3 Mose 12

Mambo ya wanawake wazazi.

1Bwana akamwambia Mose kwamba:[#3 Mose 15:19.]

2Waambie wana wa Isiraeli kwamba: Mwanamke akipata mimba na kuzaa mtoto mume atakuwa mwenye uchafu siku saba, kama anavyokuwa mwenye uchafu siku zake za kuwa miezini.

3Siku ya nane mtoto na atahiriwe.[#1 Mose 17:11-12; Luk. 2:21; Yoh. 7:22.]

4Kisha huyo mwanamke na akae siku 33, damu yake ipate kutakata; cho chote kilicho kitakatifu asikiguse, wala asiingie Patakatifu, mpaka siku za weuo wake zitimie.

5Lakini akizaa mtoto mke atakuwa mwenye uchafu majuma mawili, kama vilivyo, akiwa miezini. Kisha atakaa siku 66, damu yake ipate kutakata.

6Siku za weuo wake kwa kuzaa mtoto mume au mke zitakapotimia, na apeleke mwana kondoo wa mwaka mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima na kinda la njiwa manga au hua kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo akiwafikisha hapo pa kuliingilia Hema la Mkutano kwake mtambikaji.

7Naye atamtolea Bwana hizo ng'ombe za tambiko na kumpatia upozi; ndipo, atakapotakata kwa ajili ya hiyo damu yake iliyomtoka. Haya ndiyo maonyo ya kufundisha mambo ya mwanamke aliyezaa mtoto mume au mke.

8Lakini mkono wake usipopata mwana kondoo na achukue hua wawili au makinda mawili ya njiwa manga, mmoja kuwa ng'ombe ya tambiko ya kuteketezwa nzima, wa pili kuwa ng'ombe ya tambiko ya weuo, mtambikaji ampatie upozi. Ndipo, atakapotakata.[#Luk. 2:24.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania