The chat will start when you send the first message.
1Umekwisha kuapizwa, wewe Simba wa Mungu!
Wewe Simba wa Mungu! Wewe mji, Dawidi alimotua!
Ongezeni mwaka kwa mwaka na kula sikukuu miaka mizima!
2Kisha nitamsonga Simba wa Mungu,
kuweko kipiga kite na kuugua;
ndipo, atakapokuwa mbele yangu Simba wa Mungu wa kweli.
3Ndipo, nitakapokupigia makambi, yakuzinge,
kisha nitakujengea boma la kukusonga,
nitaisimamisha hata minara, nipate kukushinda.
4Hapo ndipo, utakaponyenyekea, useme na kulala chini,
maneno yako, utakayonitolea toka mavumbini,
yatakuwa ya kujipunguza,
sauti yako itakuwa kama ya mzimu atokaye kuzimuni,
maneno yako ya kusema uvumbini
yatakuwa ya kunong'ona tu.
5Lakini mavumo ya wale wageni waliokujia
yatakuwa kama mavumbi membamba,
kweli mavumo ya hao wakorofi
yatakuwa kama makapi yapeperushwayo;
nayo yatakuwa kwa ghafula, wagunduliwe nayo.
6Maana utakaguliwa na Bwana Mwenye vikosi,
atakapokujia na kuitetemesha nchi kwa ngurumo,
kwani ni mwenye sauti kuu,
ataleta nao upepo wa kimbunga ulio wenye nguvu
na ndimi za moto ulao.
7Yatakuwa kama ndoto, mtu aliyoiota usiku,
hayo mavumo ya wamizimu waliokuja
kumshambulia Simba wa Mungu
nao waliolipigia boma lake vita na kumsonga.
8Itakuwa kama mwenye njaa anayeota akila chakula,
lakini anapoamka hakuna kitu kwake,
au kama mwenye kiu anayeota akinywa,
lakini anapoamka hutweta na kuivuta roho yake.
Hivyo ndivyo, yatakavyokuwa mavumo ya wamizimu wote,
waliokuja kuushambulia mlima wa Sioni!
9Tumbueni macho na kuyakodoa! Yatieni giza na kupofuka!
Wamelewa, lakini si kwa mvinyo,
wanapepesuka, lakini si kwa kileo.
10Kwani Bwana amewamwagia ninyi roho ya usingizi mwingi,
akayafumba macho yenu, ninyi wafumbuaji,
akavifunika vichwa vyenu, ninyi wachunguzaji.
11Hayo yote mliyoyaona yakawa kwenu kama maneno ya kitabu
kulichofungwa na kutiwa muhuri;
kama ajuaye kusoma anapewa na kuambiwa: Kisome hiki!
atajibu: Siwezi, kwani kimefungwa na kutiwa muhuri.
12Kama asiyejua kusoma anapewa na kuambiwa: Kisome hiki!
atajibu: Sijui kusoma.
13Bwana akasema:
Ukoo huu hunikaribia na vinywa vyao,
huniheshimu kwa midomo tu,
lakini mioyo yao inanikalia mbali;
kwa sababu hii hunicha bure,
kwani hufundisha mafundisho yaliyo maagizo ya watu tu.
14Kwa hiyo na mwone, ninavyoendelea
kuufanyizia ukoo huu mambo ya mataajabu na ya vioja,
werevu wao walio werevu wa kweli kwao upotee,
nao utambuzi wa watambuzi wao usionekane.
15Yatawapata wao walao njama,
kwamba: wamfiche Bwana mashauri yao!
Nao wafanyao gizani kazi zao na kusema:
Yuko nani anayetuona? Yuko nani anayetujua?
16Mmepotea kabisa!
Uko udongo unaowaziwa kuwa sawa na mfinyanzi?
Au kiko kiumbe kiwezacho kumwambia aliyekiumba:
Hukunifanya?
Au kiko chombo kiwezacho kumwambia aliyekifinyanga:
Hujui kitu?
17Sicho kitambo kidogo bado,
Libanoni kugeuke kuwa shamba,
nayo mashamba yawaziwe kuwa mwitu?
18*Siku ile viziwi watayasikia maneno yaliyoandikwa,
nayo macho ya vipofu yaliyokuwa yenye giza jeusi yataona.
19Nao wanyonge wataendelea kumfurahia Bwana
nao walio wakiwa kuliko watu wengine
watamshangilia Mtakatifu wa Isiraeli.
20Kwani wakorofi watakuwa wamekwisha,
nao wafyozaji watakuwa wameangamia,
nao wote watakuwa wameng'olewa
waliokataa kulala usingizi, wapate kuwapotoa wenzao.
21Ndio wanaokosesha wengine shaurini,
ndio wanaowategea waamuliao penye malango ya mji,
kwani hivyo wanawapotoa waongofu, wasishinde shaurini.*
22Kwa sababu hii Bwana alimkomboa Aburahamu,
akauambia mlango wa Yakobo:
Sasa Yakobo hatapatwa tena na soni,
wala uso wake hautamvilia tena.
23Kwani watoto wake watakapoona,
mikono yangu itakayoyafanya kwao,
watalitakasa Jina langu,
ndiko kumtakasa Mtakatifu wa Yakobo
na kumcha Mungu wa Isiraeli.
24Ndipo, waliopotea rohoni watakapojua utambuzi
nao walionung'unika watajifundisha yafaayo.