Marko 11

Kuingia Yerusalemu.

(1-10: Mat. 21:1-9; Luk. 19:29-38; Yoh. 12:12-16.)

1Hapo, walipoukaribia Yerusalemu na kufika Beti-Fage na Betania penye mlima wa michekele, akatuma wanafunzi wake wawili,

2akawaambia: Nendeni katika kijiji kinachowaelekea! Mtakapoingia mle mara mtaona, pamefungwa mwana punda, ambaye mtu hajampanda bado; mfungueni, mmlete!

3Kama mtu atawauliza: Mbona mnafanya hivi? semeni: Bwana wetu anamtakia kazi! Mara atawapani, mmlete hapa.[#Mar. 14:14.]

4Walipoondoka kwenda, wakamwona mwana punda aliyefungwa mlangoni nje njiani, wakamfungua.

5Wengine waliosimama huko wakawauliza: Mnafanya nini mkimfungua mwana punda?

6Nao wakajibu, kama Yesu alivyowaambia; ndipo, walipowaacha.

7Wakampeleka mwana punda kwa Yesu, wakatandika nguo zao upesiupesi juu yake, kisha akampanda.

8Watu wengi wakatandika nguo zao njiani, wengine wakatandika matawi ya miti, waliyoyakata mashambani.

9Nao waliotangulia nao waliofuata wakapaza sauti:

Hosiana!

10Na atukuzwe ajaye kwa jina la Bwana!

Utukuzwe ufalme wa baba yetu Dawidi utujiao!

Hosiana juu mbinguni!

(11-24: Mat. 21:12-22; Luk. 19:45-48.)

11Alipoingia Yerusalemu, akaenda Patakatifu. Alipokwisha kuvitazama vyote vilivyomo, mchana ukawa umekuchwa; kwa hiyo akatoka kwenda Betania pamoja na wale kumi na wawili.

Mkuyu unaapizwa.

12Kesho yake walipotoka Betania akaona njaa.[#Luk. 13:6-9.]

13Huko mbali akaona mkuyu wenye majani, akaenda, aone, kama liko tunda juu yake. Akaufikia, asione kitu, ila majani tu, kwani siku za kuyu hazijawa.

14Ndipo, alipotoa neno la kwamba: Kale na kale mtu asile tena kwako tunda! Wanafunzi wake wakayasikia.[#Mar. 11:20.]

Kuwafukuza wachuuzi Patakatifu.

15Walipofika Yerusalemu, akapaingia Patakatifu, akaanza kuwafukuza wenye kuuzia na kununulia hapo Patakatifu, akaziangusha meza za wavunja fedha na viti vya wachuuzi wa njiwa.

16Tena hakuacha, mwenye kuchukua chombo apapitie hapo Patakatifu.

17Akawafundisha akiwaambia: Haikuandikwa ya kuwa: Nyumba yangu itaitwa nyumba ya kuombea kwao makabila yote ya watu? Lakini ninyi mmeigeuza kuwa pango la wanyang'anyi.[#Yes. 56:7; Yer. 7:11.]

18Watambikaji wakuu na waandishi walipoyasikia, wakatafuta, watakavyomwangamiza, kwani walimwogopa, kwa sababu watu wote pia walishangazwa na mafundisho yake.

19Lakini kila siku ilipokuwa jioni, wakatoka mjini.

Mkuyu ulipoapizwa.

20Asubuhi walipopita wakauona mkuyu, umekuwa umekauka toka mizizini.[#Mar. 11:14.]

21Petero akalikumbuka neno lile, akamwambia: Bwana, tazama, mkuyu, uliouapiza, umenyauka.

22Yesu akawajibu akisema: Mwe wenye kumtegemea Mungu![#Yoh. 14:1.]

23Kweli nawaambiani: Kila atakayeuambia mlima huu: Ondoka hapa, ulipo, ujitupe baharini! basi, litatimia vivyo hivyo, asipokuwa na mashaka moyoni mwake, ila akiwa anayategemea tu ya kuwa: Analolisema, litatendeka.[#Mat. 17:20; Luk. 17:6.]

24Kwa hiyo nawaambiani: Yo yote mnayoyaomba kwa kuyataka, yategemeeni tu, ya kuwa mtayapata! ndipo, mtakapoyapata kweli.[#Mat. 7:7; Yoh. 14:13; 16:23.]

25Nanyi mtakaposimama na kuomba mwondoleane, mkiwa mnamwekea mtu mfundo, Baba yenu alioko mbinguni naye awaondolee ninyi makosa yenu![#Mat. 5:23.]

26Lakini ninyi msipoondoleana, naye Baba alioko mbinguni hatawaondolea makosa yenu.[#Mat. 6:14-15.]

Ubatizo wa Yohana.

(27-33: Mat. 21:23-27; Luk. 20:1-8.)

27Walipoingia tena Yerusalemu, naye alipotembea Patakatifu, wakamjia watambikaji wakuu na waandishi na wazee,

28wakamwuliza: Hayo unayafanya kwa nguvu gani? au ni nani aliyekupa nguvu hii, uyafanye hayo?

29Yesu akawaambia: Nanyi nitawauliza neno moja; mtakaponijibu, nitawaelezea nguvu yangu ya kuyafanya hayo.

30Ubatizo wake Yohana ulitoka mbinguni au kwa watu? Nijibuni!

31Wakafikiri mioyoni mwao kwamba: Tukisema: Ulitoka mbinguni, atatuuliza: Mbona hamkumtegemea?

32Lakini tukisema: Ulitoka kwa watu, basi, waliwaogopa watu; kwani watu wote walimshika Yohana kuwa mfumbuaji wa kweli.

33Kwa hiyo wakamjibu Yesu wakisema: hatujui. Ndipo, Yesu alipowaambia: Basi, hata mimi siwaambii nguvu inayonifanyisha hayo.

Swahili Roehl Bible 1937 © Bible Society of Tanzania, 1937.
Published by: Bible Society of Tanzania