The chat will start when you send the first message.
1Ndivyo, asemavyo Bwana:
Yatawapata wale wana wabishi
wapigao shauri lisilo la kwangu,
wafanyao agano pasipo Roho yangu,
kusudi waongeze kosa kwa kosa.
2Ndio wanaokwenda kushuka Misri
pasipo kukiuliza kinywa changu,
wajipatie nguvu kwa nguvu za Farao
kwa kukikimbilia kivuli cha Misri.
3Lakini nguvu zake Farao zitawageukia, ziwatie soni,
nako kukikimbilia kivuli cha Misri kutawapatia matusi.
4Ijapo wakuu wake waje Soani,
ijapo wajumbe wake wafike mpaka Hanesi,
5wao wote wataona soni na watu wasiowafalia kitu,
kwa kuwa hawawezi kuwasaidia
au kuwapatia cho chote kuwafaliacho,
kwani wanawatia soni tu, wengine wawabeze na kuwatukana.
6Wanapita katika nchi yenye masongano na mahangaiko,
kwani wamo simba na chui, pili na nyoka za moto warukao.
Huko wanapitisha mali zao migongoni kwa punda,
nako kwenye nundu za ngamia malimbiko yao,
wayapelekee watu wasiowafalia kitu.
7Nayo Misri msaada wake ni kama mvuke, ni wa bure tu,
kwa sababu hii waliipa jina hili:
Mkuu wa maneno anayejikalia tu.
8Sasa nenda, uyachore katika kibao machoni pao,
kisha uyaandike namo kitabuni,
siku za nyuma yapate kuwashuhudia kale na kale.
9Kwani ndio watu wabishi na wana wenye uwongo,
kweli ndio wana wasiotaka kuyasikia Maonyo ya Bwana.
10Huwaambia waonaji: Msione!
nao watazamaji: Msitutazamie yaliyo ya kweli!
Sharti mtuambie yaliyo mafuta ya midomo,
sharti mtutazamie madanganyifu!
11Ondokeni njiani penye kweli! Ipotoeni mikondo inyokayo!
Tuacheni, tupumzike, tusimwone Mtakatifu wa Isiraeli!
12Kwa hiyo Mtakatifu wa Isiraeli anasema:
Kwa kuwa mmelikataa neno hili,
mkayaegemea mambo yenye ukorofi na upotovu,
mkayatumia ya kujishikizia:
13kwa sababu hii hizo manza, mlizozikora,
zitakuwa kama ufa
unaokwenda ukipanuka katika ukuta mrefu,
nao utabomoka ghafula na kuwagundua watu.
14Naye Bwana atauvunja, kama watu wanavyovunja mtungi
wakiupigapiga pasipo kuuhurumia,
hapo, utakapovunjika, kisipatikane kigae
cha kupalia moto jikoni, wala cha kutekea maji kisimani.
15Kwani hivi ndivyo, anavyosema Bwana Mungu,
aliye Mtakatifu wa Isiraeli:
Mtakaporudi na kutulia, mtaokolewa;
mtakaponyamaza na kujiegemeza,
mtapata nguvu,
lakini mmekataa!
16Mkasema: Hapana! Na tupande farasi, tupige mbio!
Kwa hiyo mtakimbia.
Mkasema: Na tupande farasi wenye mbio sana!
Kwa hiyo watakaowafukuza watawapigisha mbio.
17Elfu wa kwenu wataikimbia yowe ya mmoja;
watano wakipiga yowe, mtakimbia wote,
mpaka masao yenu yawe kama mlingoti ulioko mlimani juu
au kama bendera iliyoko kilimani.
18Kwa hiyo Bwana anangoja, apate kuwatolea upole;
kwa hiyo anainuka, apate kuwahurumia,
kwani Bwana ni Mungu wa kuamua kweli;
wenye shangwe ni wote wanaomngoja,
19kwani walio wa Sioni watakaa Yerusalemu.
Hamtalia machozi kamwe, atawaendea kwa upole;
atakapozisikia sauti za vilio vyenu atawaitikia.
20Kweli, Bwana amewalisha mikate ya masongano,
akawanywesha maji ya mahangaiko,
lakini wafunzi wako hawatajificha tena,
ila macho yako yatakuwa yakiwatazamia wafunzi wako.
21Nayo masikio yako yatasikia neno
litokalo nyuma yako kwamba:
Njia ni hii, ishikeni!
kama mtakuwa mmeiacha kuumeni au kushotoni.
22Hapo ndipo, mtakapovichafua vinyago vyenu vya miti
vilivyofunikwa na fedha navyo vilivyofunikwa na dhahabu,
utavitupatupa, kama ni takataka,
na kuviambia: Tokeni kwetu!
23Naye atakupa mvua za mbegu zako, ulizozipanda shambani,
nalo shamba litakutolea mikate itakayokuwa yenye nguvu ya kunonesha,
nao kondoo wako watalisha siku zile kwenye uwanda mpana.
24Nao ng'ombe na punda wako wanaolima shamba
watakula muhindi ulioungwa na majani yenye chumvi,
nao utakuwa umepepetwa kwa ungo na kipepeto.
25Katika kila mlima mrefu,
hata katika kila kilima kiendacho juu
kutakuwa na vijito vya maji yarukayo;
itakuwa siku ile, wengi watakapouawa,
minara itakapoanguka.
26Nao mwanga wa mwezi utakuwa kama wa jua,
nao mwanga wa jua utaongezeka mara saba,
uwe kama wa siku saba.
Itakuwa siku ile,
Bwana atakapovifunga vidonda vyao walio ukoo wake
na kuyaponya machubuko, aliyowapiga.
27Tazameni, Jina la Bwana linakuja toka mbali,
makali yake yanawaka, moshi mwingi unapanda,
midomo yake imejaa machafuko,
ulimi wake ni kama moto ulao!
28Pumzi yake ni kama mto udidimizao,
nayo maji yake hufika shingoni,
awapepete wamizimu katika pepeto liangamizalo,
atie mataifa mazima hatamu vinywani za kuwapoteza.
29Nanyi mtaimba, kama watu wanavyoimba
katika usiku wa kuandalia sikukuu,
mtafurahi mioyoni kama wasafiri
wanaokwenda na kupiga mazomari,
waje mlimani kwa Bwana aliye mwamba wa Isiraeli.
30Ndipo, Bwana atakapoipaza sauti yake yenye utukufu,
atauonyesha nao mkono wake, jinsi unavyokunjuka,
akifoka kwa ukali na kuwakisha ndimi za moto ulao,
akileta kimbunga na mvua yenye maji mengi
pamoja na mvua ya mawe.
31Kwani Waasuri watastushwa na sauti yake Bwana,
atakapowapiga kwa fimbo yake:
32kila mara fimbo ya kuwapiga itakapotokea,
Bwana akiielekeza, iwajie,
itakuwa kwa kupiga patu na mazeze,
vita vyake vitakuwa hivyo akiwatisha na kuwapigapiga.
33Kwani tangu kale pametengenezwa mahali
pa kuchinjia watu, wawe ng'ombe za tambiko,
naye mfalme amepatengenezewa pake,
napo ni papana na parefu kwenda chini;
kuzunguka hapo moto uko tayari,
hata kuni nyingi zimekwisha kupangwa;
pumzi ya Bwana yenye moto wa kiberitiberiti itaziwasha.