The chat will start when you send the first message.
1*Ikawa, kundi la watu lilipomsonga na kulisikia Neno la Mungu, alikuwa amesimama ufukoni pa ziwa la Genesareti,
2akaona vyombo viwili, vimekaa ufukoni, nao wavuvi walikuwa wameshuka wakiziosha nyavu zao.
3Ndipo, alipoingia katika chombo kimoja kilichokuwa cha Simoni, akamwomba, akisogeze mbali kidogo hapo ufukoni. Akakaa katika chombo akiwafundisha makundi ya watu.
4Alipokwisha kusema nao akamwambia Simoni: Peleka chombo kilindini, mzishushe nyavu zetu mvue samaki![#Yoh. 21:6.]
5Simoni akajibu akisema: Bwana, usiku kucha tumesumbuka kwa kazi, tusipate kitu; lakini kwa agizo lako wewe nitazishusha nyavu.
6Walipovifanya hivyo wakakamata samaki wengi sana, nyavu zao zikakatikakatika.
7Ndipo, walipowapungia wenzi wao waliokuwa katika chombo kingine, waje kuwasaidia, nao wakaja, wakavijaza vyombo vyote viwili, vikafikia kuzama.
8Simoni Petero alipoyaona hayo akampigia Yesu magoti, akasema: Ondoka kwangu, Bwana! kwani mimi ni mtu mkosaji.
9Kwani kituko kilikuwa kimemshika yeye nao wote waliokuwa pamoja naye, kwa hivyo, walivyokamata samaki wengi;
10akina Yakobo na Yohana, wana wa Zebedeo, ndio waliokuwa wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni: Usiogope! Toka sasa utakuwa ukivua watu.[#Mat. 13:47.]
11Walipokwisha kuvipeleka vyombo uvukoni, wakayaacha yote wakamfuata yeye*[#Mat. 19:27.]
12Ikawa, alipokuwa kule kwenye miji ile, mara kulikuwako mtu aliyeenezwa mwili wote na ukoma. Naye alipomwona Yesu akamwangukia kifudifudi, akamwomba akisema: Bwana, ukitaka waweza kunitakasa.
13Ndipo, aliponyosha mkono, akamgusa akisema: Nataka, utakaswe. Mara ukoma ukamwondoka.
14Kisha akamkataza, asimwambie mtu neno, akasema: Uende zako, ujionyeshe kwa mtambikaji, utoe kipaji kwa ajili ya kutakaswa kwako, kama Mose alivyoagiza, kije kinishuhudie kwao![#3 Mose 14:2-32.]
15Lakini uvumi wake ukafuliza kuendelea, wakakusanyika makundi ya watu wengi, wamsikilize wakiponywa magonjwa yao.
16Lakini yeye akajiepua, akaenda mahali palipokuwa pasipo watu, akawapo akiomba.[#Mar. 1:35.]
17Ikawa siku moja, alipokuwa akifundisha, wakakaa naye Mafariseo na wafunzi wa Maonyo waliokuwa wametoka kila mji wa Galilea na Yudea na Yerusalemu. Nayo nguvu ya Mungu ilikuwa naye ya kuponya wagonjwa.
18Papo hapo wakaja watu wakileta mtu aliyelala kitandani mwenye ugonjwa wa kupooza. Wakajaribu kumwingiza nyumbani na kumweka mbele yake.
19Wasipoona pa kumwingizia kwa ajili ya watu wengi wakapanda katika paa la nyumba, wakafumua vigae, wakamshusha hapo pamoja na kitanda chake, wakamweka katikati mbele ya Yesu.
20Alipoona, walivyomtegemea, akasema: Mwenzangu, umeondolewa makosa yako.
21Ndipo, waandishi na Mafariseo walipoanza kuwaza wakisema: Nani huyu anayesema maneno ya kumbeza Mungu? Yuko nani awezaye kuondoa makosa? Siye Mungu peke yake tu?[#Yes. 43:25.]
22Kwa kuyatambua hayo mawazo yao Yesu akajibu akiwaambia: Mnawaza nini mioyoni mwenu?
23Kilicho chepesi ni kipi? kusema: Umeondolewa makosa yako! au kusema: Inuka, uende?
24Lakini kusudi mpate kujua, ya kuwa Mwana wa mtu ana nguvu ya kuondoa makosa nchini, akamwambia mwenye kupooza: Nakuambia: Inuka, jitwishe kitanda chako, uende nyumbani kwako!
25Papo hapo akainuka machoni pao, akajitwisha kitanda, alichokilalia, akaenda nyumbani kwake akimtukuza Mungu.
26Ndipo, wote walipostuka sana, wakamtukuza Mungu, wakashikwa na woga mwingi wakisema: Utukufu, tuliouona leo, sio wa kuujua.
27Kisha alipotoka kwenda zake akaona mtoza kodi, amekaa forodhani, jina lake Lawi. Akamwambia: Nifuata!
28Naye akayaacha yote, akainuka, akamfuata.
29Kisha Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake, mkawamo na kundi jingi la watoza kodi na wengine, wakakaa chakulani pamoja nao.[#Luk. 15:1.]
30Mafariseo na waandishi wao wakanung'unika, wakawaambia wanafunzi wake: Kwa nini mnakula, tena mnakunywa pamoja na watoza kodi na wakosaji?
31Yesu akajibu akiwaambia: Walio wazima hawapaswi na mganga, ila walio wagonjwa.
32Sikujia kuwaita waongofu, ila wakosaji, wajute.
33Kisha wakamwambia: Wanafunzi wa Yohana hukaza kufunga na kuomba, vilevile nao wanafunzi wa Mafariseo, lakini wanafunzi wako hula, hunywa.
34Yesu akawaambia: Hamwezi kuwafungisha walioalikwa arusini, bwana arusi akingali pamoja nao.
35Lakini siku zitakuja, watakapoondolewa bwana arusi; siku zile ndipo, watakapofunga.
36Kisha akawaambia mfano, ya kuwa hakuna mtu akataye kiraka cha nguo mpya na kukitia katika kanzu chakavu. Kama anafanya hivyo, anaikata ile mpya, nacho kiraka cha nguo mpya hakipatani na ile chakavu.
37Wala hakuna mtu anayetia mvinyo mpya katika viriba vichakavu; kwani akiitia mle, mvinyo mpya itavipasua viriba, nayo yenyewe itamwagika, navyo viriba vitaangamia.
38Ila mvinyo mpya hutiwa katika viriba vipya.
39Wala hakuna aliyekunywa mvinyo ya kale, akitaka mpya, kwani husema: ile ya kale ndiyo nzuri.