The chat will start when you send the first message.
1Ndipo, watu wote pia walipokusanyika kama mtu mmoja katika uwanja ulioko mbele ya lango la Maji, wakamwambia mwandishi Ezera, alete kitabu cha Maonyo ya Mose, Mungu aliyowaagiza Waisiraeli.[#Ezr. 7:6.]
2Mtambikaji Ezera akayaleta Maonyo, akayaweka mbele ya huo mkutano, kwani walikuja waume kwa wake na wote walioweza kusikia na kutambua maana, ikawa siku ya kwanza ya mwezi wa saba.[#5 Mose 31:10-13.]
3Pale penye uwanja ulioko mbele ya lango la Maji akawasomea yaliyomo kitabuni, akaanza asubuhi, akamaliza, jua lilipokuwa kichwani, wakawako waume na wake na watambuzi, nao watu wote pia, wakakisikiliza hicho kitabu cha Maonyo.
4Hapo mwandishi Ezera alikuwa akisimama juu ya ulingo wa miti, walioutengeneza kwa ajili ya hili jambo, kando yake kuumeni kwake wakasimama Matitia na Sema na Anaya na Uria na Hilkia na Masea, tena kushotoni kwake Pedaya na Misaeli na Malkia na Hasumu nao Hasibadana, Zakaria na Mesulamu.
5Ezera akakifunua kitabu machoni pao watu wote, kwa kuwa alikuwa juu kuliko watu wote, napo hapo, alipokifunua, watu wote wakainuka.
6Ezera akamtukuza Bwana aliye Mungu mkubwa, nao watu wakamwitikia: Amin! Amin! na kuiinua mikono yao; kisha wakainama, wakamwangukia Bwana na kuzielekeza nyuso chini.
7Kisha Yesua na Bani na Serebia, tena Yamini, Akubu, Sabutai, Hodia, Masea, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani, Pelaya na Walawi wakawatambulisha watu haya Maonyo, watu wakiwa wamesimama papo hapo.
8Wakawasomea katika kitabu cha Maonyo ya Mungu kwa sauti kuu na kuyaeleza vema; hivyo watu waliyatambua maana papo hapo, yaliposomwa.
9Ndipo, Nehemia aliyekuwa mtawala nchi na Ezera aliyekuwa mtambikaji na mwandishi nao Walawi waliowatambulisha watu maana walipowaambia watu: Siku hii ya leo ni siku takatifu ya Bwana Mungu wenu! Msiomboleze, wala msilie machozi! Kwani watu wote walilia machozi walipoyasikia maneno ya Maonyo.[#Neh. 5:14.]
10Akaendelea akiwaambia: Haya! Nendeni, mle vinono pamoja na kunywa vinywaji vitamu! Nao wakosao vya kujiandalia wapelekeeni magawio! Kwani siku ya leo ni siku takatifu ya Mungu wetu. Kwa hiyo msisikitike! Kwani kumfurahia Bwana ndiko kunakowapa nguvu.
11Walawi wakawatuliza watu wote mioyo wakiwaambia: Nyamazeni! Kwani siku hii ni takatifu, kwa hiyo msisikitike.
12Ndipo, watu wote walipokwenda, wale, wanywe, wapeleke magawio, wafanye sikukuu yenye furaha kubwa, kwa kuwa waliyatambua hayo maneno, waliyojulishwa.
13Siku ya pili wakuu wa milango ya watu wote na watambikaji na Walawi wakakusanyika kwa mwandishi Ezera, wajifundishe vema maneno ya Maonyo.
14Wakaona palipoandikwa katika Maonyo, ya kuwa Bwana alimwagiza Mose kuwaambia wana wa Isiraeli, penye sikukuu ya mwezi wa saba wakae katika vibanda,[#3 Mose 23:42.]
15wapige mbiu na kutangaza po pote penye miji yao namo Yerusalemu kwamba: Tokeni kwenda milimani, mlete matawi ya michekele na makuti ya michikichi na matawi ya vihagilo na makuti ya mitende na matawi ya miti yo yote yenye majani mengi, mpate kujenga vibanda, kama ilivyoandikwa!
16Ndipo, watu walipotoka, wakaleta matawi, wakajijengea vibanda kila mtu juu darini kwake napo penye nyua zao napo penye ua wa Nyumba ya Mungu napo penye uwanja ulioko kwenye lango la Maji napo penye uwanja ulioko kwenye lango la Efuraimu.[#Neh. 8:1.]
17Hivyo mkutano wao wote waliorudi mafungoni kwenye kutekwa wakajijengea vibanda, wakakaa vibandani; kwani tangu siku za Yosua, mwana wa Nuni, mpaka siku hiyo wana wa Isiraeli hawakufanya hivyo, ikawa furaha kubwa sana.
18Wakasoma katika kitabu cha Maonyo ya Mungu siku kwa siku, tangu siku ya kwanza hata siku ya mwisho. Wakafanya sikukuu siku saba, lakini siku ya nane pakawa na kusanyiko kuu, kama ilivyopasa.