The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kule mlimani kwa Sinai kwamba:
2Sema na wana wa Isiraeli na kuwaambia: Mtakapoingia katika nchi hiyo, nitakayowapa, hiyo nchi nayo sharti ipate kumpumzikia Bwana.
3Miaka sita upande mbegu mashambani kwako, tena miaka sita uikatie mizabibu yako, upate kuyachuma mazao yao.[#2 Mose 23:10-11; 5 Mose 15:1-11.]
4Lakini mwaka wa saba sharti uiwie nchi yako mwaka wa kupumzika kabisa, nayo ipate kumpumzikia Bwana. Hapo usipande mbegu mashambani kwako, wala usiikatie mizabibu yako.
5Nayo masazo ya mavuno yako, kama yataota yenyewe, usiyavune, wala zabibu zitakazozaliwa na mizabibu, usiyoitunza, usizichume, kwani mwaka huu sharti uwe kabisa mwaka wa mapumziko ya nchi.
6Nchi itakayoyazaa katika mwaka wa mapumziko, na myale ninyi na watumishi wako na vijakazi wako na watu wako wa mshahara nao wageni watakaokaa kwako,
7nao nyama wako wa kufuga na nyama wa porini walioko katika nchi yao; hao wote na wayale mazao yake.
8Tena uhesabu miaka saba ya mapumziko, ndio miaka saba mara saba, siku za hiyo miaka saba ya mapumziko ziwe kwako miaka 49.
9Ndipo upige baragumu lenye sauti kuu katika mwezi wa sababu siku ya kumi ya mwezi. Siku ya Mapoza sharti mpige mabaragumu po pote katika nchi yenu yote nzima.[#3 Mose 23:27.]
10Mwaka huo wa 50 sharti mwutakase na kuwatangazia wote wakaao katika nchi yenu, ya kuwa wamekwisha kukombolewa. Mwaka huo uwe wa kupiga shangwe kwenu, mkirudia kila mtu mali zilizokuwa zake, tena mkirudi kila mtu kwa ndugu zake.[#Yes. 61:2; Luk. 4:19.]
11Kweli mwaka huo wa hamsini sharti uwe kwenu mwaka wa kupiga shangwe, msipande mbegu, wala msiyavune yatakayoota yenyewe, wala msiyachume mazao ya mizabibu, msiyoitunza.
12Kwani ndio mwaka wa shangwe, nao sharti uwe mtakatifu kwenu, myale tu mashambani yatakayozaliwa.
13Katika mwaka ulio wa shangwe kila mtu wa kwenu sharti azirudie mali zilizokuwa zake.
14Kwa hiyo akimwuzia mwenzake kitu au akinunua kitu mkononi mwa mwenzake, msidanganyane wenyewe na wenyewe.[#1 Tes. 4:6.]
15Ukinunua shamba kwa mwenzako, sharti mwihesabu miaka iliyopita tangu mwaka wa shangwe, ndipo akuuzie kwa kuipunguza hiyo miaka, aliyolivuna.
16Miaka itakayosalia ikiwa mingi, mwiongeze bei yake; lakini miaka itakayosalia ikiwa michache, mwipunguze bei yake, kwani yeye hukuuzia mavuno ya miaka tu inayohesabika.
17msidanganyane wenyewe na wenyewe. Sharti mmwogope Mungu wenu, kwani mimi Bwana ni Mungu wenu.
18Yafanyeni maongozi yangu na maamuzi yangu mkiyaangalia na kuyafanya! Ndipo, mtakapokaa katika nchi hiyo na kutulia.[#3 Mose 26:5; 1 Fal. 4:25.]
19Nayo nchi hiyo itawapa mazao yake, mle na kushiba, nanyi mtakaa huko na kutulia.
20Mkiuliza: Tutakula nini katika mwaka wa saba, tusipopanda mbegu, tena tusipoyakusanya mapato yatupasayo?
21jueni: Katika mwaka wa sita nitawaagizia neema yangu, huo mwaka uwapatie mapato ya miaka mitatu.[#5 Mose 28:8.]
22Mpande tena mbegu katika mwaka wa nane mkila mapato ya kale; mpaka mtakapoingiza mavuno ya mwaka wa tisa, na myale yale ya kale.
23Nchi isiuzwe kabisa kabisa! Kwani nchi ni yangu mimi, nanyi m wageni tu wanaokaa kwangu.[#Sh. 39:13.]
24Po pote, mtakapotwaa nchi kuwa yenu, sharti mwache njia ya kuikomboa hiyo nchi.
25Ndugu yako akiuza kipande cha shamba, alilolitwaa kuwa lake, kwa kukosa mali, tena akija mkombozi wake aliye ndugu yake wa kuzaliwa naye, basi, na akikomboe hicho kipande, ndugu yake alichokiuza.[#Ruti 4:3-4.]
26Kama mtu hana mkombozi, lakini akiweza kujipatia kwa mkono wake mali zitoshazo za kukikomboa,
27na aihesabu hiyo miaka iliyopita tangu hapo, alipokiuza, nazo mali zitakazosalia sharti amrudishie yule mtu aliyemwuzia hicho kipande cha shamba. Hivyo ndivyo, atakavyokirudia, kiwe chake tena.
28lakini asipoweza kujipatia kwa mkono wake mali zitoshazo, basi, hicho kipande cha shamba, alichokiuza, kitakaa mkononi mwake yule aliyemwuzia, hata mwaka wa shangwe utakapotimia; katika huo mwaka wa shangwe kitatoka mkononi mwake yule, mwenyewe apate kukirudia, kiwe mali yake tena.
29Mtu akiuza nyumba ya kukaa katika mji wenye boma, sharti apate mwaka mzima wa kuikomboa; hizo na ziwe siku zake za kuikomboa.
30Lakini isipokombolewa, hata mwaka wote mzima utimie, basi, hiyo nyumba iliyomo mjini mwenye boma itakuwa kabisa kabisa yake aliyeinunua kuwa yake yeye mwenyewe na ya vizazi vyake, haitatoka kwao katika mwaka wa shangwe.
31Lakini nyumba za vijiji vya huko nje po pote visivyo vyenye maboma na ziwaziwe kuwa sawa na mashamba ya hiyo nchi, ziwezekane kukombolewa, tena katika mwaka wa shangwe zitoke kwake mnunuzi.
32Namo mijini mwa Walawi nyumba za hiyo miji waliyopewa kuwa fungu lao, zitaweza kukombolewa na Walawi kila mwaka.[#4 Mose 35.]
33Kama mtu anakomboa kwao Walawi nyumba au mji, katika mwaka wa shangwe itatoka kwake na kukoma kuwa mali yake, kwani nyumba za miji ya Walawi ni fungu lao walilopewa kuwa lao kabisa katikati ya wana wa Isiraeli.
34Lakini malisho ya miji yao hayauziki, kwani ni fungu lao kuwa yao kale na kale.
35Ndugu yako akipatwa na ukosefu wa mali, asiweze tena kushikana mkono na wewe, sharti umpokee kuwa mgeni akaaye kwako na kujitunza kwako.
36Usimtoze faida ya kukopesha iliyo nyingi, ila umwogope Mungu wako, ndugu yako apate kujitunza kwako.[#5 Mose 23:20.]
37Wala usimkopeshe fedha zako kwa kujitakia faida, wala usimpe chakula chake kwa kujitakia malipo yapitayo kiasi.
38Mimi Bwana ni Mungu wenu aliyewatoa ninyi katika nchi ya Misri, niwape nchi ya Kanaani, niwe Mungu wenu.
39Ndugu yako akipatwa na ukosefu wa mali hapo alipo, akajiuza kwako, usimfanyishe kazi za utumwa.[#2 Mose 21:2.]
40Ila awe kwako kama mtu wa mshahara au kama mwingine akaaye kwako. Naye na akutumikie, hata mwaka wa shangwe utimie.
41Ndipo, atakapopata kutoka kwako, yeye pamoja na watoto wake, arudi kwao walio ndugu zake, tena na alirudie fungu lao lililokuwa lao baba zake.
42Kwani ndio watumwa wangu mimi, niliowatoa katika nchi ya Misri, hawawezekani kuuzwa kuwa watumwa wenyewe.
43Nawe usimtawale kwa ukorofi, ila umwogope Mungu wako!
44Kama unataka kuwa mwenye watumwa wako na vijakazi wako, jinunulie watumwa na vijakazi kwao wamizimu watakaokaa na kuwazunguka ninyi.[#3 Mose 25:53; Ef. 6:9.]
45Hata kwa wana wao watakaokaa kwenu ugenini mtaweza kujinunulia, hata kwao wa uzao wao wataokaa kwenu, wao watakaozaliwa katika nchi yenu, basi, hao wataweza kuwa mali zenu.
46Hata wana wenu wataokuwa nyuma yenu mtaweza kuwaachilia hao kuwa urithi wao wa mali zitakazokuwa zao kale na kale, nao mwafanyishe kazi za utumwa. Lakini ndugu zenu walio wana wa Isiraeli msitawalane wenyewe na wenyewe kwa ukorofi.
47Mgeni au mwingine atakayekaa kwako akijipatia mali kwa kazi za mkono wake, naye ndugu yako anapatwa na ukosefu wa mali hapo alipo huyo, akajiuza kwake huyo mgeni au kwa mwingine atakayekaa kwako au kwa mwingine aliye wa ukoo mgeni,
48sharti awe na njia ya kukombolewa akiisha kujiuza; kila mmoja wao walio ndugu zake ataweza kumkomboa,
49au baba yake mkubwa au mdogo, au mwanawe ataweza kumkomboa, au mmoja wao waliozaliwa naye katika mlango wake ataweza kumkomboa au mwenyewe ataweza kujikomboa akijipatia mali za kutosha kwa kazi za mkono wake.
50Ndipo yeye pamoja naye aliyemnunua na waihesabu miaka tangu hapo, alipojiuza mpaka hapo, mwaka wa shangwe utakapotimia, kisha fedha za kumnunua na zigawanywe sawasawa kwa hesabu ya hiyo miaka kuwa kama mshahara wa miaka ya mtu wa kazi.
51Kama miaka iko mingi bado, basi, katika hizo fedha, alizozipata alipojiuza, na arudishe hizo ziipasazo miaka iliyosalia kuwa makombozi yake.
52Lakini kama miaka iko michache bado, mpaka mwaka wa shangwe utakapotimia, basi, na azirudishe hizo tu ziipasazo hiyo miaka yake michache kuwa makombozi yake.[#3 Mose 25:43.]
53Kwake Bwana wake na awe kama mtu wa kazi za mshahara mwaka kwa mwaka, naye yule asimtawale kwa ukorofi machoni pako.
54Asipokombolewa kwa njia hii, atatoka utumwani katika mwaka wa shangwe, yeye pamoja na watoto wake.
55Kwani wana wa Isiraeli ni watumwa wangu mimi; ndio watumwa wangu, niliowatoa katika nchi ya Misri. Mimi Bwana ni Mungu wenu.