Yesaya 38

Kuugua na kupona kwake Hizikia.

(1-8: 2 Fal. 20:1-11; 2. Mambo 32:24.)

1Siku zile Hizikia akaugua, kufa kukamjia karibu. Ndipo, mfumbuaji Yesaya, mwana wa Amosi, alipokuja kwake, akamwambia: Hivi ndivyo, Bwana anavyosema: Yaliyo yako yaagizie walio wa mlango wako! Kwani wewe utakufa, hutarudi kuwa mzima tena.

2Hizikia akageuka na kuuelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana,

3akasema: E Bwana, na uukumbuke mwenendo, nilioufanya mbele yako kwa welekevu, nikayafanya kwa moyo wote mzima, yaliyo mema machoni pako. Kisha Hizikia akalia kilio kikubwa.[#2 Fal. 18:3-6.]

4Ndipo, neno la Bwana lilipomjia Yesaya kwamba:

5Nenda, umwambie Hizikia: Hivi ndivyo, Bwana Mungu wa baba yako Dawidi anavyosema: Nimesikia kuomba kwako, nikayaona hayo machozi yako. Basi, siku zako nitaziongeza na kukupa tena miaka kumi na mitano.

6Namo mkononi mwake mfalme wa Asuri nitakuponya, hata mji huu, maana nitaukingia mji huu.

7Nacho hiki kitakuwa kielekezo chako kitokacho kwa Bwana cha kwamba: Bwana atalifanya neno hili, alilolisema.

8Tazama: kuvuli kilichoshuka penye saa ya jua ya Ahazi nitakirudisha nyuma vipande kumi! Kisha jua likarudi penye saa ya jua vipande kumi, lilivyokuwa limevishuka.

9Huu ndio wimbo, Hizikia, mfalme wa Yuda, aliouandika katika ugonjwa wake alipokuwa amepona:

10Mimi nilisema:

Sasa, siku zangu zinapokuwa zimefika kati,

sharti niingie malangoni mwa kuzimu!

Nimenyang'anywa miaka yangu iliyosalia.

11Nilisema: Sitamwona Bwana tena,

maana Bwana yuko katika nchi yao walio hai;

huko kwao wakaao katika nchi ya vivuli

sitapata kuona mtu tena.

12Kituo changu kimeng'olewa,

kikachukuliwa kwangu kama hema la mchungaji;

nimezizinga siku za maisha yangu kama mfuma nguo

azikate penye nyuzi zinazozishika;

mchana utakapokuwa haujawa usiku bado, utanitowesha.

13Nikalia mpaka asubuhi,

maana aliivunja mifupa yangu sawasawa kama simba;

mchana utakapokuwa haujawa usiku bado, utanitowesha.

14Nikalia kama kinega au mbayuwayu

nikapiga kelele kama hua,

macho yangu yakafifia kwa kutazama juu kwamba:

Bwana ninakorofika! Nikomboe!

15Sasa nisemeje? Aliyoniambia, yeye ameyafanya.

Nami nitaendelea na kutulia miaka yangu yote

kwa ajili ya uchungu, roho yangu iliouona.

16Bwana! Kwa maneno kama hayo watu hupata uzima,

nao uzima wa roho yangu umo humo;

nami umeniponya na kunirudisha uzimani.

17Tazama! Uchungu uliokuwa kweli uchungu kwangu

umenipatia utengemano!

Kwa kunipenda wewe umeitoa roho yangu

mle shimoni mwa kutoweka,

kwani makosa yangu yote uliyatupa nyuma yako.

18Kwani kuzimuni siko, wanakokushukuru,

wala waliokufa sio wanaokushangilia,

wala walioshuka shimoni sio wanaoungojea welekevu wako.

19Aliye hai, kweli aliye hai ndiye

atakayekushukuru kama mimi leo.

Baba huwajulisha watoto mambo ya welekevu wako.

20Bwana ndiye aliyetaka kuniokoa;

kwa hiyo na tumpigie mazeze na kumwimbia

Nyumbani mwa Bwana siku zetu zote za kuwapo!

21Kisha Yesaya akasema, walete andazi la kuyu, waliweke juu ya jipu, apate kupona.[#2 Fal. 20:7.]

22Hizikia akasema: Kielekezo ni nini cha kwamba: Nitapanda tena kwenda nyumbani mwa Bwana?[#Yes. 38:7-8; 2 Fal. 20:8-11.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania