The chat will start when you send the first message.
1Mtaniona, nikimtuma mjumbe wangu, atengeneze njia mbele yangu. Yule Bwana, mnayemtafuta, atakuja kutokea Jumbani mwake, msipomwazia. Naye mjumbe wa agano anayewapendeza mtamwona, anavyokuja; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.[#Mat. 11:10; Mar. 1:2; Luk. 1:17.]
2Lakini yuko nani atakayeivumilia siku ya kuja kwake? Tena yuko nani atakayesimama, atakapoonekana? Kwani yeye ni kama moto wa mwenye kuyeyusha fedha au kama sabuni ya wafua nguo.[#Yes. 1:25.]
3Naye atakaa akiyeyusha fedha, aitakase; ndivyo, atakavyowatakasa wana wa Lawi, awang'aze, wawe kama dhahabu au fedha, wapate kumpelekea Bwana vipaji vya tambiko kwa wongofu.[#Zak. 13:9.]
4Ndipo, vipaji vya tambiko vya Yuda na vya Yerusalemu vitakapompendeza Bwana kama katika siku za kale na kama katika miaka iliyopita zamani.
5Hapo ndipo, nitakapowatokea kukata mashauri, nami nitakuwa shahidi wa kuwasuta wachawi na wavunja unyumba, nao waapao viapo vya uwongo, nao wawanyimao wakibarua mshahara, nao wakorofishao wajane hata waliofiwa na wazazi, nao wapotoao wageni pasipo kuniogopa mimi; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.*
6Kwani mimi Bwana sikugeuka, nanyi hamkukoma kuwa wana wa Yakobo.
7Tangu siku za baba zenu mmeyaacha maongozi yangu, hamkuyashika, myaangalie. Rudini kwangu! Ndipo, nami nitakaporudi kwenu; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema. Nanyi mnauliza: Turudi kwa njia gani?[#Zak. 1:3.]
8Je? Mtu anaweza kumnyima Mungu yaliyo yake? Kwani ninyi mnaninyima yaliyo yangu, mkisema: Tumekunyima namna gani yaliyo yako? Ni mafungu ya kumi na vipaji vya kupatolea Patakatifu.
9Ninyi mmekwisha kuapizwa kwa kiapizo, tena ninyi mmeninyima yaliyo yangu, taifa hili lote.[#Hag. 1:6.]
10Yapelekeni mafungu yote ya kumi mle nyumbani, kilimbiko kilimo, yawe vilaji vya Nyumbani mwangu! Kanijaribuni hivyo, kama sitawafunulia madirisha ya mbinguni, nikiwamwagia mbaraka isiyopimika kwa kufurika; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.
11Ndipo, nitakapowakemea walafi kwa ajili yenu, wasiwaangamizie mazao ya nchi, wala mizabibu yenu iliyoko mashambani isikose matunda; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.
12Ndipo, wamizimu wote watakapowatukuza kuwa wenye shangwe, kwani mtakuwa nchi ipendezayo; ndivyo, Bwana Mwenye vikosi anavyosema.
13Maneno yenu, mliyoyasema kwa ajili yangu, yamekuwa magumu; ndivyo, Bwana anavyosema, nanyi mkauliza: Tumesema nini kwa ajili yako wewe?
14Mmesema: Ni bure kumtumikia Mungu, tumejipatia nini kwa kuyaangalia maagizo yake yaliyotupasa kuyaangalia na kwa kumwendea Bwana Mwenye vikosi na kuvaa nguo za matanga?[#Sh. 73:13-14.]
15Kwa hiyo sasa tunawawazia wao wasiomkumbuka Mungu kuwa wenye shangwe, hata wao wasiomcha Mungu wamejengwa, napo hapo, walipomjaribu Mungu, wamepona.
16Hapo, wamchao Bwana walipoongeana kila mtu na mwenziwe, Bwana alitega sikio, akasikiliza; mbele yake kikaandikwa kitabu cha ukumbusho wao waliomcha Bwana na kulikumbuka Jina lake.
17Ndivyo, Bwana Mwenye vikosi asemavyo: Hao watakuwa wangu mimi mwenyewe siku hiyo nitakayoifanya mimi, nami nitawahurumia, kama mtu anavyomhurumia mwanawe aliyemtumikia.[#2 Mose 19:5.]
18Hapo ndipo, mtakapoona tena, ya kuwa wanapambanuka amchaye Bwana naye asiyemcha, tena amtumikiaye Mungu naye asiyemtumikia.