Yesaya 66

Mapatilizo ya wajanja.

1Hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Mbingu ni kiti changu cha kifalme,

nayo nchi ni pa kuiwekea miguu yangu.

Ni nyumba gani, mtakayonijengea?

Tena mahali pa kupumzikia mimi ni mahali gani?

2Hayo yote mkono wangu uliyafanya, yakawapo hayo yote;

ndivyo, asemavyo Bwana.

Ninaowatazama, ndio wakiwa

nao wapondekao rohoni,

nao wanaotetemeka wakalisikia Neno langu.

3Achinjaye ng'ombe huwa kama mwenye kuua mtu,

naye atoaye kondoo kuwa ng'ombe ya tambiko

huwa kama mwenye kunyonga mbwa,

naye atoaye vyakula kuwa vipaji vya tambiko

humwaga nazo damu za nguruwe,

avukizaye uvumba hutambikia mizimu:

hao ndio waliojichagulia njia zao,

nazo roho zao zikapendezwa na matapisho yao.

4Ndivyo, nami nitakavyojichagulia masumbufu ya kuwasumbua,

nayo matisho, waliyoyaogopa, nitayaleta kwao,

kwa kuwa nilipowaita, hawakujibu; niliposema, hawakusikia,

wakayafanya yaliyokuwa mabaya machoni pangu,

wakayachagua, ambayo nilikuwa zipendezwi nayo.

Wokovu na utukufu wa Yerusalemu mpya.

5Lisikilizeni Neno la Bwana,

mtetemekao mkilisikia Neno la Bwana!

Ndugu zenu wanaowachukia ninyi,

waliowafukuza kwa ajili ya Jina langu

walisema: Bwana na autokeze utukufu wake,

tuone, mkiufurahia!

Lakini wao watapatwa na soni.

6Usikilizeni uvumi uliomo mjini,

uliomo namo Nyumbani mwa Bwana!

Ni sauti ya Bwana

anayewalipisha adui matendo yao.

7Alipokuwa hajashikwa na uchungu bado amezaa,

alipokuwa hajaumwa bado amepata mtoto wa kiume.

8Yuko nani aliyesikia kama hayo?

Yuko nani aliyeona kama hayo?

Inakuwaje, nchi ikitokezwa siku moja?

Inakuwaje, ukoo mzima wa watu ukizaliwa kwa mara moja?

Kwani Sioni uliposhikwa na uchungu

papo hapo umewazaa watoto wake.

9Je? Mimi nifikishe watoto pa kuzaliwa, nisiwazalishe?

ndivyo, Bwana anavyosema.

Je? Mimi ninapozalisha, nilifunge tumbo la mama?

ndivyo, Mungu wako anavyosema.

10Changamkeni pamoja na Yerusalemu!

Ushangilieni, nyote mwupendao!

Furahini pamoja nao furaha kuu,

nyote mliousikitikia!

11Kwa maana mtayanyonya na kushiba

maziwa yake yenye matulizo ya moyo!

Kwa maana mtanyonya na kukamua,

mjipendezeshe kwa mfuriko wa utukufu wake.

12Kwani hivi ndivyo, Bwana anavyosema:

Tazameni! Nitauelekeza utengemano,

ufike kwake ukiwa kama mto mkubwa,

nayo matukufu ya wamizimu nitayalekeza,

yafike kwake yakiwa kama kijito kifurikacho maji.

Nanyi mtanyonya mkibebwa vifuani,

mtabembelezwa na kuwekwa magotini.

13Kama mama anavyoutuliza moyo wa mtoto wake,

ndivyo, nami nitakavyoituliza mioyo yenu;

namo Yerusalemu ndimo, mtakamotulizwa mioyo yenu.

14Mtakapoyaona, mioyo yenu itafurahi,

nayo mifupa yenu itachipuka kama majani mabichi,

nao mkono wake Bwana utajulikana kwa watumishi wake,

nayo makali yake yatajulikana kwa adui zake.

Mapatilizo ya mwisho.

15Kwani na mwone, Bwana anavyokuja motoni,

magari yake yakikimbizwa na upepo mkali,

awalipe kwa moto wa makali yake

na kwa mavumo ya moto uwakao na nguvu.

16Kwani Bwana atawapatiliza wote wenye miili ya kimtu

kwa moto na kwa upanga,

nao watakaouawa naye Bwana watakuwa wengi.

17Wajitakasao na kujeulia matambiko ya shambani

wakimfuata mtambikaji alioko kati yao,

nao walao nyama za nguruwe nazo za kibudu na za panya,

wote pamoja watatoweshwa; ndivyo, asemavyo Bwana.

18Nami ninayajua matendo yao na mawazo yao; patakuja, nitakapoyakusanya mataifa na misemo yote ya watu, nao watakuja, wauone utukufu wangu.

19Ndipo, nitakapowafanyizia kielekezo, nao waliookoka kwao wengine nitawatuma kwenda kwa wamizimu wa Tarsisi nako kwao wa Pulu na wa Ludu walio mafundi wa kupinda pindi, nako kwao wa Tubali na kwa Wagriki, nako kwenye visiwa vilivyoko mbali. Hawa hawajasikia habari za kwangu, hawajauona bado utukufu wangu; watautangaza utukufu wangu kwao hao wamizimu.[#Mat. 28:19.]

20Nao watawaleta ndugu zenu wote kuwa kipaji cha tambiko cha Bwana wakiwatoa kwenye mataifa yote; nao watapanda farasi na magari, wengine watachukuliwa katika machela, wengine watapanda nyumbu na ngamia, waje kufika Yerusalemu kwenye mlima wangu mtakatifu; ndivyo, Bwana anavyosema. Watawaleta hivyo, kama wana wa Isiraeli wanavyovipeleka vipaji vya tambiko Nyumbani mwa Bwana katika vyombo vilivyotakaswa.[#Yes. 60:3-7.]

21Namo mwao nitachukua wengine, wawe watambikaji na Walawi; ndivyo, Bwana anavyosema.[#Yes. 61:6.]

22Kwani kama zile mbingu mpya na nchi mpya, nitakazoziumba, zitakavyokaa mbele yangu, ndivyo, mazao yenu na majina yenu yatakavyokaa; ndivyo, asemavyo Bwana.[#Yes. 65:17.]

23Tena itakuwa, kila mara, mwezi utakapoandama, na kila mara, siku ya mapumziko itakapokutia, wote wenye miili ya kimtu watakuja kunitambikia; ndivyo, Bwana anavyosema.

24Kisha watatoka mjini, waitazame mizoga ya watu walionitengua; kwani mdudu mwenye kuwaumiza hatakufa, wala moto wa kuwala hautazimika, nao watakuwa tapisho kwao wote walio wenye miili ya kimtu.[#Mar. 9:44.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania