauona uso wake, ya kuwa uso wa Mose unaangaza; ndipo, Mose alipourudisha mharuma usoni pake, mpaka aingie tena kusema na Bwana.