The chat will start when you send the first message.
1Werevu wa kweli wa wanawake huzijenga nyumba zao,
lakini ujinga wao huzibomoa kwa mikono yao wenyewe.
2Ashikaye njia inyokayo humcha Bwana,
lakini azipotoaye njia zake humbeza.
3Kinywani mwa mjinga imo fimbo ya majivuno,
lakini midomo ya werevu wa kweli huwalinda.
4Pasipo ng'ombe zizi hukaa likiwa safi,
lakini mapato huwa mengi, nguvu za ng'ombe zinapotumiwa.
5Shahidi mwenye kweli haongopi,
asemaye maneno ya uwongo ni shahidi mwenye uwongo.
6Mfyozaji akitafuta werevu wa kweli haupati,
lakini mtambuzi hupata upesi kujua maana.
7Toka kwa mtu aliye mjinga!
Kwani kwake huoni midomo ijuayo maana.
8Werevu wa kweli wa mtu aerevukaye humtambulisha njia yake,
lakini ujinga wa wapumbavu huwadanganya.
9Wajinga hufyoza wakikora manza,
lakini wanyokao hupendezana.
10Moyo wenyewe hujua uchungu wa roho yake,
hata katika furaha yake mwingine hajitii humo.
11Nyumba zao wasiomcha Mungu hubomolewa,
lakini mahema yao wanyokao yatachanua.
12Ziko njia zinyokazo machoni pa watu,
lakini mwisho wao huenda kufani.
13Hata ukicheka, moyo unaweza kuumia,
mara nyingi mwisho wa furaha ni majonzi.
14Moyo ukirudi nyuma, mtu hushibishwa mapato ya njia zake,
naye mtu mwema huyapata, aliyoyasumbukia.
15Mjinga huitikia maneno yote,
lakini aerevukaye hupatambua, anapokwenda.
16Mwerevu wa kweli huogopa, huepuka penye mabaya,
lakini mjinga huchafuka, kisha huwaza, ya kuwa mambo yametulia.
17Mwenye moyo mdogo hufanya yenye ujinga,
naye mwenye mawazo mabaya huchukiwa.
18Wasiojua kitu hujipatia ujinga, uwe fungu lao,
lakini waerevukao huvikwa vilemba vya ujuzi.
19Wabaya sharti wawainamie wema,
nao wasiomcha Mungu sharti wasimame milangoni pao waongofu.
20Hata rafiki yake humchukia maskini,
lakini wampendao mwenye mali ni wengi.
21Amwendeaye mwenziwe na kumbeza hukosa,
lakini awahurumiaye wanyonge ni mwenye shangwe.
22Je? Wawazao mabaya hawapotei?
Lakini wawazao mema hujipatia upendeleo wa kweli.
23Masumbuko yote yako na mapato,
lakini yaliyo maneno matupu ya midomo huleta ukosefu tu.
24Kwao werevu wa kweli mali zao ni kama kilemba,
lakini ujinga wa wapumbavu huwa ujinga.
25Shahidi mwenye kweli huponya roho za watu,
lakini asemaye uwongo huziponza.
26Mtu akimcha Bwana analo egemeo lenye nguvu,
nao wanawe wanapo pao pa kukimbilia.
27Kumcha Bwana ni kisima cha uzima,
tena ni kuondoka penye matanzi ya kifo.
28Utukufu wa mfalme umo katika wingi wa watu,
lakini watu wanapokwisha, mkuu wao huangamia.
29Mvumilivu anao utambuzi mwingi,
lakini mwenye moyo mdogo hukuza ujinga.
30Moyo mpole ni uzima wa mwili,
lakini wivu ni kama ugonjwa wa ubovu mifupani.
31Akorofishaye mnyonge humsimanga aliyemwumba,
lakini amheshimuye humhurumia mkiwa.
32Kwa ubaya wake asiyemcha Mungu hukumbwa, aanguke,
lakini mwongofu hata kufani yuko na kimbilio lake.
33Moyoni mwa mtambuzi ndimo, werevu wa kweli unamotua,
lakini yaliyomo mioyoni mwa wapumbavu hujulikana.
34Wongofu hukuza taifa,
lakini ukosaji hutweza makabila mazima.
35Mfalme hupendezwa na mtumishi mwenye akili,
lakini humkasirikia sana anayemtweza.