Yesaya 64

Kuendelea kuomba wokovu.

1Laiti ungizipasua mbingu, ukashuka,

milima ikitukutika mbele yako!

2Kama moto unavyokoleza vijiti, viwake,

au kama moto unavyochemsha maji,

hivyo wajulishe wapingani wako Jina lako,

wamizimu watetemeke mbele yako!

3Ungefanya matendo yatishayo, tusiyoyangojea,

ukashuka, milima ikitukutika mbele yako!

4Tangu kale hawakusikia, wala hawakupata habari,

wala macho hayakuona, ya kuwa yko Mungu

anayewafanyia matendo wamngojeao, isipokuwa wewe.

5Unawaendea wafurahiao kufanya yaongokayo,

nao wakukumbukao katika njia zako.

Tazama, ulikasirika, tulipokosa

na kuendelea hivyo siku nyingi,

lakini huko nyuma tukaokolewa.

6Sisi sote tumekuwa kama wachafu,

wongofu wetu wote ukawa kama nguo yenye madoadoa;

sisi sote tukanyauka kama majani,

mabaya yetu yakatuchukua,

kama upepo unavyochukua majani makavu.

7Hakuna alitambikiaye Jina lako,

hakuna ajihimizaye kukushika,

kwani umeuficha uso wako, tusiuone,

ukatuacha, tuzimie kwa nguvu za manza, tulizozikora.

8Na sasa, Bwana, wewe ndiwe baba yetu;

sisi tu udongo, nawe ndiwe mfinyanzi wetu,

sisi sote tu kazi za mikono yako.

9Bwana, usizidi kukasirika sana,

wala usizikumbuke manza kale na kale!

Twakuomba: Tutazame! Sisi sote tu ukoo wako!

10Miji yako mitakatifu imegeuka kuwa mapori,

hata Sioni ni pori tupu, Yerusalemu umeangamia.

11Nyumba yetu takatifu iliyokuwa yenye utukufu,

baba zetu walimokushangilia, imeteketezwa na moto;

yote, tuliyoyapenda sana, yamegeuka kuwa mabomoko.

12Bwana, kwa ajili ya hayo utawezaje kujizuia?

Utawezaje kunyamaza na kutuacha,

tuzidi kunyongeka sana?

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania