The chat will start when you send the first message.
1Yatawapata wenye hukumu wanaopotoa hukumu,
nao waandishi wanaoandika makorofi!
2Hutaka kuwazuia wanyonge, wasije shaurini,
huyapokonya yawapasayo wakiwa wao walio ukoo wangu;
tena hutaka, wajane wawe mateka yao,
nao wafiwao na wazazi huwanyang'anya mali zao.
3Siku ya kukaguliwa itakapofika, mtafanya nini,
upepo wa kimbunga utokao mbali utakapovuma?
Mtamkimbilia nani, awasaidie?
Nayo matukufu yenu mtayapeleka wapi, myafiche?
4Nanyi hamtaona mzungu kuliko huu:
kupiga magoti kwenye mateka au kutupwa kwenye mizoga.
Lakini kwa hayo yote makali yake hayajatulia bado,
nao mkono wake ungaliko umekunjuka.
5Yatawapata Waasuri nao,
ijapo makali yangu yawatumie kuwa fimbo,
ijapo machafuko yangu yawe vigongo mikononi mwao.
6Ninawatuma kujia kabila lililojichafua,
ninawaagizia watu, ambao ninawakasirikia,
wateke mateka na kuyapokonya mapokonyo,
wawakanyage kama matope ya njiani.
7Lakini wenyewe hawafikiri kama hivyo,
wala mioyo yao haina mawazo kama hayo,
kwani mioyoni mwao mna neno moja tu: Kuangamiza!
Makabila ya watu, wanayotaka kuyang'oa, si machache.
8Kwani husema: Wakuu wetu wote pamoja sio wafalme?
9Je? Mji wa Kalno haukuangamia kama ule wa Karkemisi?
Mji wa Hamati haukuangamia kama ule wa Arpadi?
Nao mji wa Samaria haukuangamia kama ule wa Damasko?
10Kama mikono yetu ilivyowapata wafalme wa kimizimu na vinyago vyao vilivyokuwa vyenye nguvu kuliko vile vya Yerusalemu na vya Samaria,[#Yes. 36:18-20.]
11je? Yale, tuliyowafanyizia Wasamaria na vinyago vyao,
yaleyale tusiwafanyizie Wayerusalemu na vinyago vyao?
12Lakini hapo, Bwana atakapokuwa ameyamaliza matendo yale mlimani kwa Sioni namo Yerusalemu, ndipo, yatakapokuwa aliyoyasema kwamba: Nitauumbua moyo wa mfalme wa Asuri kwa ajili ya uzao wa ukuu wake na kwa ajili ya utukufu wa macho yake wa kujitukuza.[#Yes. 37:36.]
13Kwani alisema: Nikifanya hayo ni nguvu za mikono yangu,
tena ni werevu wangu wa kweli, kwani mimi ni mwenye akili.
Mimi nimeondoa mipaka ya makabila ya watu,
nikayapokonya malimbiko yao, nikawa ng'ombe mkali,
nikawakumba waliokalia viti vya kifalme.
14Mkono wangu ukaona mali za makabila ya watu,
kama wengine wanavyoona vituo vya ndege.
Kama watu wanavyookota mayai yaliyoachwa,
ndivyo, mimi nilivyookota nchi nzima;
nako hakuwako mwenye kupanua bawa,
wala mwenye kufumbua kinywa wala mwenye kulia.
15Shoka litawezaje kujitukuza mbele yake
aliyelitumia la kukatia?
Au msumeno utawezaje kujikuza mbele yake
aliyeutumia wa kukerezea?
Ingekuwa kama kusema: Fimbo ndiyo inayompigisha aishikaye,
au kama kusema: Kigongo kinamchukua asiye mti.
16Kwa hiyo Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi
atatuma kwao wanene jambo litakalowakondesha,
nako kwenye utukufu wao kutawaka maunguzo,
nayo yataunguza, kama moto unavyounguza.
17Nao mwanga wa Isiraeli utawawia moto;
nao utukufu wao utageuka kuwa kama ndimi za moto;
zitayaunguza maboma yao yenye mibigili na mikunju,
yateketee kwa siku moja tu.
18Hivyo atauangamiza utukufu wa misitu na wa mizabibu yao,
kuanzia shinani mpaka kwenye nyama za ndani,
itazimia, kama mwenye kufa anavyozimia.
19Miti ya misitu yao itakayosalia itahesabika,
mtoto ataweza kuiandika.
20Siku ile waliosaa wa Isiraeli nao waliopona wa mlango wa Yakobo hawatajishikiza tena kwake yeye aliyewapiga, ila watajishikiza kweli kwa Bwana aliye Mtakatifu wa Isiraeli.
21Watakaosalia kuwa sao la Yakobo
ndio watakaomgeukia Mungu mwenye nguvu.
22Ijapo wawe wengi kama mchanga wa ufukoni,
wao walio ukoo wako wa Isiraeli,
watakaomgeukia watakuwa sao tu;
wengine angamizo lao litatimizwa,
liyatokeze maamuzi yake kuwa ya kweli kabisa.
23Kwani atakayelitimiza shauri la angamizo
ni Bwana Mungu Mwenye vikosi,
atavifanyiza katika nchi zote.
24Kwa hiyo Bwana Mungu Mwenye vikosi anasema hivyo: Mlio ukoo wangu ukaao Sioni, msimwogope Mwasuri, ijapo awapige vigongo, awainulie fimbo yake na kuishika njia ya Wamisri.
25Kwani bado kitambo kidogo ndipo, machafuko yatakapokoma, makali yangu yawageukie wao, yawamalize.
26Bwana Mwenye vikosi anawashikia mjeledi, awapige, kama alivyowapiga Wamidiani kwenye Mwamba wa Kunguru, atawainulia nayo fimbo yake, kama alivyoiinulia Wamisri baharini.[#2 Mose 14:26; Amu. 7:25.]
27Siku ile mizigo yao itaondoka mabegani kwenu,
nayo miti yao ya kuwafunga itaondoka shingoni kwenu,
itavunjika tu kwa unene, mtakaoupata tena.
28Watakapokuja watapita Ayati, wavuke Migroni,
wataiacha mizigo yao Mikimasi.
29Kisha watapita katika lango la magenge,
Geba wapige makambi ya kulala usiku,
Warama watatetemeka, wa Gibea wa Sauli watakimbia.
30Pigeni yowe, ninyi wa binti Galimu!
Ninyi wa Laisi, sikilizeni! Nanyi wa Anatoti na mwone ukiwa!
31Wa Madimena watatawanyika, wakaao Gebimu watakimbia.
32Siku ya kusimama kwao kule Nobu
watainyosha mikono yao, wauteke mlima wa binti Sioni
nacho kilima cha Yerusalemu.
33Bwana aliye Bwana Mwenye vikosi atakapotokea,
ayakate matawi yao kwa nguvu zake zitishazo,
ndipo, itakapovunjika nayo miti iliyokwenda juu sana,
hiyo mirefu yenyewe itaanguka.
34Navyo vichaka vya mwituni vitakatwa kwa vyuma vikali,
mwitu wa Libanoni utaishia kwa nguvu za mwenye utukufu.