3 Mose 24

Agizo la kuziwasha taa za kinara cha Patakatifu.

1Bwana akamwambia Mose kwamba:

2Waagize wana wa Isiraeli, wakupatie mafuta ya chekele yaliyotwangwa vema kuwa safi ya kinara ya kutia siku zote katika taa zake.[#2 Mose 27:20.]

3Hapo nje ya pazia penye Sanduku la Ushahidi katika Hema la Mkutano Haroni azitengeneze hizo taa, ziwake tangu jioni hata asubuhi mbele ya Bwana pasipo kukoma. Maongozi haya na yawe ya kale na kale kwa vizazi vyenu.

4Penye kile kinara cha dhahabu tupu na azitengeneze taa zake, ziwake mbele ya Bwana siku zote.

Agizo la kuweka mikate mezani pa Bwana.

5Tena uchukue unga mwembamba, uuoke kuwa mikate kumi na miwili, kila mikate mmoja uwe wa pishi moja ya unga.

6Kisha uiweke mistari miwili, kila mstari wenye mikate sita, juu ya meza ya dhahabu tupu mbele ya Bwana.[#2 Mose 25:30.]

7Kisha uweke juu ya kila mstari uvumba ulio safi, uwe moto wa kumpendeza Bwana na kumkumbusha hiyo mikate.

8Kila siku ya mapumziko sharti aitengeneze tena mbele ya Bwana pasipo kukoma. Hili na liwe agano la kale na kale nao wana wa Isiraeli, wasiache kuitoa.

9Kisha hiyo mikate itakuwa yao Haroni na wanawe, nao sharti waile mahali patakatifu. Kwa kuwa mitakatifu yenyewe sharti iwe fungu lao litokalo kwenye mioto ya Bwana. Hii na iwe haki yao ya kale na kale.

Agizo la kuwaua wamtukanao Mungu.

10Ikawa, mwana wa mwanamke wa Kiisiraeli mwenye baba wa Kimisri alipotokea katikati ya wana wa Isiraeli, huyu mwana wa mwanamke wa Kiisiraeli akagombana na mtu wa Kiisiraeli makambini.

11Naye yule mwana wa mwanamke wa Kiisiraeli akalitukana Jina la Bwana pamoja na kuliapiza. Ndipo, walipompeleka kwa Mose, nalo jina la mama yake lilikuwa Selomiti, binti Diburi, wa shina la Dani.[#3 Mose 24:16.]

12Wakamweka kifungoni, wapate kuelezwa, kinywa cha Bwana kitakavyowaambia.[#4 Mose 15:34.]

13Bwana akamwambia Mose kwamba:

14Huyo mwenye kutukana mtokeze nje ya malago, kisha wote walioyasikia na wambandikie mikono yao kichwani pake, kisha watu wote wa mkutano huu na wamwue kwa kumpiga mawe.

15Lakini wana wa Isiraeli waambie kwamba: Mtu ye yote atakayemwapiza Mungu wake sharti alipishwe hilo kosa lake.

16Atakayelitukana Jina la Bwana sharti auawe kabisa, watu wote wa mkutano huu wakimpiga mawe. Kama ni mgeni au kama ni mwenyeji, kwa kulitukana hilo Jina hana budi kuuawa.[#2 Mose 20:7; Mat. 26:65.]

Mapatilizo yao wanaoumiza wenzao.

17Mtu akimpiga mwenzake, afe, sharti auawe naye.

18Lakini akipiga nyama, naye akifa, sharti amlipe, nyama aliye mzima kwa yule aliyekufa.[#2 Mose 21:12.]

19Mtu akimwumiza mwenziwe, apate kilema, naye sharti afanyiziwe yaleyale, aliyoyafanya:[#2 Mose 21:23-25.]

20kidonda kwa kidonda, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kilema, alichompatia mwenzake, apatiwe naye.

21Ni hivi: mtu atakayempiga nyama, naye akifa, sharti amlipe; lakini mtu atakayempiga mwenziwe, naye akifa, sharti auawe.

22Hukumu za kwenu sharti ziwe moja, mwenye kuhukumiwa kama ni mgeni au kama ni mwenyeji. Kwani mimi Bwana ni Mungu wenu.[#2 Mose 12:49; 3 Mose 19:34.]

23Mose alipokwisha kuwaambia wana wa Isiraeli maneno haya, wakamtokeza yule mwenye kutukana nje ya makambi, wakamwua kwa kumpiga mawe; wana wa Isiraeli wakafanya, kama Bwana alivyomwagiza Mose.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania