The chat will start when you send the first message.
1Kisha nikasikia uvumi mkuu kama wa makundi mengi ya watu waliomo mbinguni, wakisema:
Haleluya! Wokovu na utukufu na uwezo ni wa Mungu wetu,
2kwani hukumu zake ni za kweli na za wongofu.
Kwani amemhukumu yule mgoni mkuu wa kike aliyeiangamiza
nchi kwa ugoni wake, akamlipiza damu za watumwa
wake waliouawa na mkono wake yeye.
3Wakasema mara ya pili: Haleluya! Moshi wake hupanda juu kale na kale pasipo mwisho.[#Yes. 34:10.]
4Ndipo, wale wazee 24 nao wale nyama wanne walipoanguka chini na kumsujudia Mungu aliyekaa kitini mwa kifalme wakisema: Amin, Haleluya![#Ufu. 5:14; Sh. 106:48.]
5Sauti ikatoka kitini mwa kifalme ikisema: Mvumisheni Mungu wetu, enyi watumwa wake nyote mnaomwogopa yeye, mlio wadogo na wakubwa!
6Nikasikia uvumi kama wa makundi mengi na kama uvumi wa maji mengi na kama uvumi wa ngurumo yenye nguvu wa kwamba:
Haleluya! Kwani mfalme ni Bwana Mungu wetu
aliye Mwenyezi.
7Tushangilie na kupiga vigelegele
na kumtukuza yeye! Kwani ndoa ya Mwana kondoo
imefika, naye mkewe amejitengeneza,
8akapewa kuvaa nguo za bafta zing'aazo na kumetuka.
Maana hizi nguo za bafta ndio wongofu, watakatifu
waliopewa.
9Akaniambia: Andika! Wenye shangwe ndio walioitiwa vyakula vya arusi ya Mwana kondoo. Akaniambia: Maneno haya ni yake Mungu kweli.[#Luk. 14:15.]
10Nikaanguka miguuni pake, nimsujudie. Ndipo, aliponiambia: Angalia, sivyo! Mimi ni mtumwa mwenzenu wewe na ndugu zako walioushika ushuhuda wa Yesu; umwangukie Mungu! Kwani ule ushuhuda wa Yesu ndio Roho ya ufumbuaji.[#Ufu. 12:17; 22:8-9; Tume. 10:25-26.]
11Kisha nikaziona mbingu, zikifunuka, nikaona farasi mweupe; mwenye kumpanda anaitwa mwelekevu na mkweli, maana huamua kwa wongofu wa kuupigia vita.[#Ufu. 1:5; 3:14; 6:2; Yes. 11:4-5; Mat. 24:30.]
12Macho yake ni moto unaowaka, kichwani pake anavyo vilemba vingi vya kifalme. Analo jina, aliloandikwa; hakuna aliyelijua pasipo yeye mwenyewe.[#Ufu. 1:14; 2:18; 3:12.]
13Amevaa nguo iliyochovywa katika damu. Jina lake huitwa Neno la Mungu.[#Yes. 63:1-2; Yoh. 1:1.]
14Makundi ya mbinguni yakafuatana naye, wakiwa wamepanda farasi weupe waliovikwa nguo za bafta zing'aazo na kumetuka.[#Ufu. 17:14.]
15Kinywani mwake mkatoka upanga mkali wa kuwapiga wamizimu akiwachunga kwa fimbo ya chuma. Yeye ndiye atakayekamua kamulioni mwenye mvinyo chungu ya makali ya Mungu Mwenyezi.[#Ufu. 12:5; 14:19-20; Sh. 2:9; Yes. 63:3.]
16Naye alikuwa ameandikwa jina katika nguo yake penye kiuno: MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA.[#Ufu. 17:14; 1 Tim. 6:15.]
17Kisha nikaona malaika mmoja aliyesimama katika jua na kupaza sauti kuu akiwaambia ndege wote warukao mbinguni kati: Njoni, mkusanyikie vyakula vingi vya Mungu,[#Ez. 39:4,17-20.]
18mpate kula nyama za miili ya wafalme na nyama za miili ya wakuu na nyama za miili ya wanguvu na nyama za miili ya farasi na ya wale waliowapanda na nyama za miili yawaungwana na ya watumwa wote walio wadogo na wakubwa!
19Nikamwona yule nyama na wafalme wa nchini na vikosi vyao vikikusanyika, wampelekee vita yeye aliyempanda yule farasi na makundi yake.[#Ufu. 16:14,16; 17:12-14; 19:11.]
20Ndipo, yule nyama alipokamatwa pamoja na mfumbuaji wa uwongo; ni yule aliyevifanya vielekezo mbele yake vya kuwapoteza navyo wale waliojitia chapa cha yule nyama nao waliokiangukia kinyago chake. Wakingali wa hai hao wawili wakatupwa ziwani mwenye moto uwakao kwa nguvu za viberitiberiti vilivyomo.[#Ufu. 13:1,11-17; 20:10; Dan. 7:10,26.]
21Nao waliosalia wakauawa kwa upanga uliotoka kinywani mwake yeye aliyempanda yule farasi. Nao ndege wote wakashiba nyama za miili yao.