The chat will start when you send the first message.
1Bwana akamwambia Mose kwamba:[#4 Mose 30.]
2Sema nao wana wa Isiraeli na kuwaambia: mtu akitaka kuyalipa, aliyoyaapa ya kujitoa kuwa wake Bwana, sharti wewe uyapime makombozi ya mtu.
3Nacho kipimo chako ni hiki: mtu mume aliye wa miaka ishirini mpaka sitini makombozi yake, utakayompimia, ni fedha hamsini, zikipimwa na mizani ya Patakatifu.
4Kama ni mwanamke, makombozi yake utakayompimia, ni fedha thelathini.
5Akiwa na miaka mitano mpaka ishirini, makombozi yake, utakayompimia, ni fedha ishirini, kama ni mtu mume; kama ni mwanamke, ni fedha kumi tu.
6Akiwa wa mwezi mmoja mpaka miaka mitano, makombozi yake, utakayompimia, ni fedha tano, kama ni mtu mume; kama ni mwanamke, utampimia makombozi ya fedha tatu tu.
7Akiwa wa miaka sitini na zaidi, kama ni mtu mume, makombozi yake, utakayompimia, ni fedha kumi na tano; kama ni mwanamke, fedha zake ni kumi.
8Lakini kama ni mkosefu wa mali, asiweze kuyalipa hayo makombozi, uliyompimia, na wamsimamishe mbele ya mtambikaji, naye mtambikaji na ampimie makombozi yake akiyalinganisha na mali, yule mwenye kuapa anazoweza kuzipata kwa mkono wake; hicho kiwe kipimo chake mtambikaji cha kumpimia hayo makombozi.
9Kama ni nyama, watu wanayemtolea Bwana kuwa toleo la tambiko, kila mmoja, atakayemtoa katika nyama hao, atakuwa mtakatifu,
10wasimbadilishe wala wasilete mwingine pia, kama mwema kwa mbaya au mbaya kwa mwema. Kama mtu anabadilisha nyama kwa nyama, wote wawili watakuwa watakatifu, yule wa kwanza na yule, aliyemleta wa kubadili.
11Kama nyama ni mwenye uchafu, wsiweze kumtolea Bwana kuwa ng'ombe ya tambiko, na wamsimamishe huyo nyama mbele ya mtambikaji.
12Naye mtambikaji na ayapime makombozi yake kwa kumpambanua kuwa mwema au mbaya, nayo makombozi yake, mtambikaji atakayoyapima kuwa sawa, basi, yatakuwa yaleyale.
13Naye kama anataka kumkomboa kweli, ataongeza fungu la tano la hayo makombozi, uliyoyapima.
14Mtu akiitakasa nyumba yake kuwa kipaji kitakatifu cha Bwana, mtambikaji na ayapime makombozi yake kwa kuipambanua kuwa njema au mbaya; nayo makombozi, mtambikaji atakayoyapima, yatakuwa yaleyale.
15Kama mwenye kuitakasa anataka kuikomboa na aongeze fungu la tano la fedha, ulizozipima kuwa makombozi yake, kisha itakuwa yake tena.
16Mtu akitakasa kipande cha shamba lililo fungu lake kuwa mali ya Bwana, utayapima makombozi yake kwa kipimo cha mbegu zinazoenea hapo: kama hicho kipande cha shamba kinataka mbegu za mawele frasila kumi makombozi yake ni fedha hamsini.
17Kama yule mtu anakitakasa kile kipande cha shamba lake kuanzia katika mwaka wa shangwe, makombozi yake ni yaleyale, uliyoyapima.
18Kama anakitakasa baada ya mwaka wa shangwe, mtambikaji na amhesabie fedha kwa hesabu ya miaka itakayosalia mpaka mwaka wa shangwe utimie; vivi hivi fedha za makombozi, alizozipima, zitapunguzwa.
19Kama mwenye kulitakasa shamba lake anataka kulikomboa, sharti aongeze fungu la tano la fedha za makombozi, uliyoyapima, kisha litakuwa lake tena.
20Lakini kama halikomboi hilo shamba, akaliuza kwa mtu mwingine, haliwezekani kukombolewa tena.
21Kwani hapo, litakapotoka katika mwaka wa shangwe kwake aliyelinunua, litakuwa mali ya Bwana kama shamba lililotiwa mwiko wa kuwa mali ya mtu; nalo litakuwa fungu lake mtambikaji.
22Mtu akitoa shamba, alilolinunua, lisilo shamba la fungu lake mwenyewe, akilitakasa kuwa lake Bwana,
23mtambikaji na amtolee jumla ya fedha, ulizozipima kuwa makombozi yake, mpaka mwaka wa shangwe utakapotimia; nazo hizo, ulizozipima, sharti yule azitoe siku hiyo kuwa mali za Bwana.
24Katika mwaka wa shangwe shamba hilo litarudi kwake yeye, ambaye alilinunua kwake, maana ni fungu lake la nchi lililo lake mwenyewe.[#3 Mose 25:10.]
25Nayo makombozi yote, utakayoyapima, sharti uyapime kwa fedha zilizopimwa kwa mizani ya Patakatifu, fedha moja iwe ya thumuni nane.
26Wana wa kwanza wa nyama wa kufuga mtu asiwatakase kuwa wake Bwana, kwani ndio wake Bwana kwa kuzaliwa wa kwanza, kama ni ng'ombe, au kama ni mbuzi au kondoo, ni wake Bwana.[#2 Mose 13:2.]
27Kama ni mwana wa nyama mwenye uchafu, anaweza kumkomboa kwa kulipa makombozi, uliyoyapima, na kuongeza fungu lao la tano; lakini asipomkomboa atauzwa kwa hayo makombozi, uliyoyapima.
28Yo yote, mtu atakayomtolea Bwana kuwa yake kwa kuyatia mwiko wa kutunzwa na mtu, akiyatoa katika yo yote yaliyo yake yeye, kama ni mtu au nyama wa kufuga au shamba lililo la fungu lake mwenyewe, hayawezekani wala kuuzwa wala kukombolewa, maana yote pia yaliyotiwa mwiko wa kutunzwa na mtu ni matakatifu yenyewe, ni yake Bwana.[#4 Mose 18:14; 21:2.]
29Mtu ye yote aliyetiwa huo mwiko wa kutunzwa na mtu hawezekani kukombolewa, hana budi kuuawa kabisa.[#1 Sam. 15:3,9.]
30Kila fungu la kumi la nchi, kama ni la mbegu za nchi au kama ni la matunda ya nchi, ni lake Bwana, ni mali takatifu za Bwana.[#4 Mose 18:21.]
31Kama mtu anataka kulikomboa fungu lake la kumi, sharti aongeze fungu la tano la fedha zake.
32Hata kila fungu la kumi la ng'ombe na la mbuzi na la kondoo, yaani kila atakayepita chini ya fimbo, ni fungu la kumi lililo mali takatifu za Bwana.
33Hapo watu wasitazame sana, kama ni mwema au kama ni mbaya, wala wasimbadilishe. Kam mtu anambadilisha, yule wa kwanza pamoja na badili yake watakuwa wote wawili mali takatifu za Bwana, wasiwezekane kukombolewa.
34Haya ndiyo maagizo, Bwana aliyomwagiza Mose mlimani kwa Sinai ya kuwaambia wana wa Isiraeli.[#3 Mose 26:46.]