The chat will start when you send the first message.
1Mwaka wa 15 wa kutawala kwake Kaisari Tiberio Pontio Pilato alikuwa mtawala nchi ya Yudea, naye Herode alikuwa mfalme wa Galilea, naye Filipo, ndugu yake, alikuwa mfalme wa Iturea na wa nchi ya Tarakoniti, naye Lisania alikuwa mfalme wa Abilene,
2tena Ana na Kayafa walikuwa watambikaji wakuu. Hapo ndipo, neno la Mungu lilipomjia Yohana, mwana wa Zakaria, huko nyikani.
(3-18: Mat. 3:1-12; Mar. 1:1-8.)3Akaenda katika nchi zote za kando ya Yordani, akatangaza ubatizo wa kujutisha, wapate kuondolewa makosa.[#Mar. 1:4.]
4Ikawa, kama ilivyoandikwa kitabuni mwa maneno ya mfumbuaji Yesaya:
Iko sauti ya mtu apigaye mbiu nyikani:
Itengenezeni njia ya Bwana!
Yanyosheni mapito yake!
5Vibonde vyote vifukiwe,
navyo vilima vyote na vichuguu vyote vichimbuliwe!
Napo palipopotoka panyoshwe,
napo penye mashimo pawe njia za sawasawa,
6wote wenye miili wauone wokovu wake Mungu.
7Akawaambia makundi ya watu waliotokea, wabatizwe naye: Ninyi wana wa nyoka, nani aliwaambia ninyi, ya kuwa mtayakimbia makali yatakayokuja?[#Mat. 23:33.]
8Tendeni mazao yaliyo ya kujuta kweli! Msianze kusema mioyoni mwenu: Tunaye baba yetu, ndiye Aburahamu! Kwani nawaambiani: Katika mawe haya ndimo, Mungu awezamo kumwinulia Aburahamu wana.
9Miti imekwisha wekewa mashoka mashinani, kila mti usiozaa matunda mazuri hukatwa, utupwe motoni.
10Yale makundi ya watu wakamwuliza wakisema: Basi, tufanye nini?
11Akajibu akiwaambia: Mwenye nguo mbili amgawie mwenziwe asiye nayo, naye mwenye vyakula na afanye vilevile!
12Watoza kodi nao walipokuja, wabatizwe, wakamwuliza: Mfunzi, tufanye nini?
13Naye akawaambia: Msitoze kuvipita hivyo, mlivyoagizwa!
14Walipomwuliza nao askari wakisema: Nasi tufanye nini? akawaambia: Msimwendee mtu kwa nguvu wala kwa ukorofi, tena mtoshewe na mishahara yenu!
15Watu walipokuwa wakingoja, vya Yohana vitakapotokea wazi, wote waliwaza mioyoni mwao kwamba: Yeye labda ni Kristo; ndipo, Yohana[#Yoh. 1:19-28.]
16aliposema akiwaambia wote: Mimi nawabatiza kwa maji; lakini anakuja aliye na nguvu kunipita mimi, nami sifai kumfungulia kanda za viatu vyake. Yeye atawabatiza katika Roho takatifu na katika moto.
17Ungo wa kupepetea umo mkononi mwake, apafagie pake pa kupuria ngano; ngano atazikusanya, aziweke chanjani mwake, lakini makapi atayachoma kwa moto usiozimika.
18Hivyo aliwapigia watu mbiu njema na kuwaonya hata mengine mengi.
19Lakini mfalme Herode alipoumbuliwa naye kwa ajili ya Herodia, mke wa nduguye, na kwa ajili ya mabaya yote, Herode aliyoyatenda,[#Mat. 14:3-4; Mar. 6:17-18.]
20akayaongeza mabaya yake na kumfunga Yohanba kifungoni.
21Lakini watu wote walipokuwa wakibatizwa, Yesu anaye alipobatizwa, ikawa, alipokuwa katika kuomba, ndipo, mbingu zilipofunuka,
22Roho Mtakatifu akamshukia mwenye mwili kama wa njiwa, sauti ikatoka mbinguni: Wewe ndiwe mwanangu mpendwa, nimependewa na wewe.[#Luk. 9:35.]
23Yesu alipoianza kazi yake alikuwa wa miaka kama 30. Akadhaniwa kuwa mwana wa Yosefu, wa Eli,[#Luk. 4:22.]
24wa Matati, wa Lawi, wa Melki, wa Yanai, wa Yosefu,
25wa matatia, wa Amosi, wa Nahumu, wa Esili, wa Nagai,
26wa Mahati, wa Matatia, wa Simei, wa Yoseki, wa Yoda,
27wa Yohana, wa Resa, wa Zerubabeli, wa Saltieli, wa Neri,
28wa Melki, wa Adi, wa Kosamu, wa Elmadamu, wa Heri,
29wa Yesu, wa Eliezeri, wa Yorimu, wa Matati, wa Lawi,
30wa Simeoni, wa Yuda, wa Yosefu, wa Yonamu, wa Eliakimu,
31wa Melea, wa Mena, wa Matata, wa Natani, wa Dawidi,[#2 Sam. 5:14.]
32wa Isai, wa Obedi, wa Boazi, wa Salmoni, wa Nasoni,[#Ruti 4:17-22.]
33wa Aminadabu, wa Ramu, wa Hesiromu, wa Peresi, wa Yuda,[#1 Mose 29:35.]
34wa Yakobo, wa Isaka, wa Aburahamu, wa Tera, wa Nahori,[#1 Mose 21:2-3; 11:10-26.]
35wa Serugi, wa Ragau, wa Pelegi, wa Eberi, wa Sala,[#1 Mambo 1:24-27.]
36wa Kenani, wa Arpakisadi, wa Semu, wa Noa, wa Lameki,[#1 Mose 5:3-32.]
37wa Metusela, wa Henoki, wa Yaredi, wa Mahalaleli, wa Kenani,
38wa Enosi, wa Seti, wa Adamu wa Mungu.[#1 Mose 5:1-3.]