The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose: Waambie watambikaji, wana wa Haroni, kwamba: Mtambikaji asijipatie uchafu kwa kugusa mfu kwao walio ukoo wake,[#Ez. 44:20-25.]
2ila kwao tu walio ndugu zake wa kuzaliwa nao, maana ndio walio kwake karibu: mama yake na baba yake na mwanawe wa kiume na wa kike na mkubwa au mdogo wake,
3hata umbu lake aliyezaliwa naye akiwa ni mwanamwali bado, asipokuwa bado na mwanamume, basi, hata kwake ataweza kujipatia uchafu.
4Lakini kwa mwingine aliye wa ukoo wake, ijapo awe mkuu, asijipatie uchafu wa kuupoteza utakatifu wake.
5Wasijinyoe vichwani kuwa wenye kipara, wala ndevu zao wasizikate pembenipembeni, wala wasijichore nembo miilini mwao.[#3 Mose 19:27-28.]
6Sharti wawe watakatifu wa Mungu wao, wasilibezeshe Jina la Mungu wao. Kwani ndio wanaozitoa ng'ombe za tambiko za kumteketezea Bwana, zilizo chakula chake Mungu wao, kwa hiyo sharti wawe watakatifu.
7Mwanamke mgoni wasimchukue wala asiye mwenye macheo, wala mwanamke aliyefukuzwa na mumewe wasimchukue, kwani yeye ni mtakatifu wa Mungu wake.
8Nawe sharti umwazie kuwa mtakatifu kwa kuwa yeye ndiye anayemtolea Mungu wako chakula chake, kwa hiyo awe mtakatifu kwako, kwani mimi Bwana ninayewatakasa ninyi ni mtakatifu.
9Binti mtambikaji akianza kuzini humbezesha baba yake, kwa hiyo sharti ateketezwe kwa moto.
10Naye aliye mtambikaji mkuu miongoni mwa ndugu zake aliyemiminiwa kichwani pake mafuta ya kumpaka, aliyejazwa gao lake, apate kuyavaa yale mavazi yampasayo, asiziache wazi nywele za kichwani pake, wala asizirarue nguo zake,[#2 Mose 29:7; 3 Mose 10:6.]
11wala asiingie mo mote mwenye mfu ye yote, asijipatie uchafu, wala kwa baba yake wala kwa mama yake.
12Asitoke Patakatifu, asipapatie Patakatifu pa Mungu wake uchafu, kwani amekwisha kuvikwa kilemba, ndio mafuta ya Mungu wake yaliyompaka. Mimi ni Bwana.
13Naye mwanamke, atakayemchukua, sharti awe mwanamwali.
14Asichukue mjane wala aliyefukuzwa na mumewe wala mgoni asiye mwenye macheo, ila achukue mwanamwali tu aliye wa ukoo wao, apate kuwa mkewe.
15Ni kwamba: asiwatie uchafu walio wa uzao wake kwao walio ukoo wake, kwani mimi Bwana ndiye aliyemtakasa.
16Bwana akamwambia Mose kwamba:
17Mwambie Haroni kwamba: Mtu aliye wa vizazi vitakavyozaliwa nao walio wa uzao wako, kama ni mwenye kilema, asije kumtolea Mungu wake chakula chake.
18Kila mtu mwenye kilema asinikaribie, kama ni kipofu au kiwete au mwenye pua mbaya au mwenye kiungo kilicho kirefu zaidi,
19au kama ni mtu aliyevunjika mguu au mkono,
20au kama ni mwenye nundu au mwenye kifua kikuu au mwenye chongo au mwenye upele mbaya au mwenye buba au mwenye mapumbu yaliyovunjika.
21Kila mwenye kilema aliye wa uzao wake mtambikaji Haroni asije kumtolea Bwana ng'ombe za tambiko za kuteketezwa; kwa kuwa mwenye kilema asije kumtolea Mungu wake chakula chake.
22Lakini kula ataweza kula chakula cha Mungu wake kilicho kitakatifu chenyewe nacho kilicho kitakatifu.
23Asiingie tu hapo mbele ya lile pazia, wala asiijie meza ya kutambikia kwa kuwa mwenye kilema, asipapatie Patakatifu pangu uchafu. Kwani mimi ni Bwana anayepatakasa.
24Nayo maneno haya Mose akamwambia Haroni na wanawe na watu wote wa Isiraeli.