Luka 4

Kujaribiwa kwa Yesu.

(1-13: Mat. 4:1-11; Mar. 1:12-13.)

1Yesu akajaa Roho takatifu, akarudi akitoka huko Yordani, akapelekwa na Roho nyikani,

2akajaribiwa siku 40 na Msengenyaji. Siku zile hakula cho chote; zilipokwisha pita, akaona njaa.

3Msengenyaji akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili, liwe chakula!

4Yesu akamjibu akisema: Imeandikwa:

Mtu hataishi kwa chakula tu, ila kwa kila neno la Mungu.

5Kisha akampandisha mlimani, akamwonyesha kwa kitambo kidogo ufalme wote pia wa ulimwengu.

6Kisha Msengenyaji akamwambia: Nguvu hii yote na utukufu wake nitakupa wewe; kwani mimi nimepewa, nami humpa ye yote, nimtakaye.

7Basi, wewe ukiniangukia hapa machoni pangu, yote yatakuwa yako.

8Yesu akajibu akimwambia: Ondoka nyuma yangu, Satani! Imeandikwa:

Umwangukie Bwana Mungu wako na kumtumikia peke yake!

9Kisha akampeleka Yerusalemu, akamsimamisha juu pembeni hapo Patakatifu, akamwambia: Kama ndiwe Mwana wa Mungu, ruka hapa, ujitupe chini!

10Kwani imeandikwa:

Atakuagizia malaika zake, wakulinde,

11nao watakuchukua mikononi mwao,

usije kujikwaa mguu wako katika jiwe.

12Yesu akajibu akimwambia: Liko neno la kwamba:

Usimjaribu Bwana Mungu wako!

13Msengenyaji alipokwisha kumjaribu yote akaondoka, akamwacha kwanza.[#Luk. 22:28; Ebr. 4:15.]

Mahubiri katika Nasareti.

(14-15: Mat. 4:12-17; Mar. 1:14-15.)

14Yesu akarudi Galilea mwenye nguvu ya Roho, akavumika katika nchi zote zilizoko pembenipembeni.

15Naye alipofundisha katika nyumba zao za kuombea akatukuzwa nao wote.

(16-30: Mat. 13:53-58; Mar. 6:1-6.)

16*Alipofika Nasareti, - ndio mji, alimolelewa, - akaingia siku ya mapumziko nyumbani mwa kuombea, kama alivyozoea. Alipoinuka kuwasomea

17akapewa kitabu cha mfumbuaji Yesaya; alipokifunua hicho kitabu akaona mahali palipolandikwa:[#Yes. 61:1-2.]

18Roho ya Bwana inanikalia,

kwa hiyo ameanipaka mafuta,

niwapigie maskini mbiu njema.

Amenituma, niwatangazie mateka,

ya kuwa watakombolewa,

nao vipofu, ya kuwa wataona,

niwape ruhusa walioumizwa, wajiendee,

19niutangaze mwaka wa Bwana upendezao.[#3 Mose 25:10.]

20Kisha akakifunga kitabu, akamrudishia mtumishi, akaketi. Ndipo, wote waliokuwamo humo nyumbani mwa kuombea walipomkazia macho,

21akaanza kuwaambia: Leo hivi yaliyoandikwa hapa yametimia masikioni penu.*

22Nao wote wakamshuihudia ya kuwa ndivyo, wakastaajabu maneno ya upole yaliyotoka kinywani mwake, wakasema: Huyu si mwana wa Yosefu?[#Luk. 3:23; Yoh. 6:42.]

23Akawaambia: Kweli mtaniambia fumbo hili: Mganga, jiponye mwenyewe! Hata huku kwako, ulikokulia, yafanye, tuliyoyasikia, ya kuwa yamefanyika Kapernaumu![#Mat. 4:13.]

24Lakini akasema: Kweli nawaambiani: Hakuna mfumbuaji anayepokelewa kwao, alikokulia.[#Yoh. 4:44.]

25Nawaambiani ya kweli: Siku za Elia kulikuwa na wajane wengi katika Waisiraeli; ni hapo, mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, ikawa njaa kubwa katika nchi zote.[#1 Fal. 17:1,9; 18:1; Yak. 5:17.]

26Lakini hao Elia hakutumwa kwa mwenzao mmoja, ila alitumwa Sareputa wa Sidoni kwa mwanamke mjane wa kule.

27Tena siku za mfumbuaji Elisa kulikuwa na wenye ukoma wengi katika Waisiraeli, lakini kwao hao hakuna aliyetakaswa ila Namani wa Ushami.[#2 Fal. 5:14.]

28Wote waliokuwamo humo nyumbani mwa kuombea walipoyasikia haya, mioyo yao ikajaa makali,

29wakainuka, wakamfukuza mjini, wakampeleka ukingoni pa mlima, ambao mji wao ulikuwa umejengwa juu yake, wapate kumsukuma chini.

30Lakini yeye akapita katikati yao, akaenda zake.

Mwenye pepo.

(31-37: Mar. 1:21-28.)

31Akashuka kwenda Kapernaumu, mji wa Galilea, akawa akiwafundisha siku ya mapumziko.[#Mat. 4:13; Yoh. 2:12.]

32Nao wakashangazwa na mafundisho yake, kwani maneno yake yalikuwa yenye nguvu.[#Mat. 7:28-29; Yoh. 7:46.]

33Humo nyumbani mwa kuombea mkawa na mtu mwenye pepo mchafu, akapaza sauti na kupiga kelele:

34Acha! Tuko na jambo gani sisi na wewe, Yesu wa Nasareti? Umekuja kutuangamiza. Nakujua, kama u nani; ndiwe Mtakatifu wa Mungu.

35Yesu alipomkaripia akisema: Nyamaza, umtoke! ndipo, yule pepo alipomkumba, aanguke katikati, kisha akamtoka pasipo kumwumiza.

36Wote wakaingiwa na kituko, wakasemezana wao kwa wao wakiuliza: Neno gani hilo? Anawaagiza pepo wachafu kwa nguvu ya kifalme, nao hutoka!

37Huo uvumi wake ukatoka, ukafika po pote penye nchi zilizoko pembenipembeni.

Mkwewe Simoni.

(38-44: Mat. 8:14-17; Mar. 1:29-39.)

38Alipoondoka nyumbani mwa kuombea akaingia nyumbani mwa Simoni. Naye mama ya mkewe Simoni alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwombea kwake.

39Akaja, akasimama kichwani pake, akaikaripia homa; ndipo, ilipomwacha. Papo hapo akainuka kitandani, akawatumikia.

40Jua lilipokuchwa, wakaja wote waliokuwa na wanyonge wa magonjwa menginemengine, wakiwaleta kwake; akawaponya kwa kuwabandikia mikono kila mmoja.

41Hata pepo wakatoka wengi wakipiga kelele na kusema: Wewe ndiwe Mwana wa Mungu. Lakini akawakaripia, akawakataza kusema, ya kuwa walimjua kuwa yeye ni Kristo.[#Mat. 8:29; Mar. 3:11-12.]

42Lakini kulipokucha, akatoka, akaenda mahali palipokuwa pasipo watu. Ndipo, makundi ya watu walipomtafuta, wakaja kwake, wakamzuia, asiondoke kwao.

43Lakini akawaambia: Inanipasa kuipigia hata miji mingine mbiu njema ya ufalme wa Mungu, kwani hiyo ndiyo, niliyotumiwa.[#Luk. 8:1.]

44Kisha akawa akiipiga hiyo mbiu katika nyumba za kuombea zilizoko Galilea.[#Mat. 4:23.]

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania