Habakuki 1

Ukosaji wa Yuda.

Hili ndilo neno zito, aliloliona mfumbuaji Habakuki.

1Bwana, hata lini nikulilie, unisaidie? Nawe husikii!

2Hata lini nikulalamikie kwa kukorofishwa? Nawe huniokoi!

3Mbona umeniacha, nione maovu,

ukatazama tu, ninavyosumbuliwa?

Uangamizo na ukorofi uko mbele yangu,

yako magombano, hata mashindano hutokea.

4Kwa hiyo Maonyo yanakosa nguvu,

mashauri yapasayo hayatokei kale na kale,

kwani asiyemcha Mungu humnasa aliye mwongofu,

kwa hiyo yanyokayo yakitokea yamekwisha kupotolewa.

Mabaya, Wakasidi watakayoyafanya.

5Yatazameni mambo yaliyoko kwa wamizimu, myaangalie!

Ndipo, mtakapozizimka kwa kustuka.

Kwani mimi hizi siku zenu nitatenda tendo,

kama lingesimuliwa, msingeliitikia.

6Kwani mtaniona, nikiwainua Wakasidi,

lile taifa kali lenye mioyo miepesi,

ni wale wanaokwenda katika nchi za mbali,

wajipatie makao yasiyo yao.

7Ndio watu watishao kwa kutia woga,

kwao hao hutoka amri zilizo za majivuno tu.

8Farasi wao hupiga mbio kushinda machui,

ni wepesi sana kuliko mbwa wa mwitu wawindao jioni.

Wapanda farasi wa kwao hujitata;

tena hao wapanda farasi wakija kutoka mbali

huruka kama tai wakimbiliao kula.

9Wao wote hujia kukorofisha,

nyuso zao zote pia zikiwa zimeelekea mbele,

hukusanya mateka kama ni mchanga.

10Hao ndio watakaowafyoza wafalme,

hata wakuu watawacheka;

hao ndio watakaoteka kila boma,

maana hulikusanyia mchanga kuwa boma, kisha huliteka.

11Baadaye hujiendea kama upepo,

huenda zao na kuzidi kukosa,

nguvu zao huziwazia kuwa mungu wao.

Ombo na ombolezo la mfumbuaji.

12Kumbe wewe Bwana, siwe Mungu wangu mtakatifu toka kale?

Kwa hiyo hatutakufa.

Wewe Bwana, umemweka, atupatilize;

wewe Mwamba wetu, umemtia nguvu, atuchapue.

13Macho yako yanatakata, hayawezi kuyaona tu hayo mabaya,

huwezi kabisa kuvitazama tu, watu wanavyosumbuliwa.

Mbona sasa unawatazama tu wapokonyaji na kujinyamazia kimya,

asiyekucha akimmeza aliye mwongofu kuliko yeye?

14Unataka, watu wawe kama samaki wa baharini

au kama wadudu wakosao awatawalaye?

15Yeye amewapandisha hawa wote kwa ndoana,

akawakamata namo katika nyavu zake,

akawakusanya katika majarifa yake,

kwa hiyo akafurahi na kupiga vigelegele.

16Kwa sababu hii huzitambikia nyavu zake,

huyavukizia nayo majuya yake,

kwani kwa msaada wao mafungu yake ni yenye manono,

navyo vyakula vyake ni vyenye mafuta.

17Je? Kwa hiyo utamwacha, awatoe vivyo hivyo,

wavu wake uliowakamata,

akiendelea kuua mataifa mazima pasipo kuwahurumia?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania