The chat will start when you send the first message.
1Wasiomcha Mungu hukimbia pasipo kufukuzwa,
lakini waongofu hutulia pasipo kustushwa kama mwana wa simba.
2Kwa ajili ya mapotovu ya nchi wakuu wake huwa wengi,
lakini mtambuzi mwenye akili huitengemanisha siku nyingi.
3Mtu akosaye mali akikorofisha wanyonge,
ni mvua ifurikayo pasipo kuleta chakula.
4Wayaachao Maonyo huwasifu wasiomcha Mungu,
lakini wayaangaliao Maonyo huwakasirisha sana.
5Watu wabaya hawatambui mashauri yaliyo sawa,
lakini wamtafutao Bwana huyatambua yote.
6Maskini ashikaye njia yake pasipo kukosa ni mwema
kuliko apotoaye njia zake akipata mali nyingi.
7Ayashikaye Maonyo ni mwana wa mtambuzi,
lakini aliye mwenzao walafi humtia baba yake soni.
8Ajipatiaye mali kwa kukopesha na kutaka faida nyingi
huzikusanyia mwingine atakayezigawia wanyonge.
9Ayageuzaye masikio, yasisikie Maonyo,
akimwomba Mungu hutapisha.
10Apotezaye waongofu, washike njia mbaya,
hutumbukia mwenyewe katika shimo lake,
lakini wasiokosa watapata mema, yawe mafungu yao.
11Mtu mkwasi ni mwerevu wa kweli machoni pake yeye,
lakini mnyonge mwenye utambuzi humchunguza.
12Waongofu wakishangilia, uko utukufu mwingi,
lakini wasiomcha Mungu wakipata ukuu, watu hujificha.
13Ayafichaye mpotovu yake hatafanikiwa,
ayaungamaye na kuyaacha atahurumiwa.
14Mwenye shangwe ni mtu ajiangaliaye pasipo kukoma,
lakini aushupazaye moyo wake huangushwa na mabaya.
15Simba angurumaye na chui atamaniye kula
ni mtu asiyemcha Mungu akitawala watu wanyonge.
16Mkuu akosaye utambuzi huwakorofisha watu sana,
lakini achukiaye mapato ya upotovu hukaa siku nyingi.
17Mtu alemewaye moyoni na damu ya mtu, aliyemwua,
hutangatanga hata kuingia shimoni, asione wamshikizao.
18Aendeleaye pasipo kukosa huokoka,
lakini ajipotoaye kwa kushika njia mbili, mara huanguka katika moja.
19Alilimiaye shamba lake hushiba chakula,
lakini akimbiliaye mambo ya bure hushiba ukosefu.
20Mtu mwenye kweli hupata mbaraka nyingi,
lakini ajihimizaye kupata upesi mali nyingi hakosi kukora manza.
21Kuzitazama nyuso za watu hakufai,
lakini wako wajikoseshao kwa ajili ya kitonge cha wali.
22Ajikazaye sana kupata mali nyingi huwa mwenye jicho baya,
hajui, ya kuwa ukosefu utamjia.
23Amwonyaye mtu mwisho atashukuriwa
kuliko asemaye mororo kwa ulimi wake.
24Apokonyaye mali za baba na za mama na kusema: Huku siko kukosa,
yeye ni sawa na mtu aangamizaye vibaya.
25Aliye na roho yenye tamaa nyingi huzusha magomvi,
lakini amwegemeaye Bwana hushibishwa sana.
26Auegemeaye moyo wake yeye ni mpumbavu,
lakini aendeleaye kwa werevu wa kweli yeye hupona.
27Amgawiaye mkosefu hataona ukosefu,
lakini ayafumbaye macho yake huapizwa kabisa.
28Wasiomcha Mungu wakipata ukuu, watu hujificha,
lakini wakiangamia, waongofu huongezeka.